![]() |
| ALIYEKUWA Mkurugenzi wa jiji laArusha, Dk John Pima akiongea na wakili wake Valentine Nyalu ndani ya mahakama kabla ya kesi kuanza |
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa jiji la la Arusha, Dk John Pima (44) na wenzake wawili wamefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakikabiliwa na kesi ya nyingine ya uhujumu uchumi yenye mashtaka sita yakiwemo mawili ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.
Mashitaka mengine ni kutumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri ,ufujaji na ubadhirifu ambayo Dk Pima na wenzake wamesomewa Juni 21, mwaka huu mbele ya hakimu Mkazi wa mahakama hiyo , Bittony Mwakisu anayesikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022.
Washitakiwa wengine ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha ya halmashauri hiyo, Mariam Mshana (40), ambaye alikuwa amembeba mtoto wake mdogo mahakamani hapo na aliyekuwa mkuu wa idara ya Uchumi na Mipango, Innocent Maduhu (40).
Hii inakuwa ni kesi ya tatu kwa Dk Pima na wenzake kwani Juni 17, mwaka huu Dk Pima na wenzake wanne walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa nane ya ufujaji wa mali ya umma na kughushi nyaraka katika kesi mbili za uhujumu uchumi ambapo kesi hiyo inawakabili washitakiwa watano wakiwemo waliokuwa wachumi katika jiji hilo, Nuru Ginana na Alex Daniel.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022, iliyosemwa Juni 21, mwaka huu washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita ambapo kosa la kwanza linalowakabili ni ufujaji na ubadhirifu wa Sh103 milioni, kosa la pili na la tatu ni kutumia nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri.
Kosa la tano linalomkabili Maduhu peke yake ni utakatishaji fedha huku la sita likiwa ni la utakatishaji fedha linawakabili washitakiwa wote watatu.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule, Wakili wa Serikali, Charles Kagilwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Richard Jacopiyo huku washtakiwa hao wakiwakilishwa na Mawakili, Valentino Nyalu na Sabato Ngogo.
Akiwasomea mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Kagilwa alieleza mahakamani hapo kuwa shitaka la kwanza linawakabili washitakiwa wote watatu ambapo ni la ufujaji na ubadhirifu kinyume cha sheria ya uhujumi uchumi na sheria za kuzuia na kupambana na rushwa.
Alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa wote katika tarehe tofauti kati ya Machi 28, mwaka huu na April 14, mwaka huu wakiwa wameajiriwa wa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI wakiwa kama mkurugenzi wa halmashauri jiji la Arusha, Mkuu wa Idara ya Fedha na mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango waliweza kutumia milioni 103 ambazo zimekuja kwao kupitia nafasi zao.
Wakili wa serikali Kagilwa alieleza kuwa shitaka la pili linawakabili washitakawa wote watatu ambapo wanadaiwa walituma nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri wao kinyume cha sheria za kuzuia na kupambana na rushwa na uhujumi uchumi.
Alidai kuwa mnamo tarehe 27 machi mwaka huu katika jiji wilaya na mkoa wa Arusha washitakuwa hao wakiwa wameajirikiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutumia nyaraka, dokezo walitoa taarifa zao uongo kuonyesha kwamba Maduhu aliomba masurufu kwa ajili ya kununua mchanga moramu shilingi milioni 103 kwa nia ya kutengeneza matofali wakati wakijua ni uongo.
Katika kosa la tatu ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa wote walitumia nyaraka kumdanganya mwajiri wao ambapo mnamo tarehe 27 machi, huu katika jiji wilaya na mkoa wa arusha kwa nafasi ya mkurugenzi wa jiji la Arusha, Mkuu wa kitengo cha fedha na Mkuu wa kitengo cha mipango na uchumi waliweza kumdanganya mwajiri.
Ilidaiwa waliandaa maombi ya masurufu ya safari zikiwa na taarifa za udanganyifu wakijifanya bwana, Innocent Maduhu ambaye ni mchumi aliomba malipo ya kiwanda cha ujenzi wa kiwanda cha matofali kiasi cha shilingi milioni 103.
Ilidaiwa katika shitaka la nne washitakiwa hao walitumia nyaraka kwa nia ya kumdanganya mwajiri wao ambapo mnamo Aprili 28, mwaka huu walijifanya kuonyesha Maduhu alirejesha fedha za ununuaji 'material' kwa ajili ya ununuaji wa vifaa vya kujenga kiwanda cha matofali wakati wakijua si kweli.
Shitaka la tano la utakatishaji fedha linalomkabili, Madihu peke yake ambapo anadaiwa mnamo Aprili , mwaka huu alijipatia gari yenye namba za usajili T 844 DYY aina ya Subaru Forester kwa fedha ambazo ni zao la uhalifu la kumdanganya mwajiri wake
Wakili Kagilwa alisoma shitaka la sita la utakatishaji fedha linalowakabili washitakiwa wote watatu wanadaiwa kuwa katika terehe tofauti kati ya Machi 23, mwaka huu na Mei 25, mwaka huu walijipatia fedha taslim sh milioni 103 wakati wakijua fedha hizo zilitokana na zao la uhalifu la kumdanganya mwajiri wao.
Washitakiwa wote wamekanusha mashitaka yote ambapo wakili wa serikali Kagilwa alieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mwakisu aliahirisha shauri hilo Julai 5, mwaka huu litakalorudi mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa ambapo washitakiwa wote walirejeshwa mahabusu kwenye gereza la mkoa la Kisongo.
Awali Juni 17, mwaka huu, Dk Pima na wenzake wanne walifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Bittony Mwakisu, wakikabiliwa na makosa nane katika kesi mbili za uhujumu uchumi.
Dk Pima na wenzake watatu Innocent Maduhu (aliyekuwa mchumi wa Jiji), Nuru Ginana (mchumi), Alex Daniel (mchumi),
Hata hivyo mshitakiwa mwingine ni Mshana ambaye alikuwa Mwekahazina wa Jiji hilo hakuwepo mahakamani hapo, hivyo upande wa Jamhuri ukaomba mahakama kutoa hati ya wito na kukamatwa kwa mshitakiwa huyo ambaye ni wa pili katika kesi zote.
Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Akisa Mhando na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Hamidu Simbano huku Dk Pima na Maduhu wakiwakilishwa na Wakili Valintine Nyalu.
Katika kesi ya kwanza, Dk Pima, Mariam, Maduhu na Ginana wanakabiliwa na mashitaka manne ambayo ni ufujaji na ubadhirifu huku makosa mengine yakiwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Aidha washitakiwa hao wataendelea kukaa mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ambapo kila mmoja anapaswa kuwa na wadhamini wawili watakaoweka kiasi cha shilingi 32 milioni au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ambapo hawakuweza kukamilisha masharti hayo.
Awali katika kesi ya kwanza ya uhujumu uchumi namba 3/2022 inawakabili Dk Pima,Mariam,Maduhu na Ginana wanakabiliwa na mashitaka manne ambayo ni ufujaji na ubadhirifu huku makosa mengine yakiwa ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu ambapo kwa pamoja wanadaiwa kati ya Aprili 14 hadi 16 mwaka huu,katika wilaya na Mkoa wa Arusha wakiwa waajiriwa wa serikali,walitenda kosa la ufujaji na ubadhirifu wa fedha Sh67 milioni.
Shitaka la pili ni matumizi ya nyaraka kwa malengo la kumdanganya mwajiri ambapo wanadaiwa kutumia nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari dokezo lenye maelezo kuwa Nuru amenunua na kusambaza moramu yenye thamani ya Sh65 milioni kwa ajili ya Soko la Samunge huku wakijua nyaraka hiyo siyo ya kweli na wakimdanganya mwajiri.
Shitaka la tatu ilidaiwa kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri,ambapo wanadaiwa Aprili 14,2022 wakiwa na nia ovu walitumia nyaraka ya maombi ya masurufu(safari) ikionyesha Nuri amenunua na kusambaza moramu ya Sh65 milioni huku wakijua wanamdanganya mwajiri wao.
Alitaja shitaka la nne kuwa ni matumizi mabaya ya nyaraka kwa malengo ya kumdangaya mwajiri ambapo wanadaiwa Aprili 28,mwaka huu wakiwa na nia ovu ua kumdanganya mwajiri walitumia nyaraka ya marejesho ya masurufu ikionyesha Nuru amefanya marejesho ya Sh65 milioni ikiwa ni malipo maalum ya kazi za nje ya kituo chake cha kazi.
Katika kesi ya pili ya uhujumu uchumi namba 4/2022 washitakiwa ni Dk Pima,Mariam,Maduhu na Daniel wanakabiliwa na makosa manne ikiwemo la ufujaji na ubadhirifu pamoja na matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri.
Akiwasomea mashtaka hayo,Wakili Akisa alidai kosa la kwanza ni ufujaji na ubadhirifu ambapo kati ya Aprili 14 hadi 16,mwaka huu wakiwa waajiriwa wa serikali kwa pamoja na kwa nia ovu walifanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kwa matumizi yao binafsi Sh65 milioni iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya matumizi ya umma.
Alitaja shitaka la pili katika kesi hiyo kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri kinyume na sheria ambapo wanadaiwa Aprili 14,mwaka huu walimdanganya mwajiri kupitia nyaraka yenye dokezo lililokuwa linahusiana na shughuli za kila siku za mwajiri ambapo walidanganya Daniel amenunua na kusambaza moramu yenye thamani ya Sh65 milioni huku wakijua kwa kufanya hivyo ni kumdanganywa mwajiri.
Alidai shitaka la tatu kuwa ni matumizi ya nyaraka kwa malengo ya kumdanganya mwajiri ambapo,Aprili 14,mwaka juu wakiwa na nia ovu walitumia nyaraka ya maombi ya masurufu,ikiwa na maelezo ya uongo yakionyesha Daniel amesambaza moramu kwa ajili ya matengenezo ya barabara hivyo adai Shilingi 65 milioni huku wakijua wanamdanganya mwajiri wao.
Shitaka la nne ni matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri ambapo wanadaiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu kupitia nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari marejesho ya masurufu iliyoandikwa Aprili 26,2022 iliyohusiana na shughuli za mwajiri.
Alidai nyaraka hiyo ilikuwa na maelezo ya udanganyifu kuwa Alex anafanya marejesho ya Shilingi 65 milioni ikiwa ni matumizi ya kusambaza moramu katika taasisi mbalimbali za serikali kwa ajili ya kutengeneza barabara huku wakijua kwa kufanya hivyo wanamdanganya mwajiri.
Aidha washitakiwa hao walikana kutenda makosa hayo ambapo Mahakama ilitoa masharti ya dhamana kuwa kila mshitakiwa awe na wadhamini wawili kila mmoja adeposit Sh32.5 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani kama hiyo.
Washitakiwa hao walitakiwa kutokusafiri nje ya mipaka ya Tanzania na kuwasilisha hati zao sa kusafiria ambapo pia walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kuwa wataendelea kukaa mahabusu hadi watakapotimiza masharti hayo.
Hakimu Mwakisu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai Mosi mwaka huu ambapo watuhumiwa hao watasomewa maelezo ya awali.
Mashauri haya yamekuja baada ya Mei 24 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwasimamisha kazi maafisa sita wa Jiji hilo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za jiji na tuhuma za kughushi nyaraka.
.jpeg)
0 Comments:
Post a Comment