WANANCHI WAFURIKA KUFUATULIA KESI YA MAUAJI YA LOLIONDO

UMATI Mkubwa wa watu umejitokeza mahakamani kufuatilia kesi ya mauaji inayowakabil watu 25 wakiwemo madiwani tisa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi,(CCM),  wilayani Ngorongoro, Ndirango Senge Laizer, wanaodaiwa kumuua askari polisi mwenye namba G 4200 Koplo Garlus Mwita.


Aidha  upande wa Jamhuri umebadili hati ya mashitaka ambapo kwa sasa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama ya mauaji na mauaji.


Pia mawakili wa utetezi 14 waliokuwa mahakamani hapo wakiongozwa na Jeremiah Mtobesya walikuja juu wakitaka upelelezi wa shauri hilo ukamilike mapema kwani miongoni mwa washitakiwa yupo  mwanafunzi anayepaswa kuendelea na masomo na mzee mwenye umri mkubwa. 

Wakili wa Serikali, Pendo Shemkole aliwasomea upya  mashitaka hayo leo Juni 30, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi, Herieth Mhenga wa mahakama ya hakimu Mkazi Arusha  anayesikiliza shauri hilo la mauaji namba 11/2022.

Alieleza mahakamani hapo kuwa kosa la kwanza ni kula njama ya mauaji ambalo linawaka ili washitakiwa wote ambapo wanadaiwa katika tarehe na sehemu isiyofahamika walipanga njama ya kuua maafisa wa serikali na polisi  waliokuwa wakishiriki kuweka mipaka kwenye Pori Tengefu la Loliondo.


Wakili wa Serikali Shemkole aliwasomea shitaka la pili la mauaji ambapo alieleza kuwa mnamo tarehe 10 Juni 2022 eneo la Ololosokwan wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa nia ovu walisababisha kifo cha askari polisi mwenye namba G 4200 Koplo Garnus Mwita.



Washitakiwa hao ni pamoja na Molongo Paschal, Albert Selembo,  Simeli Parmwati, (19) ambaye ni mwanafunzi, Lekayoko Parmwati, (21) Sapati Parmwati, (30) Ingoi Olkedenyi Kanjwel, (20) Sangau Morongeti, (Morijoi Parmati, (20) Morongeti Meeki, (Kambatai Lulu,(40) na  Moloimet Yohana,(37)?

Wengine ni  Ndirango Senge Laizer, (52) Joel Clemes Lessonu, (54)  Simon Nairiam Orosikiria, (59)  Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, (41) Luka Kursas, (49)  Taleng'o Twambei Leshoko, (37) Kijoolu Kakeya, (56)   Shengena Killel, (34) Kelvin Shaso Nairoti, (33)  Lekerenga Koyee, (68) Fred Victor (39) Wilsom Tiuwa Kiling, (32) na  James Mumes Taki (28)


Hakimu Mkazi Mhenga aliwaeleza washitakiwa hao hawapaswi kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza shauri hilo.

Wakili wa serikali Shemkole aliomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa hoja iliyomnyanyua wakili wa utetezi Mtobesya ambaye alieleza kuwa moja ya shitaka linalowakabili  wateja wao linataka wafikishwe mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika hivyo akataka upelelezi uharakishwe ili kesi ianze kusikilizwa.

"Miongoni mwa washitakiwa kuna ambao umri umesogea na mmoja ni mwanafunzi tunaomba upelelezi uende kwa haraka ili watu hawa waweze kusikilizwa. Pia ni haki ya kila mtu kupata 'speed trial' kwa sababu haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa ni rai yetu upelelezi uharakishwe washitakiwa wapate haki yao ya kusikilizwa," alieleza Mtobesya mahakamani hapo.


Mawakili wengine wa utetezi walioshirikiana na Mtobesya ni pamoja na Jebra Kambole, Joseph ole shangai, Peter Madeleka, Denis moses, Adolf Temba na  William Ernest.


Wengine ni Yonas Masiaya, Nicolas ole Seteu, Samaito Mollel, Julius john Lukumay, Ngeeyan Laizer, Deogratius Njau na John Lairumbe.

Shauri hilo limeahirishwa mpaka Julai 14, litapokuja kwa ajili ya kutajwa ambapo washitakiwa wote wamerejeshwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo kutoka na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

MABISHANO MAKALI YA KUSHERIA 

Awali yaliibuka mabishano makali ya kisheria wakati wakili wa serikali, Shemkole alipoiomba mahakama aweze kubadili hati ya mashitaka kwa kuongeza shitaka moja.

Ombi hilo lilimnyanyua wakili wa utetezi, Mtobesya ambaye alipinga hati hiyo ya mashitaka isifanyiwe marekebisho kwani marekebisho yanapaswa kufanywa wakati shauri lipo katika hatua za usikilizwaji huku akirejea vifungu mbalimbali vya sheria.


"Na inaweza kuwa kwa mahakama inayoweza kusikiliza haya makosa ambayo ni Mahakama Kuu kwa mujibu wa sheria endapo kunakuwa kuna shida kwenye 'charge sheet' inaweza kufanyiwa marekebisho sijui kwa nini wenzetu wameamua kubadili kwenye hatua ya sasa," alieleza Mtobesya huku akinukuu vifungu vya sheria.



Naye wakili mwingine wa Utetezi,  Madeleka  aliungana na Mtobesya kupinga kubadilishwa kwa hati hiyo huku akitaja vifungu vya sheria vinavyoeleza kuwa hati ya mashitaka itabadilishwa kama kesi itakuwa imefikia hatua ya kusikilizwa (trial)  ambayo ni hatua  mahakama inapokea vielelezo na kusikiliza mashahidi.

Alidai hii kesi iko katika hatua za mwanzoni kwa namna yoyote ile kubadili hati ya mashitaka ni kinyume cha kifungu cha sheria alizozitaja huku akiweka msisitizo kwa kurejea mashauri yaliyowahi kufanyiwa uamuzi kwenye mahakama za juu.

"Mheshimiwa hakimu, Wakili Msomi Mtobesya amezungumza kubadili mashitaka kunapokuwa na utofauti kati ya mashitaka na ushahidi unaotolewa mahakamani  ambao hapa haupo. Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza hii kesi hivyo tunaomba mahakama isikubaliane na ombi la kubadilisha hati ya mashitaka," aliomba wakili Madeleka

Akijibu hoja hizo wakili wa Serikali, Semkole aliomba kutofautiana kwa hoja za kisheria zilizotolewa na mawakili hao kwa kile alichoeleza kuwa hakuna sheria inayokataza kubadili hati ya mashitaka kesi inapokuwa haijaanza kusikilizwa hivyo akaiomba mahakama imruhusu kufanyia mabadiiliko hati hiyo kwa kuongeza shitaka moja.

Akiwasilisha hoja za nyongeza wakili wa utetezi, Mtobesya alieleza kuwa hivyo ni vitu vya kisheria hivyo wakili wa serikali anapaswa kuelewa mamlaka ya mahakama  yanatokana na sheria huku akiendelea kusisitiza kuwa wakili wa serikali  hajaiongoza vema mahakama hiyo ambayo haina nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo  ili aweze kufanya mabadiliko hayo kwenye hati ya mashitaka.



"Zoezi ambalo mahakama yako inaombwa kulifanya ni kinyume cha 'procedure' .Zoezi hili halijaombwa sawasawa mahakama hii inapaswa kuelekezwa sawasawa namna ya kufanya hayo mabadiliko kwenye hati ya mashitaka.Hivyo tunaomba mahakama ikatae ombi hilo," alisisitiza wakili Mtobesya.

Mara baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Hakimu Mkazi Mhenga aliomba muda wa dakika 20 ili aweze kupitia hoja hizo na kutokea uamuzi mdogo.

Katika uamuzi wake aliamua kukubaliana na ombi la upande wa jamhuri la kufanyia marekebisho hati hiyo ya mashitaka kwa kile alichoeleza kuwa mabadiliko hayo hayataleta tofauti katika kesi inayowakabili.


"Kuruhusu mabadiliko ya hati ya mashitaka hakuwezi kuleta 'injustice' yoyote kwa washitakiwa ila kujua mashitaka wanayokubaliana nayo mahakamani ambayo ni haki yao," alieleza Hakimu Mkazi Mhenga.

Alisema kuwa hoja kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kufanya mabadiliko hati hiyo ya mashitaka haiko kisheria kwani hakuna sheria yoyote inayokataza mabadiko ya hati ya mashitaka.

Hakimu Mkazi Mhenga alisema kuwa kufanyia mabadiliko hati hiyo ya mashitaka na kuongeza shitaka hilo haitaleta tofauti yoyote hivyo akautaka upande wa mashitaka kufanyia mabadiliko hati hiyo ya mashitaka.

 UMATI WA WATU WAFURIKA MAHAKAMANI

Umatu mkubwa wa watu ulifutika manakamani hapo kuanzia majira ya asubuhi ambapo wengi wao walionekana kuanza kusimama nje ya mahakama kabla ya baadaye kuingia ndani ya viwanja vya mahakama kisha kwenda kukaa kwenye viti vilivyopo gorofa ya pili ya kituo cha utiaji haki Arusha.

Aidha wakati kesi hiyo ilipotajwa wananchi hao ambao wengi wanaonekana ni jamii ya wafugaji wa kimaasai kutokana na mavazi ya rubega waliyovaa na lugha waliyokuwa wakiongea waliwahi kuingia kwenye chumba cha mahakama hali iliyowalazimu askari magereza kuingilia kati na kuanza kupanga watu.

Ilibidi baadhi ya watu wapungue kutoka kwenye cgumba cha mahakama ili kuwezesha mawakili wa utetezi na waandishi wa habari ambao walikuwa wamebaki nje ya chumba hicho waweze kuingia.

Mara baada ya shauri hilo kuahirishwa kwa muda wakati washitakiwa hao wakiwa mahakamani hapo baadhi walionekana wakiongea na mawakili wao ambapo askari magereza walisitisha zoezi hilo na kuwapelekeka washitakiwa hao kwenye mahabusu iliyopo mahakamani hapo mpaka hakimu aliporudi kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo ndipo wakarejeshwa.

0 Comments:

Post a Comment