
ALIYEKUWA Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na washitakiwa wenzake sita leo wakiongozwa na askari magereza kuingia kwenye mahakama ya wazi
ALIYEKUWA Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, (34), wenzake
sita wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wamesomewa upya hati ya mashitaka
ambapo kwa sasa wanakabiliwa na mashitaka matano.
Katika mashitaka hayo Sabaya anakabiliwa na mashitaka yote matano
ya kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, kushawishi na
kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na kutakatisha fedha.
Washitakiwa sita waliobaki wakikabiliwa na mashitaka mawili kila
mmoja ya kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji fedha kinyume cha sheria.
Hati hiyo ya mashitaka imesomwa leo (Septemba 9, 2021) na Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Tarsila Gervas mbele ya hakimu mkazi, Dkt. Patricia
Kisinda anayesikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi namba 27/2021.
Washitakiwa hao walisomea mashitaka hayo baada ya upande wa
jamhuri kuwasilisha mahakamani hapo hati na kibali maalum kutoka kwa Mkurugenzi
wa Mashitaka Nchini, (DPP) zilizoipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo
ambalo linapaswa kusikilizwa kwenye mahakama kuu.
“Mheshimiwa
hakimu kama ilivyokuwa amri ya mahakama ilikuwa bado ni kutajwa. Upelelezi
umekwisha kamilika ni shauri la uhujumu uchumi mahakama yenye mamlaka ya
kusikiliza ni mahakama kuu lakini mwendesha mashitaka ameona kwa maslahi
ya umma shauri hili lisikilizwe na mahakama ya hakimu mkazi,” wakili mwandamizi
Tarsila alieleza mahakamani hapo.
Aliwasilisha
mahakamani hapo kibali na hati hiyo huku akirejea vifungu vya sheria ya uhujumu
uchumi alivyovitumia kuleta (hati na kibali hicho) kwa ajili ya mahakama kuipa mamlaka
mahakama hiyo kuendelea kusikiliza shauri hilo.
“Mheshimiwa
hakimu kwa kuwa mahakama hii imeshakuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hili
tunaomba kuwasilisha hati ya mashitaka ili washitakiwa waweze kusomewa
mashitaka yanayowakabili,” Wakili wa
Serikali Tarsila ameieleza mahakama hiyo.
Washitakiwa wengine kwenye shauri hilo ni pamoja na Enock Mnkeni,
(41) maarufu Dikdik, Watson Mwahomange, (27) maarufu Mamimungu, John
Aweyo, maarufu Mike One, Silvester Nyengu, (26) maarufu Kicheche,
Jackson Macha, (29) na Nathan Msuya, (31).
WASOMEWA
MASHITAKA
Akiwasomea
mashitaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tarsila aliieleza mahakama hiyo
kuwa, shitaka la kwanza linawakabilia washitakiwa wote saba ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume cha
sheria ya uhujumu uchumi.
Akisoma
maelezo ya kosa, Wakili huyo ameeleza kuwa, mnamo Januari 22, mwaka huu, Sabaya akiwa
katika maeneo tofauti ndani ya jiji la wilaya ya Arusha akiwa mtumishi wa umma kwa nafasi ya mkuu wa wilaya ya Hai
iliyopo mkoani Kilimanjar na anadaiwa kukiuka masharti yake ya ajira.
Sabaya
anadaiwa kushirikiana na washitakiwa wenzake sita ambao si maafisa wa serikali
lakini kwa makusudi kabisa walifanya vitendo vya uhalifu kwa kutumia nafasi ya
Lengai ole Sabaya ambaye ni mtumishi wa umma na kujipatia fedha za Kitanzania
shilingi milioni 90 kwa manufaa yao.
Katika
Shitaka la pili linalomkabili Sabaya peke yake ni la kujihusisha na vitendo vya
rushwa kinyume na sheria ya kupambana na kuzia rushwa.
Imedaiwa
mahakamani hapo kuwa mnamo Januari 22,
2021, Sabaya akiwa kwenye maeneo ya Kwamrombo yaliyo katika kwenye jiji na
wilaya ya Arusha alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kumtaka Frances Mroso
ampatie shilingi milioni 90 za Kitanzania.
Sabaya
anadaiwa kushirikiana na washitakiwa wenzake sita kama kushinikiza kupatiwa
kiasi hicho cha fedha ili wasitoe taarifa za jinai dhidi ya Mrosso ambapo kwa
wakati huo walikuwa wakimtuhumu kwamba alikuwa na makosa ya ukwepaji kodi.
Kosa
la tatu ni kujihusisha na vitendo vya rushwa, shitaka linalomkabili Sabaya peke
yake anayedaiwa kuwa mnamo Januari 22, 2021 alijihusisha na vitendo vya rushwa
kwa alijipatia shilingia milioni 90
kutoka Frances Mrosso akishirikiana na washitakiwa wenzake sita katika
kumshinikiza ili wasitoe taarifa ya kosa la jinai ambalo walimtuhumu nalo
Mrosso.
Kosa
la nne ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana
na rushwa ambalo linamkabili Sabaya peke yake ambapo anadaiwa mnamo Januari 22,
2021 akiwa kwenye maeneo ya Kwamromboo jijini na wilayani Arusha alitumia
vibaya mamlaka yake ya ukuu wa wilaya ya Hai iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Sabaya
anadaiwa kwa makusudi kabisa alimtisha Mrosso kumfungulia mashitaka ya kukwepa
kodi kinyume cha sheria za tawala za mikoa kwa madhumuni ya kujipatia shilingi milioni 90 kwa faida yake na
washitakiwa wengine sita.
Kosa
la tano ni utakatishaji fedha kinyume na
sheria ambalo linawakabili washitakiwa wote saba ambapo wanadaiwa kuwa mnamo
Januari 22, 2021 maeneo ya Kwamrombo
,
wote kwa pamoja walijipatia fedha kiasi cha shilingi milini 90 wakati wakijua
walipokuwa wakipokea fedha hizo ni zao la vitendo vya rushwa.
Washitakiwa
wote walikana mashitaka yao hivyo wakili wa serikali mwandamizi, Tarsila
aliomba mahakama ipange tarehe kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa hao hoja za
awali kuhusiana na makosa yao.
Mawakili wa utetezi Moses Mahuna na Charles Abraham hawakuwa na pingamizi na ombi hilo.
Hakimu
Mkazi, Dkt Kisinda aliahirisha shauri hilo mpaka Septemba 16,mwaka huu ambapo
washitakiwa wote walirudishwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo kutokana na
mashitaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.
MWISHO

0 Comments:
Post a Comment