RAIS, Samia Suluhu ametangaza kurudisha tozo ya Sh100 iliyokuwa ikitozwa katika mafuta ya taa, petroli, na dizeli.
Wizara ya Nishati iliondoa tozo hiyo Februari 28, mwaka huu ikisema uamuzi huo umetokana na kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na vita kati ya Urusi na Ukraine.
Rais Samia ametangaza kuirejesha tozo hiyo leo Machi 30, 2022 wakati anapokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Samia amesema suala la upandaji wa bei za mafuta yamekuwa yakipanda tangu katikati ya mwaka jana na kwamba walichukua hatua yakupunguza tozo kwa mara ya kwanza ili kushusha bei ya mafuta kwa wananchi.
Mwezi mmoja uliopita, Wizara ya nishati nchini Tanzania ilisema ilifikia uamuzi wa kuondoa tozo ya shilingi 100 kwa kila lita ya Dizeli, Petroli na mafuta ya taa ambayo ilipaswa kulipwa na watumiaji wa mafuta nchini humo kuanzia mwezi Machi mpaka Mei , mwaka huu kulingana na tathmini ya mwenendo wa soko la dunia katika mafuta.
Hatua hii ilikadiriwa kupunguza mapato ya serikali ya shilingi bilioni 30 za Tanzania kwa kila mwezi.
Taarifa ya wizara ya nishati ilisema pia kuwa uamuzi huo uliaenda sambamba na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa ya kupunguzwa kwa tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta hapa nchini zenye thamani ya Sh102 bilioni kwa mwaka, kwa lengo la kupunguza bei za mafuta na kuwapa unafuu wananchi.
Taasisi zilizoguswa na maelekezo hayo ya Rais Samia ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (tozo ya udhibiti), Mamlaka ya Bandari (tozo ya miundombinu), Mamala ya Mapato Tanzania (tozo ya kuchakata taarifa), Shirika la Viwango Tanzania (tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta).
Hata hivyo bei mpya ya mafuta iliyoanza kutumika Machi 02, 2022 zikizingatia marekebisho ya kanuni alizoweka waziri wa nishati, January Makamba , imefutwa na rais Samia ingawa hawajasema lini inaanza wala kuisha.
Amewataka wabunge, mawaziri wanaosimamia sekta hiyo kuwaambia ukweli wananchi kuwa vita ya Russia na Ukraine imepandisha bei ya mafuta.
“Mafuta yanapopanda ndio kila kitu kinapanda nauli zitapanda, usafirishaji wa bidhaa utapanda. Sasa hivi kutoa kontena la bidhaa kutoka China kuleta Tanzania, kwa kontena nadhani la futi 40 lilokuwa dola (za Marekani) 1500 sasa hivi ni dola (za Marekani) 8,000 hadi 9,000,”amesema.
Amesema na hilo inaenda kuathiri bei za bidhaa na kuwataka viongozi kuwaeleza sababu za kupanda kwa bei ya bidhaa nchini.
Amewataka wawaambie wananchi ukweli ili wasikae kusema kuwa Serikali inakaa kimya na haichukui hatua.
Kuhusu mafuta ya kula, amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kuangalia upya uamuzi waliouweka kwa ajili ya kulinda viwanda vya nchini.
Amesema uamuzi huo ulilenga kulinda viwanda vya nchini lakini imeonekana badala ya kulinda, baadhi ya viwanda vimekufa na hivyo kusababisha bei ya mafuta ya kula kuwa juu.
“Sasa mmezuia mafuta ya nje hayaingii viwanda vya ndani havizalishi. Bila shaka wananchi watapiga kelele kwa sababu bei itakuwa kubwa,”amesema.
0 Comments:
Post a Comment