MTANDAO wa Kupinga Ukatili Kijinsia, (MKUKI) Mkoani Arusha umeamua kuelekeza nguvu katika kupinga ukatili katika vyuo vya elimu ya juu na kati mkoani hapa kwani athari zake ni kubwa kwa mhanga na Taifa kuwa na wahitimu wasio na viwango.
Hayo yamesemwa leo Novemba 26,2021na na mwenyekiti wa Mtandao huo, Joyce Mwanga wakati akiongea na waandishi wa habari juu uzinduzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yatakayofanyika kesho ambapo Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela anatarajiwa kuwa mgeni rasmi..
Amesema kuwa rushwa ya ngono kwa vyuo vya kati na elimu ya juu iko juu ukilinganisha na shule za sekondari na msingi ambapo watoto hao wanaweza kutoa taarifa kwa wazazi walezi au waaalimu.
" Rushwa ya ngono kwenye vyuo imekuwa kama imehalalishwa kiasi kwamba mtu anaona hawezi kufanikiwa mpaka atoe rushwa ya ngono nafikiri hiyo ndiyo sababu imekuwa ikishamiri kila kukicha," amesema Mwanga.
Kwa upande wake Katibu wa MKUKI, Violet Ayub amesema kuwa kutokana na utafiti uliofanywa na Mwanaidi Seleman Mahanyu akifanya utafiti wake shahada ya uzamili ya Maendelo ya Jamii iliyochapishwa mwaka 2020 kwenye wilaya ya Arumeru ulibaini kuwa kata zinazoongoza kwa ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake ni Usa River, Kikatiti na Maji ya Chai.
Violet ambaye pia ni Mkurugenzi wa taasis ya Vision for Youth,(V4Y) alisema kuwa sababu zinazopelekea mtu kufanya ukatili wa kijinsia ni pamoja na kutochangamana na watu au kuwa na historia ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia hivyo kuamua kulipiza kisasi kwa kuwafanyia wengine ukatili.
Alisema kuwa sababu nyingine ni kuwa kwenye vikundi vya vileo kama bangi na pombe ambapo hawa kufanya ukatili mpaka kwenye ngazi ya familia, masuala teknolojia ya mawasiliano na ukosefu wa elimu juu ya masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ambapo hupelekea watu kufanya ukatili.
Kwa upande wake mjumbe wa MKUKI, Faustina Nillan alisema kuwa mkuki Arusha wameweka mkakati endelevu wa kuwafikia kwa pamoja wananchi walio maeneo ya pembezoni ili kuwasaidia waweze kujua haki zao.
"Kauli mbiu ya kidunia Komesha ukatili kwa wanawake sasa na sisi tumejipanga kukomesha ukatili kwa wanawake walio vyuoni tuweze kutoa elimu zaidi lakini kikubwa zaidi wajue ni wapi waende kupata msaada wa kisheria," alisema Nillan ambaye pia ni Mkurugenzi wa Wanawake na Watoto Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT) na kuongeza.
...Tunataka wajue wamueleze nani anayeweza kuwasaidia lakini hata wale watetandaji wa vitendo hivi waweze kufahamu wanamkuki wako Arusha wanamulika kila kona kuangalia ni kwa nini wanafanya vitendo hivyo tunawaambia waache ukatili wa kingono, ukatili wa kijinai ili waweze kufahamu kwamba watashitakiwa kwa mujibu wa sheria,".
Kwa upande wake mjumbe mwingine wa MKUKI Arusha, Zukra Karunde alisema kuwa madhara ya ukatili wa kingono kwenye vyuo vikuu vikuu una madhara kubwa kwa mhanga na jamii.
"Sisi tunaangalia zaidi yule aliyefanyiwa ukatili ule lakini ukatili wa kingono anaofanyiwa kuna sababu zinazopelekea afanyiwe ukatili ule aidha anataka apatiwe alama nzuri ili aweze kufanikisha lengo lake la kuhitimu lakini adhari zake ni kubwa kwa taifa kwani tunapata wataalamu wasio wazuri kwenye jamii yetu," alisema Zukra.
Zukra ambaye pia ni mkurugenzi wa Friends For Kids Speak Out,(FRIKISO) alisema kuwa baadhi ya wahitimu wamekuwa hawafanyi vizuri kwenye usahili kutokana na kuwa akiwa chuoni alikuwa hasomi bali anategema kutoa rushwa ya ngono ili kufaulu mitihani.
Kwa miaka 30 sasa asasi za kiraia zimekuwa zikiadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kampeni hii ya kimataifa hufanyika kuanzia Novemba 25 mpaka Desemba 10 ya kila mwaka.
0 Comments:
Post a Comment