SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Nchini, (TANAPA) limeanza utekeleza mikakati ya kukabiliana na athari za ukame kwa kujaza maji kwenye mabwawa na kunasua wanyama walionasa kwenye tope kwenye hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Aidha wameweka mikakati ya ujenzi wa mabwawa ya kisasa, kuondoa tope katika mabwawa sanjari na kuchimba visima virefu vitakavyotumia umeme wa jua.
Hayo yamesemwa Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi-Mawasiliano wa TANAPA, Pascal Shelutete kwenye taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari Desemba Mosi,2021 wakati akizungumzia tukio la wanyama kunasa kwenye bwawa ndani ya hifadhi ya Mikumi.
Alisema kuwa TANAPA inathibitisha kuwa video fupi iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao kuanzia alfajiri ikionyesha baadhi ya wanyama kunasa katika tope kuwa imetokea kwenye hifadhi ya Taifa ya mikumi.
Shelutete alisema kuwa hali hiyo inasababishwa na changamoto ya ukame iliyoathiri maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya hifadhi za Taifa kutokana na kuchelewa kwa mvua na hivyo kusababisha upungufu wa maji katika maendeo mbalimbali ya hifadhi.
“Shirika limechukua hatua stahiki kukabiliana na hali hiyo ikiwemo mkakati wa dhahrura wa kujaza maji katika mabwawa hayo na kuwanasua wanyama waliozama,” alisema Shelutete na kuongeza.
….Hata hivyo mvua zilizonyesha jioni ya Novemba 30, mwaka huu zimewezesha maji kiasi kujaa katika mabwawa husika na wanyama kurejea katika halui ya kawaida ya matumizi ya mabwawa,”.
Hata hivyo hapa nchini sekta mbalimbali zimeshaonyesha kuathiriwa na ukame huku kukitolewa miito mbalimbali kulinusuru Taifa na janga hilo.
Waziri wa nishati, January Makamba, ambaye wizara yake inanyoshewa kidole kutokana na mwendo wa kusuasua wa upatikanaji wa nishati ya umeme, amenukulwa na vyombo mbalimbali vya habri (si Raia Mwema) akisema kuna haja ya kuwa na tathmini ya kina kuhusu tatizo hilo.
Tanzania inakabiliwa na upungufu wa MW 345 za nishati ya umeme kutokana kushuka kwa kina cha maji katika vyanzo vyake kulikosababishwa na ukame huo.
Kwenye maeneo mbalimbali nchini imeshuhudiwa matangazo ya mgawo wa maji safi na salama yanayosambazwa na mamlaka mbalimbali za maji .
Hata hivyo hivi karibuni mkurugenzi wa mamlaka ya hali ya hewa, Dkt. Agnes Kijazi alionya kuhusu mabadiliko hayo ya hali ya hewa.
Viongozi wa dini wameanza kuchukua jukumu la kujishughulisha na Imani kwa ajili ya kumuomba mola ili kuliepusha taifa na janga hilo la ukame. Mufti mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zuber bin Ally anawataka waimini kwa Imani zao kuweka dua ili nchi ivuke salama katika kipindi hiki.
Kumekuwa na mitazamo mingi inayojadiliwa kuhusiana na hali hiyo ya ukame, huku wengine wakilaumu mamlaka kwa kutoweka vipaumbele mahsusi vya kulinda mazingira na vyanzo vya maji, ingawa wengine wanasema hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya tabia nchi yatokanayo ya shughuli za kibinadamu.
0 Comments:
Post a Comment