Watu watano kutoka familia moja wakazi wa Kitongoji cha Magulio, kijiji na Kata ya Kamsisi Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na mvua kubwa wakiwa wamelala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, (RPC) Ali Makame Hamad amesema tukio hilo limetokea Machi 2,2022 majira ya saa 4 usiku ambapo familia hiyo wote walikuwa wamelala katika chumba kimoja.
"Watu hao watano wote wa familia moja ambao majina yao ni Masalu Sengule (32), Muri Shija (25), Nkiya Masalu (7), Vumi Masalu (5), Mariam Masalu mwenye umri wa miezi mitano wote wakazi wa Kijiji cha Kamsisi",alisema ACP Hamad.
Katika tukio lingine linalofanana na hilo watu wawili waliofahamika kwa majina ya Faines Mihani (37) na Elizabeth Nyandwi (13) ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la Sita Shule ya Msingi Mlibanzi walifariki Dunia papo hapo baada ya kupigwa na radi wakiwa shambani wanalima.
Tukio hilo limetokea mnamo Februali 28,2022 majira ya saa 9 jioni katika Kijiji Cha Mlibanzi,Kata ya Ipwaga Tarafa ya Kabungu Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.
0 Comments:
Post a Comment