Mbunge wa jimbo la Vunjo Dkt Charles Kimei amewaomba wadau wa maendeleo waliopo nje na ndani ya jimbo hilo kuungana na kuongeza nguvu katika ujenzi wa vivuko vilivyopo kwenye maeneo tofauti tofauti jimboni humo jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi tofauti na ilivyo sasa.
Dkt Kimei alisema kutokana na jiografia ya jimbo hilo ilivyo maeneo mengi yanahitaji vivuko imara vitakavyowawezesha wakulima na wafugaji kufikisha bidhaa zao sokoni katika kipindi kizima cha mwaka tofauti na sasa ambapo mvua zinapoanza kunyesha mawasiliano hukatika kwa baadhi ya maeneo.
Aliyasema hayo katika maeneo ya kijiji cha Mshiri kata ya Marangu Mashariki wakati akizindua kivuko kilichojengwa na wadau wa maendeleo akiwemo yeye na kugharimu zaidi ya milioni 5 ambapo wananchi wapatao 4000 wa vijiji vya Mshiri na Masia wataweza kunufaika nacho.
Alisema kutokana na hali ilivyo katika kuchangia ustawi wa jamii ni wajibu wa wadau wa maendeleo kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha zile changamoto ndogondogo wanashiriki kuzitatua ili kuweza kuchangia ukuaji wa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwa na uhakika wa kufikiwa kwa mawasiliano ya barabara.
"Tukiona kama kuna changamoto ni bora sisi tuonyeshe dira ya kutafuta suluhisho badala ya kila kitu kusubiria serikali na hata kama tutaishia njiani sasa ndipo tuende tukaombe kuongezewa nguvu kutoka serikalini"alisema Dkt Kimei
Alisema ataendelea kuiomba serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na Vijijini TARURA ili waweze kuondoa changamoto hiyo ya vivuko ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wadau wa maendeleo katika jimbo hilo ambao tayari wameonyesha mfano.
Jonas Mawalla ni diwani wa kata ya Marangu Mashariki ambapo alisema kivuko hicho kitakuwa kimerahisisha mawasiliano ya vijiji viwili ambapo wananchi walipata adha ya kuvuka ng'ambo moja kutokana na kukosekana kwa kivuko hicho hivyo kuchangia kuwakwamisha kiuchumi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mshiri John Mtui alisema kupatikana kwa kivuko hicho kutawezesha kuokoa maisha ya wakazi wa kijiji hicho ambapo mkazi mmoja alishawahi kusombwa na mafuriko wakati akijaribu kuvuka katika eneo hilo wakati wa mvua za masika Happ mwaka jana.
Katika hatua nyingine Dkt Kimei alizindua kivuko cha Koongo-Sangai kinachounganisha vitongoji vya Sawai na Kimangaro vilivyopo kata ya Mwika Kaskazini na Mwika Kusini kilichojengwa na Rotary club ya Mwika kwa gharama ya zaidi ya milioni 10 pamoja na nguvu za wananchi.
Mratibu wa ujenzi wa vivuko kutoka Mwika Rotary club Ananyise Kawiche alisema lengo la chama chao ni kutatua kero za msingi katika jamii ambapo hadi sasa tayari wameshajenga vivuko tisa katika kata za Mwika Kaskazini na Mwika Kusini pamoja na kuoteaha miti na miradi mingine
"Leo tunakabadhi kivuko hiki hapa na kuwa sio mali yetu kama Rotary ila ni mali ya wanakijiji wa Kimangaro hivyo ni wajibu wenu kukilinda na kukitunza ili kiwe endelevu na faida kwa vizazi vijavyo"alisema
Diwani wa Mwika Kusini Dan Pius alisema wannachi wa kata yake walishiriki kujenga kivuko hicho ambacho kupatikana kwake kutawezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa ukaribu zaidi kwani wananchi walikuwa wakitumia muda mwingi kuzunguka kufuata huduma hizo.
0 Comments:
Post a Comment