ARDHICARE Yawezesha Mamia ya Wananchi kupata Hati Mbeya

 



KAMPUNI ya mipango miji ya ARDHICARE Consult Limited imewezesha mamia ya wananchi wa Jiji la Mbeya kuanza kumilikishwa maeneo yao kisheria kwa kupatiwa hatimiliki na Ofisi ya Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mbeya.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilika kwa  Zoezi la Urasimishaji Ardhi lililotekelezwa na kampuni hiyo kwenye mitaa yao, chini ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Kati ya mwezi Novemba, 2021 hadi mwanzoni mwa Januari mwaka huu, zaidi ya wananchi 346 wa kata za Uyole na Iganjo tayari walikuwa wameshatimiza sifa na baadhi yao kupatiwa hatimiliki na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Ofisi ya Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mbeya. 


Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mwenza wa ARDHICARE, Edward Kinabo, wakati akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya wananchi waliofika Uyole katika Ofisi za kampuni hiyo tawi la Mbeya, kupata tafsiri ya maana ya maelezo yaliyomo  kwenye hati zao.


Kinabo alisema wananchi hao 346, wa mitaa ya Iwambala, Ishinga, Mwanyanje na Hasanga, ni sehemu tu ya wananchi takribani 10,000 wa kata za Uyole na Iganjo ambao wanaendelea kulipia ankara za hati ili wapate hati zao mapema mwaka huu.

"Tunaishukuru wizara ya ardhi na halmashauri ya jiji Mbeya kwa kutuamini na kutupa ushirikiano mzuri unaotuwezesha kuifanya vema kazi yetu", alisema Kinabo.

"Na zaidi,  tunawapongeza wananchi wengi kwa kuelimika, kuhamasika na kujitokeza kwa wingi katika zoezi hili.Adhima yetu ni kuhakikisha kila mmiliki anapata hati yake haraka iwezekanavyo", aliongeza kiongozi huyo.

Alieleza kuwa mbali na wananchi waliohudumiwa moja kwa moja na zoezi hilo, kampuni hiyo pia ilitoa elimu ya ziada, ikafanya uhamasishaji na kutoa msaada elekezi uliowezesha baadhi ya wananchi waliopimiwa zamani kupata hati.

"Kwa mpango huu, serikali imetukomboa. Zamani ungempata wapi wa kupima eneo kwa bei nafuu hivi? Na mimi niwashukuru sana Jiji kwa kutuletea hawa jamaa (ARDHICARE). Wanafanya kazi yao kwa utaalam na uadilifu mkubwa. Hawajatuacha njiani... wamehakikisha mpaka tunapata hati kama hivi", alisema Peter Mwankusye, mkazi wa mtaa wa Iwambala akiwa na hati yake mkononi. 

Awali akitoa ufafanuzi namna kazi hiyo ilivyofanyika, Kinabo alisema zoezi hilo linatekelezwa chini ya Mpango wa Taifa wa Kurasimisha Ardhi na Kudhibiti Ujenzi Holela, kwenye maeneo yote ya mijini yaliyoendelezwa bila kupangwa, kupimwa wala kumilikishwa. 

Alisema zoezi hilo linahusisha shughuli za kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi, kufanya utambuzi wa kila miliki ya ardhi na kisha kuandaa michoro ya mipango miji inayobeba maeneo yote kwa mujibu wa sheria ya mipango miji Na 8 ya mwaka 2007, kifungu cha 355 na kanuni zake za mwaka 2018. 

Hatua nyingine ni kupima na kusimika mawe ya alama za mipaka (beacons) katika kila miliki ya ardhi na kuandaa ramani za upimaji kwa mujibu wa sheria ya upimaji ardhi kifungu cha 324 na kanuni zake. 

Aidha, baada ya michoro ya mipango miji na ramani za upimaji kusajiliwa na wizara ya ardhi, ndipo mchakato wa umilikishaji huanza kwa wananchi kupatiwa ankara za kulipia hati zao ambazo gharama yake hutofautiana kati ya mmiliki mmoja na mwingine kulingana na ukubwa na aina ya matumizi ya ardhi husika.

Akigusia umuhimu wa zoezi hilo alisema zipo faida nyingi ikiwemo kufanikisha upatikanaji wa barabara kwa njia ya maridhiano, thamani ya ardhi na jengo kuongezeka pamoja na miliki ya ardhi kuwa salama zaidi dhidi ya uvamizi, utapeli na kuepusha migogoro ya mipaka baina ya majirani iliyokithiri kwenye maeneo mengi yaliyoendelezwa kiholela.

Nyingine ni kumpa mwananchi fursa ya kukopesheka kwa dhamana ya hati yake na kutanua wigo wa mapato ya serikali yatokanayo na kodi ya ardhi iliyopimwa na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi kwa ujumla.

0 Comments:

Post a Comment