Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, (Takukuru) inafuatilia jumla ya kiasi cha shilingi 12.6 bilioni zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani Arusha.
Pia taasisi hiyo imekamilisha uchunguzi wa majalada 11 yanayohusu rushwa kati ya taarifa 128 zilizofikishwa mbele ya taasisi hiyo ambapo imefungua mashauri mapya manne mahakamani.
Hayo yameelezwa leo na kamanda wa Takukuru mkoani Arusha,James Ruge wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha kuanziz mwezi Oktoba hadi Desemba 2021.
Alitaja fedha hizo zilitolewa kutekeleza miradi ya utoaji chanjo ya Uviko -19 ,ujenzi wa miundombinu ambayo ni madarasa na mabweni,sekta ya afya na ujenzi wa barabara.
Ruge alisema kati ya fedha hizo zipo zaidi ya sh,10 bilioni zilijenga vyumba vya madarasa 516 katika wilaya mbalimbali mkoani Arusha ambapo wanazifuatilia kujua kama fedha hizo zilitumika au zilipigwa na wajanja.
Hatahivyo,alisisitiza kwamba katika hatua ya awali ya ufuatiliaji wa miradi hiyo ofisi yake ilibaini mapungufu mbalimbali kama udanganyifu katika makato ya kodi ya zuio,watoa huduma kutotoa stakabadhi za malipo sanjari na kutokufuatwa kwa ramani za ujenzi hasa madarasa.
“Takukuru mkoa wa Arusha kupitia ofisi zote za wilaya ilifuatilia miradi hii kuanzia hatua ya awali ya utekelezaji wake ambapo baadhi ya miradi hiyo ilibainika kuwa na mapungufu,” amesema Ruge.
Alisema kuwa ofisi yake ilifungua mashauri mapya manne mahakamani katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021 , mashauri 27 yanaendelea mahakamani huku jamhuri ikishinda mashauri 9 ambapo watuhumiwa walikutwa na hatia.
0 Comments:
Post a Comment