Na Gift Mongi
Moshi
AZMA ya serikali ya kuwa na vituo vya afya kwenye kila kata imetajwa kushindwa kufanikiwa katika jimbo la Vunjo hivyo zinahitajika jitihada za maksudi ziongezwe kujenga vituo hivyo kwani kwa sasa jimbo hilo lenye kata 16 lina vituo vya afya vya kata viwili pekee.
Mbunge wa jimbo la Vunjo Dr. Charles Kimei aliyabainisha hayo katika ziara anayoendelea nayo ya kutembelea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo la Vunjo ambapo alisema pamoja na kuwepo kwa vituo vya afya vya taasisi binafsi lakini tatizo ni utofauti wa gharama za matibabu.
Katika ziara yake kwenye kata ya Kahe Mashariki kijiji cha Ghona aliweza kubaini ukosefu wa kituo cha afya licha ya wananchi kuanzisha ujenzi wake kwa kuweka msingi uliogharimu zaidi ya milioni 16 na kwa sasa haijaendelezwa.
Alisema vituo vingi vinamilikiwa na watu binafsi zikiwemo taasisi za dini na kuwa vituo vingine hutoza gharama kubwa ambazo wananchi wengi wanashindwa kuzimudu tofauti na ambapo ingekuwepo vile vya serikali
"Vituo vingine hawatumii bima za afya wanataka fedha taslimu ndio maana gharama za matibabu zinakuwa ni msalaba mkubwa kwetu hususani watu wa Vijijini"alisema
Alisema kukamilika kwa kituo hicho Cha afya cha Ghona kutaweza kupunguza mzigo wa wagonjwa kwenye hospitali nyingine na kuwa kuna haja sasa ya serikali kuliangalia suala hilo kwa mapana kwani tayari wananchi wameshaonesha mwitikio wa kujitolea kwa ajili ya maendeleo.
Awali, mwenyekiti wa kijiji cha Ghona kata ya Kahe Mashariki, Shwaibu Adamu Mrisha alisema pamoja na eneo hilo kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ya mara kwa mara lakini bado suala la uwepo wa kituo cha afya kwenye kata yao limekuwa changamoto.
Mwenyekiti huyo aliiomba serikali kuwaunga mkono wananchi wa kijiji cha Ghona waliotoa michango yao na kuwezesha kuanzishwa kwa msingi wa jengo la kituo cha afya katika kata yao na kuwa wapo tayari kea mida wowote kuongeza nguvu pindi watakapohitajika.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ghona kata ya Kahe Mashariki akiwemo Willium Mfinanga alisema changamoto ya kutokuwepo kwa kituo cha afya maeneo ya karibu kuwa imesababisha baadhi ya akina mama wajawazito kupoteza maisha wakati wa kutembea umbali mrefu kutafuta huduma.
Katika ziara hiyo mbunge wa jimbo la Vunjo, Dr. Charles Kimei alitembelea miradi katika kata ya Kahe Mashariki pamoja na kata ya Kahe Magharibi ambapo alikagua miradi ya ujenzi wa zahanati, madarasa ya shule, maabara, vyumba vya ofisi za waalimu pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi.

0 Comments:
Post a Comment