WABUNGE EALA WACHARUKA MELI KUTOKARABATIWA KWA MIAKA 10


WABUNGE wa bunge la Afrika Mashariki,(EALA) wacharuka baada ya kupokea taarifa kuwa meli ya utafiti ya jumuiya hiyo, RMV Jumuiya  imeshindwa kufanya kazi kwa miaka 10 kutokana na kutotengwa  fedha za ukarabati huku vibali vya kimataifa vya kutumia meli hiyo vikiwa havijalipiwa.


Aidha, wakati meli hiyo haifanyi kazi manahodha na wahandisi wa meli hiyo wameendelea kulipwa mishahara inayofikia zaidi ya dola za Marekani 470,632 sawa na zaidi ya shilingi bilioni moja kwa miaka nane kwa mujibu wa taarifa ya hesabu  zilizokaguliwa mwaka 2019.


Waliyasema hayo juzi wakati wakichangia taarifa ya kamati ya bunge ya fedha juu ya maendeleo ya  ujenzi wa makao makuu ya baraza la bonde la ziwa Victoria ambayo makao makuu yake yapo Kisumu nchini Kenya na meli ya utafiti ya RMV Jumuiya.  


Pia watumishi hao wahandisi na manahodha hao, Peter Nkwama na Herman Bundala wakiwa hawajalipiwa gharama za kuongeza maarifa kitaaluma kwa miaka mitano  hivyo kupoteza sifa za kuendesha meli hiyo  mpaka wakaongeze ujuzi huo


Meli ya utafiti ya  MV Jumuiya  ilitolewa na shirika la maendeleo la Uingereza ,(JFID) kwa EAC Mei, 2006 na ikafanya kazi kwa miaka mitano ambapo ikasimama kufanya shughuli zake ikihitaji marekebisho madogo lakini mpaka sasa haijatengenezwa ikiwa ni zaidi ya miaka 10



Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Maryam Ussi kichangia taarifa hiyo ya kamati alisema kuwa kitendo cha EAC kuacha kuikarabati  meli hiyo kwa kipindi hicho kumeikosesha jumuiya mapato.


 

“Kwa kipindi chote wamekuwa wakiomba fedha za ukarabati huo lakini hawapatiwi na kuna watu wanalipwa  kwa ajili ya kuisimamia hii meli wakati haifanyi kazi hizi ni fedha ambazo zinapotea,” alisema Mbunge Maryam na kuongeza


 


…Tunahangaika masuala ya fedha wakati tuna mali za jumuiya ambazo zingeweza kutuingizia mapato lakini haziwezi kutokana na kuacha kutoa fedha zifanyiwe ukarabati mdogo si sahihi hata kidogo fedha zitolewe ukarabati ufanyike meli yetu ifanye kazi,”.



Kwa upande wake mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Dkt Abdullah Hasnuu Makame Dkt Makame alisema kuwa  jambo lipo katika baraza la mawaziri na kwa miaka 10 hawajachukua hatua yoyote jambo alilodai kuws linasikitisha sana



Alisema kuwa Desemba 5,2019 aliyoa hoja bungeni hapo  akitaka mawaziri wa EAC wawe wanawasilisha taarifa zao za miradi na shughuli nyingine za Afrika mashariki kwenye bunge hilo walau mara mbili kwa mwaka.


Makame alisema kuwa hiyo itawawezesha wabunge kujua utekelezaji wa maamuzi ya baraza la mawaziri wa EAC na wakuu wan chi yametekelezwa kwa kiwango gani na kwa nini hayajatekelezwa kwa lengo la kuhakikisha masuala ya mtangamano yanaenda vizuri.


 


“Tunauliza nini kimesababisha isikarabatiwe wanasema kuwa hakuna kifungu cha matengenezo,  kama mwaka wa kwanza hakukuwa na kifungu hicho ni kwa nini wasikiweke mwaka unaofuata? Kwa nini hawajaweka kifungu hicho kwa miaka 10 wakati wanajua kuna meli inahitaji marekebisho,” alihoji Dkt Makame na kuongeza.


…Hapa tunaona kuna njama za kusababisha ile meli isifanye kazi, kama siyo njama basi ni uzembe. Labda kuna watu wanafanya njama meli iuzwe kama mtumba kwa bei rahisi waichukue wao au uzembe ambapo watu wanatakiwa kuchukuliwa hatua,”.


 


 Naye mbunge wa EALA kutoka Kenya, Fatma Ibrahim alisema kuwa kuna watu wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu meli imeharibika kwa miaka 10 sasa na haijatengenezwa na ukiangalia fedha zilizotumika kuinunua ni nyingi kuliko zile zinazohitajika kwa ajili ya kuifanyia matengenezo.

Alisema kuwa meli hiyo ilifanyiwa ukaguzi kitaalam ikaonekana iko kwenye hali nzuri ikikarabatiwa itaendelea na kazi zake hivyo kuiingizia mapato EAC kwani inavyozidi kukaa bila kufanya kazi inaharibika.


Mbunge Fatma alisema kuwa hata mabaharia wa meli ya Utafiti ya Jumuiya hawajalipiwa fedha za kuongeza ujuzi kitaaluma kama ambavyo wanatakiwa kufanya  na ni fedha ndogo jambo aliloelezea kuwa linasikitisha sana kwani sheria za waendesha vyombo vya majini inataka kila mara waongeze ujuzi wapatiwe vyeti ili waweze kuwa na vigezo vya kuendesha vyombo vya majini.


 


“Tunaona kama kuna watu hawako makini na kazi yao, kama kuna kitu hatujaelewa au kama wanataka kuuza hii meli au kufanyaje. Haiwezekani EAC yote wanasikia wanaona na hawafanyi kitu ni ajabu sana,”alisema mbunge Fatma.


Kwa upande wake Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Habib Mnyaa alisema kuwa Baraza la mawaziri wa EAC hawafanyi kazi yao inavyopaswa na ndiyo wamechelewesha masuala ya kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa meli hiyo.



Alisema kuwa inasikitisha kuona kwa zaidi ya miaka mitano manahodha na wahandisi wa meli hiyo hawajaenda kozi za kuongeza ujuzi kama sheria za kimataifa zinavyotaka hivyo hawataweza kuendesha meli hiyo.


“Ripoti imebaini Baraza la Mawaziri wa EAC ndiyo wanaochelewesha haya mambo kiasi kwamba hiyo meli imekaa bila kufanya kazi lakini wafanyakazi wake wanalipwa mishahara wakati meli yenyewe haifanyi kazi inayotakikana,” alisema Injinia Mnyaa na kuongeza


…Hii meli ikikarabatiwa ina uwezo wa kuishi zaidi ya miaka 100 kwa sababu maji ya ziwa hayana chumvi lakini itawezekana kama itakuwa inafanyiwa ukarabati kwa wakati,”.


 


.


 

0 Comments:

Post a Comment