Dkt. Tulia ametoa pongezi hizo leo Mei 20, 2022 wakati akifungua semina ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa wake na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa utakaofanyika Mei 22, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
“Nadhani sitakuwa nimekosea nikisema ongezeko la faida baada ya kodi ambayo Benki yetu ya CRDB imepata mwaka jana kufikia Sh bilioni 236 kulinganisha na Sh bilioni 165 mwaka 2020, ni ukuaji mkubwa wa faida kupata kutokea,” alisema Dkt. Tulia.
Amesema kuwa CRDB imeendelea kudhihirisha kivitendo kuwa “Benki kiongozi” nchini kwani kila mwaka imekuwa ikiendelea kutoa faida ya uwekezaji kwa wanahisa wake huku akizitaka taasisi nyengine za umma na binafsi kuiga mfano.
Aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina ya elimu ya fedha na uwekezaji kwa ajili ya wanahisa wake na Watanzania huku akibainisha kuwa umahiri wa masuala ya fedha wa wananchi ni moja ya msingi muhimu wa maendeleo ya watu wa taifa lolote duniani.
“Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuongoza katika utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa Watanzania. Siku chache zilizopita, mliandaa semina mliyoiita CRDB Bank Uwekezaji Day, mimi niliichungulia mtandaoni nikiwa Dodoma. Semina ile ilikuwa nzuri sana, watoa mada walitufungua macho wengi wetu,” Dkt. Tulia amesema huku akiitaka benki hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza ujumuishi wa kifedha.
Amewahamasisha wanahisa wa Benki ya CRDB kutumia haki yao ya kimsingi ya kuhudhuria Mkutano Mkuu utakaofanyika kesho tarehe 21 Mei 2022. Vilvile aliipongeza Benki hiyo kwa kuja na mfumo wa mkutano kupitia mtandao ambao unawezesha wanahisa wengi kushiriki na hivyo kuimarisha utawala bora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay amesema benki hiyo ikiwa benki ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80, inajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa katika benki hiyo.
“Niwakaribishe Watanzania wengine waje kuwekeza ndani ya Benki yetu ili nawao waanze kunufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na Benki yao,” aliongezea Dkt. Laay.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB , Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo Wanahisa wao pamoja na Watanzania wengine ili kuwajengea uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hususan katika soko la hisa la Da es Salaam.
“Kwa kutoa elimu hii Wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika Benki yao ya CRDB, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha na Watanzania wengine pia kuwekeza katika hisa hususan za Benki ya CRDB na kuanza kupata gawio,” aliongezea Nsekela.
Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha Wanahisa katika Mkutano Mkuu utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kupitia Mtandao. “Mkutano utaanza saa 3 asubuhi, watu wa mtandaoni wataweza kujiunga kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App,” alisema Nsekela.
Benki ya CRDB imeweka muongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yake ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii ya Instagram, twitter, lakini pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa Wanahisa.
Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na
Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara.
Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania na Burundi kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni 3 na kupitia mtandao mpana wa matawi 268, zaidi ya CRDB Wakala 19,000, 550 ATM, mashine za manunuzi 1,500 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.







0 Comments:
Post a Comment