CPB WAUZA UNGA WA NGANO DRC


 
 

BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania, (CPB) imefanikiwa kupanua wigo wa masoko la bidhaa zake  ambapo  imeuza tani 120 ya unga wa ngano chapa Nguvu  kwenye  nchi ya jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

 

 

Shehena hiyo ya ngano iliondoka nchini leo (Januari 7,2022) kwa njia ya barabara kuelekea kwenye Mji wa Lubumbashi ulioko kwenye mkoa wa Katanga Juu.

 


Meneja wa CPB,  kanda ya Kaskazini, Hiza Kiluwasha akiongea na waandishi wa habari jijini Arusha wakati magari yaliyobeba ngano hiyo yakiondoka kwenye kinu chao cha kusagia nafaka  alisema kuwa wamepata oda nyingine kutoa nchini Sudan Kusini na Kenya.

 

Alisema kuwa unga wa ngano chapa NGUVU umetokana na ngano iliyolimwa kwa mkataba kati ya CPB na  wakulima wa wilaya Siha, Karatu, Monduli na Hanang’ ambapo waliwakopesha mbegu aina ya SC Select kisha wakawaunganisha na taasisi ya fedha  waliowakopesha fedha kwa ajili ya patiwa mikopo .

 

Soko hilo la unga wa ngano chapa nguvu limekuja siku chache baada ya  uamuzi wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC) kuikubalia Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo kujiunga na jumuiya.

 

 

 

“Tuko hapa tunapakia unga wa ngano tani 120 zinaenda Lubumbashi nchini DRC, lengo kuu hasa kwamba tumefungua masoko ya nje ya nchi. Taasisi yetu iko chini ya Wizara ya Kilimo ambayo imetupa jukumu la kufufua zao la ngano juhudi ambazo tumezianza msimu uliopita wa kilimo mwaka 2021,” anaeleza Kiluwasha na kuongeza.

 

…Tulianza kwa kuingia mikataba na wakulima wanaolima ngano kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa kuwapatia mbegu bora tuliyoiagiza nje ya nchi na kuwaunganisha na taasisi za fedha ili waweze kununua mbolea na kupiga dawa kwa wakati ili wapate mavuno mengi na mwisho sisi tukainunua ngano yao yote.

 

…Baada ya kuinunua ngano hiyo ililetwa hapa kiwandani tukaisindika na tulipewa maagizo na serikali kuwa unga wa ngano tutakaozalisha uuzwe hapa nchini na tutafute masoko nje ya nchi sasa yamefunguka  mbali ya hii tunayoipoeleka Lubumbashi kuna nyingine itapelekwa Sudan ya Kusini, Kenya, Rwanda na Burundi.

 

….Yote hii ni katika kuhakikisha mkulima wa ngano anapolima anakuwa na uhakika wa soko la bidhaa hiyo na tayari tumeshaenda kwa wakulima kuingia makubaliano ya kuendesha kilimo cha ngano cha mkataba kwa msimu wa kilimo wa mwaka huu 2022 ambayo unawahakikishia wakulima  soko la ngano yao kwani tutainunua yote.

 

….Mkataba huu unalenga kuhakikisha mkulima wa ngano anapata mavuno bora yenye tija kwa kuhakikisha anapata mkopo, mazao yake yanakuwa na kinga ya majanga kwa kuyakatia  bima, kuendesha kilimo kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo na wakati wa kuvuna anakuwa na vifaa vya kuvunia hivyo ngano hiyo inakidhi vigezo vya ubora wa ndani na wa kimataifa,”.

 

Hata hivyo, Kiluwasha  alisema kuwa mbali ya zao la ngano pia CPB inashughulika na  mazao mengine kama mahindi, maharage, mchele, kila kitu kinachohusu nafaka CPB wananunua kuhakikisha wakulima wanakuwa na uhakika wa soko la mazao yao huku akiwasisitiza wakulima kuhakikisha wanazingatia kanuni bora za kilimo.

 

“Sisi  tunawahakikishia wakulima tutanunua mazao yao na tutawalipa hapohapo, hivyo wakulima walio Kanda ya Kaskazini kama una mahindi, ngano, maharage, mchele wayalete sisi tutanunua kwa bei ya soko na tutawalipa kwa wakati, “ alisema Kiluwasha na kuongeza.

 

…Sisi hapa tunaeneo kubwa la kuhifadhi mazao hivyo tukinunua mazao kama mahindi, tunayasindika na eneo la kuhifadhi ni kubwa kwa kabisa kuhakikisha mazao ghafi yote tunayoyanunua kutoka kwa wakulima tunayaongezea ubora na kuyauza kama bidhaa.

 

…Kwenye mkataba huo tuliweka bei ya kununua ngano hiyo kutoka wakulima iwe shilingi 800 kwa kilo ambayo ni bei ya juu ukilinganisha na bei shilingi 500 waliyokuwa wakipewa na wanunuzi binafsi ambayo lengo letu ilikuwa ni kuinua uchumi wa wa mkulima wa ngano na limefanikiwa iliyokuwa ikitolewa,".

 


 

Dereva anayepeleka shehena hiyo ya ngano nchi ya Jamhuri ya kidemorasia ya Kongo, Ernest Mollel alisema kuwa wanatazamia kutumia siku 10 kuwa wamefikisha mzigo huo Lubumbashi.

 

“Napitia njia ya Arusha Dodoma Iringa Mbeya Tunduma nitachukua takribani wiki moja na nusu nitakuwa nimefika Lubumbashi,” alisema Mollel.

 


Afisa kilimo kutoka CPB, Marco Ndonde anasema katika msimu uliopita wa mwaka 2021  bodi hiyo iliingia mkataba na wakulima wenye  jumla ya ekari 2,937 kwenye wilaya za Siha mkoani Kilimanjaro,  wilayani Hanang' mkoani Manyara na Karatu na Monduli.

 

Alisema kuwa walipata jumla ya tani 1,136 ya ngano ikiwa na ubora mzuri kwani CPB walihakikisha wanakuwa karibu na wakulima katika hatua zote kuanzia shambani kuanzia hatua ya mwanzo ya kuandaa shamba, uchambuzi wa mbegu bora, upandaji, utunzaji, uvunaji na namna ya kuihifadhi kabla ya kuifikisha sokoni.

 


Afisa Ubora wa CPB, Kanda ya Kaskazini, Kombo Abdalah alisema kuwa unga wa ngano chapa nguvu una ubora uliothibitishwa na Shirika la Viwango nchini, (TBS)  pamoja na  wa

 

Alisema kuwa ngano kabla haijapokelewa kiwandani hapo kitu cha kwanza wanaangalia hali ya ukaukaji, protin, uzito ainisho na gluten na baada ya unga kupatikana hurejea kuangalia vitu hivyo ili kuhakikisha walaji wanapata kitu kilicho bora.

 

“Tukishaipokea ngano hapa Kiwandani tunaiweka kwenye kihenga, hapo tunaendelea na shughuli za kuiandaa ngano kwa ajili ya kuisaga kwa kuangalia kiwango cha unyevu ili iweze kukoboleka vizuri na tupate unga mzuri,” anasema Kombo na kuongeza.

 

…Ukisaga ngano ikiwa kavu zaidi unapata unga mchache na kitaalam manake hiyo ni hasara na ukiweka maji mengi unga utatoka na unyevu hivyo unga utawahi kuharibika na utatengeneza ukungu hivyo unga utakuwa haufai kwa matumizi ya binadamu,”.

 


Afisa Usagishaji wa Kiwanda cha CPB, Kimweri Gasper alisema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani 120 za ngano kwa saa 24.

 

“Mashine zetu ni za kisasa, kuna mashine za kubaini na kuondoa uchafu, mawe, vyuma na tukisaidiana na watu wetu wa ubora ngano yetu hupimwa kuhakikisha kuwa haina sumu kuvu ili iwe salama kwa mtumiaji wa mwisho,” anasisitiza Kimweri.

 


Afisa Masoko na Mauzo wa CPB, Kapistorano Tweve alisema kuwa kuwa tokea wameingiza unga huo sokoni umepokelewa vizuri na wananchi wa mikoa mbalimbali jambo alilodai kuwa linampa uhakika na kwenye nchi za jirani nako utapolewa vizuri.


Afisa manunuzi na ugavi wa CPB Kanda ya Kaskazini, David Jackson amesema kuwa msimu wa mwaka 2021 walinunua ngano ghafi tani 1,136

sawa na kilo 1, 136,000 ambayo ni sawa na gunia 11,360 zenye ujazo wa kilo 100 kwa kila moja.


 





 

0 Comments:

Post a Comment