ALIYOSEMA RAIS SAMIA, WAKATI AKIPOKEA TAARIF YA CAG NA RIPOTI YA TAKUKURU

 

YALIYOJIRI LEO MACHI 30, 2022 WAKATI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, SAMIA SULUHU HASSAN AKIPOKEA RIPOTI YA CAG NA TAKUKURU IKULU JIJINI DODOMA


Aliyosema Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan*


#Taarifa mlizoziwasilisha leo, ni fursa kwetu viongozi na Watendaji wa Serikali kujitathimini na kutathimini utendaji wetu na wa taasisi zetu, pia ni fursa kwetu kutathimini tija na ufanisi wa taasisi zetu katika utekelezaji wa majukumu yake.


#Nashukuru kwamba tathimini zilizofanywa na taasisi zote za nje zimeona kuna upungufu wa kiwango cha rushwa nchini na tumepanda nafasi saba kwenda juu hivyo niwapongeze Watanzania wote na taasisi za Serikali kwa kazi nzuri mnazozifanya zikaleta hali hiyo.


#Kuna michango ambayo haiwasilishwi kwenye mifuko ya jamii, naomba Mashirika yanayohusika na kutopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko hiyo yakasimamiwe vizuri. Aidha, kuna Mashirika 38 ya umma yanayoendeshwa bila kuwa na Bodi ya Wakurugenzi, kama kuna Waziri anayeendesha mashirika yasiyokuwa na bodi siwezi kumuelewa na sijui tatizo ni nini.


#Tulifanya kazi ya kuangalia utendaji wa mashirika yaliyo chini ya Mawizara na kuyatathimini,  Sasa ni wakati Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na Taasisi zinazohusika tukae kuangalia mashirika haya ili yale ya kuyafuta tuyafute.


#Kwa mwaka ujao wa fedha, tumeelekeza fedha nyingi sana kwenye kuimarisha umeme kwa kujenga vituo vitakavyoimarisha upatikanaji wa umeme, naomba mnaohusika mkazisimamie fedha  zitoke na zikafanye kazi hiyo ili umeme uwe wa kutosha.


#Kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Nyerere la kuzalisha umeme ni kweli kuna mambo kadhaa ambayo yamechelewesha utekelezaji wake lakini tunategemea litakamilika mwaka 2024 na tutahakikisha kwamba linajengwa kama lilivyosanifiwa, bora tuchelewe lakini tufike.


#Thamani ya Shirika la Ndege la Tanzania inashushwa kwa sababu ya madeni waliyoyarithi na ndege wanazoziendesha wanakodi kutoka Shirika la Ndege za Serikali hivyo lazima tukae tuone jinsi ya kuondoa madeni hayo na kuwapa baadhi ya ndege ili thamani ya shirika hilo ipande.


#Bado SADC wanaiamini Tanzania, bado wanajadili kuipa tena Bohari yetu tenda ya kusambaza dawa ndani ya eneo la SADC hivyo Bohari hii irekebishwe, isimame iwe bohari inayojitambua na iweze kufanya kazi hii.


#Ni kweli kwenye Balozi zetu kuna majumba mabovu lakini nilitoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kuzungumza na benki zetu na sekta binafsi ili wale ambao wanaweza wakajenge katika viwanja vya Balozi zetu halafu zitumike kibiashara ili Ubalozi upate na Shirika lipate.


#Kutokana na malalamiko yanayosemwa kutoka nje, kuna baadhi ya meli zinaondoka bila kushusha mizigo ambapo kwa upande wa TPA, meli zinakaa siku mbili hadi tatu kushusha mizigo lakini kwa upande wa TICTS meli zinakaa hadi siku 28 kwa hiyo wahusika mkaangalie kuna tatizo gani, ingawa ni kampuni binafsi lakini wanatakiwa kuendana na masharti na taratibu zilizowekwa na Bandari.


#Nimeanza kupata malalamiko kuwa wauza dawa za kulevya wote wanatolewa hivyo nyie mliowaweka ndani angalieni vizuri, kama mna ushahidi wa kutosha endeleeni na kesi zao na kama hamna ushahidi angalieni nini mnaweza kufanya.


#Tunapofika mahali hatukuelewana na Mwekezaji na tunataka kukatisha mkataba basi Sheria zifuatwe ili tukate mikataba kuendana na  taratibu zinavyosema ili kuiepusha Serikali kulipa gharama tunazodaiwa kwani tumelipa fedha nyingi sana kwa kukatisha mikataba bila kufuata taratibu.


#Serikali za Mitaa bado kuna upotevu mkubwa wa mapato, Waziri husika endelea kuzisimamia halmashauri katika suala hilo na usione shida wala kuwaonea huruma kuwafukuza wanaofanya vitendo vya wizi, anayeharibu fedha za Serikali muweke pembeni.


#Kuhusu mapendekezo ambayo yaliyotolewa kwenye ripoti ya mwaka uliopita na bado hayajafanyiwa kazi, Ninaagiza Mawaziri na Makatibu Wakuu wote kuangalia hoja mlizojibu na ambazo bado hamjazijibu zijibiwe na ziende Bungeni au kwa zile ambazo hazijibiki basi mchukue hatua kwa wale waliofanya makosa hayo.


#Nawaagiza Makatibu Wakuu ambao ndio Maafisa masuhuli kuwa wasiwe viongozi wa kutoa njia za kuchota fedha za Serikali bali wawe wasimamizi wa fedha hizo, muhoji kwa nini fedha zimetumika vibaya, msiwatetee wanaotumia vibaya fedha za Serikali.


#Kila Wizara na Shirika inatakiwa kuwa na vitengo madhubuti vyenye watu wenye weledi kwa ajili ya kufanya tathmini na ufuatiliaji, hivyo Katibu Mkuu Kiongozi kupitia Chuo cha Uongozi mfanye mafunzo ya haraka ili watu wanaosimamia vitengo hivi ambao hawako vizuri wapewe zana zote ili waweze kufanya kazi hizo.


#Kuna malalamiko ya kupanda kwa bei za bidhaa, kwa sababu ya UVIKO 19 hakukuwa na uzalishaji viwandani, uzalishaji ndio unaanza hivi sasa hivyo, kutokana na uchache wa bidhaa bila shaka bei zinapanda kwa bidhaa nyingi tunazoziagiza nje.


*Aliyosema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), CP Salum Hamduni*


#Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wako mahiri, kwa utashi ulionao kwa kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini, TAKUKURU inakuahidi kuendelea kuongeza juhudi katika kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye rasilimali za umma hususan utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


#Kwa mwaka 2020/21 kupitia oparesheni mbalimbali zilizofanywa na TAKUKURU, tumefanikiwa kuokoa jumla ya shilingi bilioni 29..3 pia, TAKUKURU iliweza kufanya uchunguzi na kukamilisha majalada 1, 053 ya makosa ya Rushwa yakiwemo majalada  9 ya rushwa kubwa ambazo zina thamani kuanzia shilingi bilioni moja na kuendelea.


#Na kwa wale watakaobainika na kuthibitishwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, nakuahidi Mhe. Rais Samia kuwa hawatabaki salama, tutawashughulikia vilivyo.


*Aliyosema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.*


#Kwa mwaka 2020/21, Ofisi ya CAG imefanikiwa kufanya kaguzi 7 katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Mikoa na Rufaa, daraja la Kigongo-Busisi na Wami, ujenzi wa mradi wa umwagiliaji maji, usanifu na usimamizi wa baadhi ya miradi ya maji, uboreshaji wa viwanja vya ndege, usanifu na usimamizi wa miradi ya barabara jijini Dodoma. 


#Kwa mwaka 2020/21, Ofisi ya CAG imefanya jumla ya kaguzi maalum 56 ambapo kaguzi 37 ni za Mamlaka ya Serikali za Mitaa, 12 Serikali Kuu, 6 Mashirika ya Umma na moja ya mifumo ya TEHAMA.


#Katika kuunga mkono jitihada za Serikali pamoja na maelekezo yako kuhakikisha kwamba fedha zote kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kinatumika kama kilivyopangwa, tunaendelea na ukaguzi katika maeneo yote yaliyopatiwa fedha za miradi za UVIKO 19 Tanzania na naahidi kwamba kila fedha iliyotumika itakaguliwa kuhakikisha imetumika kwa kufuata Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo husika.


Leo Ofisi ya CAG inawasilisha jumla ya ripoti 20 zinazojumuisha masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika ukaguzi uliofanyika kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2021. Baadhi ya ripoti hizo ni kutoka Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma, Miradi ya Maendeleo, Ukaguzi wa ufanisi, Ukaguzi wa Mifumo ya TEHAMA na ripoti 12 za Ukaguzi wa Ufanisi zinazohusu sekta mbalimbali.



0 Comments:

Post a Comment