MZEE ABOMOA NYUMBA ZAKE KUWAKOMOA WANAOVIZIA KURITHI

 

 

MZEE , Iddy Nzella Maganga, (89)  ameamua kuzivunja nyumba  zake mbili zenye thamani ya zaidi ya shilingi 200 milioni kwa madai kuwa baadhi ya watoto wake wana nia ovu juu ya nyumba hizo kwani wamekuwa wakimtesa kwa lengo la  kumdhulumu  mali hizo.

 

Amesema  uamuzi huo ameuchukua akiwa na akili timamu na amefanya  ili kuwakomesha watoto wasiotaka kufanyakazi wakisubiri mali za urithi .

 

 

Akiongea na waandishi wa habari JUali 12, 2022 nje ya nyumba hizo zilizopo maeneo ya Ngarenaro NHC jijini Arusha  mzee huyo alisema kuwa  watoto wake hao wa kiume wamekuwa wakimtesa  ikiwemo kumfungia kwenye chumba cha giza kwa wiki moja bila kumpa chakula hali iliyomazimu kula kunyesi.

 

 

Maganga ambaye alifiwa na mke wake wa ndoa , amesema kuwa alifikia uamuzi wa kuzivunja nyumba hizo  baada ya kubaini  baadhi ya watoto wake wakiongozwa na Abdalah Maganga  wanania ovu juu ya mali zake na huenda akafa siku sio nyingi .

 

 

"Hii nyumba ni mali yangu nilijenga na mke wangu ambaye kwa sasa ni marehemu, huyu mtoto Abdalah alinifungia ndani wiki moja nikiwa nakula kinyesi changu sijitambuli na nilikuja kuokolewa na mtoto wangu wa kike, anaiwa  Jasmin na mume wake baada ya kuvunja kitasa na kunitoa na kunipeleka hospitali, " alisema Mzee Maganga na kuongeza.

 

…Jirani yangu anaitwa mama Masawe ambaye nilikuwa nikienda kuchukua chakula kwake alimpigia simu mtoto wangu Jasmin na kumwambia kuwà mbona mzee Abdalah  haonekani siku ya nne akija kuchukua chakula ,ndipo Jasmin na mumewe walipokuja na kukuta Abdalah amenifungia ndani, ". 

 

AELEZA UKATILI ZAIDI  ALIOFANYIWA

 

Mzee Maganga   ambaye ana watoto sita, kwa sasa anaishi kwa mtoto wake, Jasmin maeneo ya Kwa Morombo ambapo amefafanua kuwa mtoto wake, Abdallah alikuwa na nia mbaya juu yake, kutaka afariki dunia ili ajimilikishe nyumba hiyo kinyume cha sheria.

 

Alisema licha ya kuwa hiyo nyumba hizo ni mali yake lakini Abdallah alikuwa hamruhusu  kuingia ndani  ya nyumba hizo hata pale anapokuwa akitafuta msaada kwa kijana huyo, alikuwa akifunga milango na geti la kuingilia ndani.

 

Hivyo Mzee Maganga aliwataka watoto wake, Abdallah na Riziki  kukaa mbali na mali zake, watafute mali zao kwani baada ya kufanikiwa kubomoa nyumba hiyo anampango wa kuliuza eneo hilo muda wowote kuanzia sasa.

 

"Baada ya kupata fahamu nilianza taratibu za kuuza nyumba  yangu lakini kila nikifika na mteja nafungiwa nje na mwanangu Abdallah  hataki niingie ndani hata kujisaidia,"alisema Mzee Maganga kwa uchungu.

 

Naye mtoto wa mzee huyo,  Jasmin  alisema kuwa alimwokoa baba yake akiwa kwenye hali mbaya baada ya kumkuta hajitambui na amefungiwa kwenye chumba kidogo kwa wiki moja bila kupatiwa chakula wala maji.

 

"Nilimkuta baba yangu akiwa kwenye hali mbaya sana alikuwa haongei, chumba kilikuwa na giza kimefungwa na kinanuka kinyesi na alikuwa akila kinyesi chake, nilimpeleka hospitali na baada ya kupatiwa matibabu alipata nafuu na kurejea katika hali ya kawaida na sasa naishi naye,"alisema Jasmin.

 MTOTO WAKE ASEMA ANAMWACHIA MUNGU

Kwa upande wake,  Abdallah  alikanusha madai yaliyotolewa na baba yake ya  kumfungia kwenye chumba kwa wiki nzima bila chakula huku akidai kuwa yeye anaishi kwenye nyumba hiyo kama mwangalizi mara baada ya mama yake kufariki huku akidai mahusiano na baba yake yalianza kudorora tokea alipoenda kuishi kwa  mdogo wake, Jasmini.

 

Alisema kuwa alishtushwa sana kuona kundi la watu zaidi ya 50 wakivamia nyumba hiyo siku ya jumamosi wiki iliyopita na kufanya uharibifu.

 

Abdallah alisema kuwa alijitahidi kutafuta msaada polisi lakini hakuupata kwa wakati kwani polisi walifika kwa kuchelewa na  kukuta tayari nyumba zote zimevunja na vitu kutolewa nje.

 

"Mimi sina ugomvi na baba yangu ila sina mawasiliano naye kwa muda baada ya kuchukuliwa na kuishi na mdogo wangu Jasmin, nitakachofanya kwa sasa ni kumwachia Mungu tu,"alisema Abdalah. 

 

Mdogo wake  Mzee Maganga, Hassan Abdalah,  alisema hana mawasiliano na kaka yake  ingawa alishauri kuwa kitendo kilichotokea kinapaswa kumalizika kisheria mahakamani.

 

Tukio hilo limekuwa gunzo kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha huku wengi wakionekana kuunga mkono hatua aliyochukua mzee Maganga kwa kile wanachoeleza kuwa kwa sasa vijana wengi hawataki kufanya kazi wamekaa wakivizia ni lini wazazi wao watakufa ili warithi mali.

 

Mkazi wa Terati, Thomas Laizer alisema kuwa afadhali wazee sasa wakaamka pale wanapoona vijana wanawaombea wafe ili warithi basi wauze mali zao na wazitumie taratibu mpaka hapo Mungu atakapowachukua.

 

Hata hivyo wananchi wengine walipinga kwa kile walichodai kuwa mwanadamu anapoishi inapendeza anapoondoka basi aache kwa familia kitu ambacho kitakuwa ukumbusho wa maisha yake hivyo mzee huyo angeweza kuchukua hatua nyingine kuwaadhibu vijana wake lakini si kuvunja nyumba.

 

0 Comments:

Post a Comment