SAKATA la Mawaziri wa wanaohusika na masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kushindwa kuhudhuria kwenye bunge la jumuiya hiyo, (EALA) limechukua sura mpya baada ya kuelezwa endapo hawatatokea tena leo itakuwa ni hujuma kwa bunge.
Aidha ofisi ya spika haikuwa na taarifa yoyote juu ya sababu iliyopelekea mawaziri wote kutohudhuria bungeni hata kwa njia ya mtandao kama baadhi yao walivyozoea.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa EALA kutoka Kenya, Aden Omar Abdikadir ambaye aliongoza kikao hicho cha alhamisi baada ya spika wa bunge hilo, Martin Ngoga kutokuwa kwa taarifa.
Aden amesema kuwa endapo leo hatatokea waziri hata mmoja italazimu bunge hilo kuahirishwa tena kwa sababu wao ndiyo wana miswada ya kuwasilisha bungeni jambo alilosema kuwa hiyo watakuwa wanahujumu kazi za bunge.
"Kazi zetu hapa zinakuwa ni ngumu kutekeleza lazima wawepo mawaziri wazichukue. Wao ndiyo wazizungumzie hoja hizo. Wamewekwa pale kwenye bunge ili waweze kuzisikiliza," amesema Aden na kuongeza.
...Hatuwezi kupeleka muswada kwa hatua inayofuata mpaka waziri mmoja asimame aseme anaomba muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza, mara ya pili kama waziri hayupo hakuna mtu anaweza kufanya hiyo kazi.
..Sasa watakuwa kama hawaji hapa basi wanahujumu kazi ya bunge,"..
Alipotakiwa kueleza endapo ofisi ya spika ina taarifa zozote juu ya ni kwa nini mawaziri hao toka nchi sita zinazounda EAC hawajafika bungeni alisema mpaka anaahirisha na anaondoka eneo la bunge hakuna taarifa yoyote kutoka kwa waziri yeyote.
Mwenyekiti wa baraza la Mawaziri kwa sasa anatokea Kenya nafasi hiyo inashikwa kwa kipokezana ambapo nchi inayoshika nafasi ya mwenyekiti wa marais na waziri anayehusiana na masuala ya EAC anakuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri.
Kwa upande wake mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Habibu Mnyaa amesema kitendo walichofanya mawaziri hao ni cha aibu na hakijapata kutokea kwenye historia ya bunge hili.
"Kulikuwa na miswada na matatu ambayo yote ni ya baraza la mawaziri ambao wanaopaswa kuwasilisha hoja na kila nchi ina mawaziri wawili wanaowakilisha nchi zao kwenye EAC na majukumu yao yameanishwa kwenye mkataba wa kuanzisha jumuiya," amesema Mnyaa na kuongeza.
....Bunge haliwezi kuendelea bila mawaziri kuwepo kwa sababu yale yanayojadiliwa na wabunge wanapaswa wayachukue ili yakafanyiwe kazi na serikali sasa mawaziri wasipokuwepo wabunge hawawezi kuzungumza wenyewe,".
Mnyaa amedai kuwa kuna wakati hali hiyo ilijitokeza ya Mawaziri kutohudhuria vikao vya bunge na Spika Martin Ngoga akalazimika kuahirisha bunge huku akiwataka mawaziri kuhudhuria vikao ili shughuli za bunge ziweze kuendelea.
“Sisi tumetoka nyumbani tumekuja hapa (Bungrni Arusha) tunalipwa kila siku kwa ajili ya kushiriki shughuli za bunge sasa kama hazifanyiki kwa sababu ya mawaziri hawaji basi ni tatizo," amesema Mnyaa na kuongeza.
....Mawaziri wanatengeneza miswada yao wenyewe na hawapo, wao wenyewe ni tatizo inakuwa kama wamesusa hatuwaelewi kwa kweli. Kungekuwa hakuna hizo hoja za Mawaziri basi tusingeshangaa sana. Sasa kuna miswada yao kwa nini waondoke wote, je hawana uratibu miongoni mwao.
...Kuna wakati mawaziri wanahudhuria kwa njia ya mtandao kimewashinda nini leo hata mmoja miongoni mwao kufanya hivyo?,".
Kwa upande wake, Mbunge wa Eala kutoka Tanzania, Mariam Ussi Yahaya,alisema kuwa kikao cha bunge walikuwa wajadili ripoti nne zikiwemo mbili zilizokuwa ziwasilishwe na mawaziri wenyewe na moja ni ripoti ya kamati ya mahesabu ,ambazo zote zimekwama kwa sababu ya mawaziri kutohudhulia vikao.
Alisema kuwa moja ya ripoti zilizokuwa zijadiliwe ni pamoja na suala la sheria za Jumuia ya Afrika Mashariki ambazo zinapaswa zianze pia kutumika kwenye Nchi wanachama.
"Hoja nyingine zilizokuwa zijadiliwe ni mswada wa usafiri wa anga kwa kutumia ndege (cassoa)ambao imeonekana kuwa ni usafiri ghali zaidi kwa nchi za jumuiya na hivyo kuwaumiza wananchi wetu ambao wamekuwa wakisafiri kufanyabiashara na wanafunzi kwenda kusoma kwenye Nchi wanachama," alisema Ussi.
Alisema ripoti inaonyesha kuwa usafiri ndani ya Nchi wanachama wa EAC ni ghali Sana suala ambalo lilipaswa lijadiliwe mbele ya mawaziri ili waamue namna ya kupunguza gharama za usafiri wa anga .
"Wabunge tunapaswa tufanye kila nchi ili wananchi wetu wanufaike na jumuiya yao ya Afrika Mashariki kwa gharama nafuu za usafiri ndio maana tulijipanga kuwaomba mawaziri waone namna ya kupunguza gharama za anga Kwa Nchi za EAC,"amesema Ussy
Kwa upande wake mbunge wa EALA kutoka Tanzania Abdullah Hasnuu Makame alisema kuwa wanaelewa kuws kwa upande wa Kenya Waziri na Naibu wake wamejiuzulu ili waweze kugombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu kwa mujibu wa katiba yao waziri hapaswi kuwa mbunge.
Hata hivyo licha ya kuwa hakuridhishwa na yaliyotokea lakini akaenda mbali kwa kuelekeza lawama zake kwa nchi ya Sudan ya Kusini aliyodai kuwa mawaziri wake wanaohusiana na masuala ya EAC hawajawahi hata kufika kula kiapo kwa ajili ya kushiriki shughuli za chombo hicho.
"Tokea tumewapokea ndugu zetu wa Sudani Kusini kwa mara ya kwanza mwaka 2017 hili bunge halijawahi kupokea waziri wao. Hilo jambo la kisikitisha miongoni mwa mambo ambayo wabunge walikuwa kujadili ni taarifa ya Mawaziri juu ya hatua zipi Jumuiya izichukue ili kuwaleta Sudan ya Kusini kwenye kiwango cha mtangamanl sawa na nchi nyingine zilizotangulia kijiunga na EAC," alisema Abdullah na kuongeza.
...Tukumbuke hili jambo la kusema bila kumung'unya maneno miongoni mwa nchi zinazochangia EAC kwa kusuasua ni Sudan ya Kusini ni jambo linalotutia simanzi kuangalia wenzetu hawachangii na mawaziri wao kwenye vikao hawaji sasa tunajiuliza kuna nini ni mambo ambayo wengine hawayasemi kwa sauti ila yanaongelewa chinichini.
0 Comments:
Post a Comment