SERIKALI imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) , zinazolenga kuondoa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika fani ya ununuzi na ugavi kwani pesa nyingi za serikali zinatumika kupitia taaluma hiyo.
Aidha imeitaka kumchukulia hatua madhubuti mtaalamu yeyote atakayethibitika anakiuka kanuni za maadili au kutoa ushauri wa ununuzi kinyume na sheria ya ununuzi wa umma kwani ni uzembe na ukosefu wa weledi katika kusimamia mnyororo wa ununuzi na ugavi unapelekea kukwamisha utekelezaji wa miradi na miradi mingi kufanyika chini ya kiwango.
Hayo yalisemwa leo Desemba mosi, 2021 jijini Arusha na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela wakati akifungua kongamano la 12 la wataalamu hao.
Alisema kuwa bado kuna wataalamu wachache wanafanya kazi chini ya kiwango cha taaluma yao hivyo akaiagiza bodi ya PSPTB kuendelea kusimamia taaluma hiyo kwa kuchukua hatua madhubuti kuinua weledi wa wataalamu hao pamoja na wengine wote wanaoshiriki katika mchakato wa ununuzi na ugavi kwa kuwajengea uwezo katika taratibu za manunuzi na usimamizi wa mikataba .
" Mada mliyoiweka katika kongamano hili, inayosema ubunifu wenye suluhisho katika utekelezaji wa mnyororo wa ununuzi na ugavi kwa kutambua ushindani na mapinduzi ya viwanda kwa maendeleo ya jamii itaipa changamoto bodi ya PSPTB na wataalam kuweza kutambua umuhimu wao katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na serikali ili kuweza kuongeza tija na faida katika sekta binafsi," alisema waziri Nchemba.
Alisema kuwa kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa maadili kwenye kada hii iwe chachu ya bodi kuongeza usimamizi wa maadili na kuchukuwa hatua stahiki kwa wahusika kwani taaluma hii ni muhimu sana ili kufikia adhima ya serikali ya awamu ya sita ya kuendelea kuwaletea watanzania maendeleo kwa kasi .
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, alitoa wito kwa waajiri wote kutoa ushirikiano kwa bodi hasa linapokuja swala la usimamizi wa taaluma ya ununuzi na ugavi pamoja kuzingatia matakwa yote na sheria za bodi ili kuleta tija ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.
Alisema kuwa katika taasisi nunuzi 85 zilizofanyiwa ukaguzi kwenye viashiria vya rushwa miradi mitatu yenye kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 616.5 ilibainika kuwa na viashiria vikubwa vya rushwa ukilinganisha na taarifa ya mwaka 2018/2019 ambayo iliobainika kuwa ukaguzi wa miradi 131 ulionyesha kuwa na miradi 39 ilikuwa na viashiria vya rushwa .
Waziri Nchemba alisema kuwa kwa mujibu wa ukaguzi uliofanywa na mamlaka ya uthibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2020/2021 umethibitisha kuwa ukaguzi wa mikataba 282 yenye dhamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5000.7 na mikataba 281 sawa na asilimia 99.6 imesimamiwa vizuri na kuleta dhamani ya fedha huku mkataba mmoja ulionyesha kuwa na usimamizi wa kiwango cha chini sana.
Awali Mkurugenzi mtendaji wa PSPTB , Godfred Mbayi aliishukuru serikali kwa kumteua, Jacob Kibona kuwa mkurugenzi wa bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo kwani kwa miaka mitatu nafasi hiyo ilikuwa wazi hali iliyokwamisha baadhi ya mambo katika utendaji wa taasisi hiyo.
Alisema kuwa kwa mwaka 2021 wamesajili jumla ya wataalam 1,166 ambapo wamefanya mitihani katika hatua tatu tofauti bila kutangaza kutokana na kutokuwa na bodi ya wakurugenzi na idadi hiyo imefanya idadi ya wataalamu kuongezeka na kufikia zaidi ya wataalam elfu 12.
"Hata hivyo ndugu mgeni rasmi, tunazo 'session' tatu zilizofanya mitihani bila kutangazwa kutokana na kutokuwa na mkurugenzi wa bodi ya wakurugenzi ya wakurugenzi kitendo hicho kimewaathiri vijana wengi na maafisa walio kazini, hasa katika promosheni na ajira kwa vijana," alisema Mbayi
Akimkaribisha Waziri Nchemba kuzungumza na wataalam hao, mwenyekiti wa bodi, Kibona alisema kuwa atafanya kazi kwa weledi uliotukuka kwa kipindi chote cha nafasi yake na kumaliza matatizo yote ambapo bodi itahakikisha inachukuwa hatua kali za kinidhamu kwa wataalumu wote watakao sababisha watu kupoteza imani na taasisi hiyo ya ununuzi na ugavi
0 Comments:
Post a Comment