MWENYEKITI wa Mtaa wa Korongoni, Goodluck Lekajo, (41) ameileza mahakama kuwa wazazi wa mshitakiwa Joel Kazimoto walikamatwa na polisi mara tatu tofauti wakati wakati mshitakiwa huyo akitafutwa.
Ameeleza hayo leo mbele ya hakimu Mkazi, Pamela Meena, wa mahakama ya hakimu Mkazi Arusha anayesikiliza shauri hilo wakati alipokuwa akihojiwa na wakili wa utetezi Edmund Ngemera.
Ameeleza kuwa kuna wakati mama yake Joel alikamatwa na polisi na wakati mwingine alikamatwa binti (hakumtaja jina) akiwa barabarani.
"Tulishakaa kikao na Sunda, (Emanuel Wado) nyumbani kwa mzee Kea (baba wa mshitakiwa) akatueleza sababu za kamata kamata watu wa familia ya Mzee Kea," ameeleza shahidi huyo wa nne upande wa jamhuri.
Lekajo ameieleza mahakama kuwa kwenye kikao walikuwa Sunda, askari polisi, Rajabu Isaya, Jeremiah ambaye ndiye alimtafutia kazi Joel nyumbani kwa Sunda na kaka yake Joel, Kazimoto.
Hata hivyo aliieleza mahakama hiyo kuwa alipata taarifa kuwa kabla ya kikao hicho Sunda na mke wake, ambaye hakumtaja jina walishafika nyumbani kwa mzee Kea mara mbili na kufanya kikao ingawa mara mara zote uongozi wa mtaa haukushirikishwa.
Lekajo ameeleza kuwa kwenye kikao kilichoitwa kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Arusha ambapo hakumbuki tarehe wala mwezi, mlalamikaji akiwa familia ya mzee Kea ambao walikuwa wanalalamikia kamata kamata ya mara kwa mara ambayo walikuwa hawajui nini sababu.
Anaeleza kuwa mshitakiwa Joel alipopigiwa simu alisema kuwa kama ni kwa mkuu wa wilaya atakuja na kweli alifika.
Awali shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa mwishoni mwa mwaka 2019 siku asiyoikumbuka alimuuzia Joel kiwanja mtaa wa Mkonoo kata ya Terati ingawa alishindwa kuwasilisha mkataba wa mauziano.
Shauri hilo limeahirishwa mpaka Mei 4, mwaka huu litakaporudi kwa upande wa jamhuri kuendelea kutoa ushahidi ambapo mshitakiwa amerudishwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo.
WAANDISHI WAPATA WAKATI MGUMU
Katika hatua nyingine shauri hilo lilichelewa kuanza kwa zaidi ya dakika 40 kuanzia saa 6:15 mchana mpaka 6:50 mchana baada ya hakimu anayesikikiza shauri hilo kudai waandishi wa habari wameandika vibaya habari kuhusu shauri hilo.
Wakili wa serikali, Grace Madikenya aliyekuwa amesimama kwenye mlango wa chumba cha mahakama aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wasingeweza kuingia kusikiliza shauri hilo kwani waliripoti vibaya kesi hiyo.
Waandishi walimweleza ni vema wakawasiliana na mwandishi wanayemlalamikia badala ya kuwazuia waandishi ambao hawahusiki na hiyo habari wanayoilalamikia iliyoandikwa kwenye blog moja, (si hii).
Wandishi wa habari walimweleza kuwa wamefuata taratibu zote ikiwemo kufuata barua ya utambulisho kwa mtendaji mkuu wa mahakama kuu kanda ya Arusha ambapo wakili Madikenya alisisitiza mahakama ndiyo imeamua hivyo kisha akawaruhusu waandishi kuingia kuonana na hakimu.
Hakimu Meena baada ya kuonyeshwa barua ya mtandaji wa makama aliwaeleza waandishi kuwa kwa kuwa waliripoti vibaya ikiwemo kukosea majina yake na wakili wa serikali hivyo itabidi awasiliane na viongozi wake ambapo aliamuru mawakili wa pande zote, mshitakiwa pamoja na waandishi kusubiri nje.
Hata hivyo baada ya kuwasiliana na viongozi wake aliwaita waandishi kisha akaisoma barua hiyo akasema mtu aliyeisaini barua hiyo, L Mrutu na kuogonga muhuri kwa niaba ya mtendaji mkuu wa mahakama hastahili.
Hata hivyo waandishi walimweleza kuwa wao walifuata utaratibu wa kufika kwenye ofisi ya uhusiano ya mahakama kisha wakapatiwa barua kama aliyewapa anastahili au la hilo ni suala la mahakama.
Bado hakimu Meena aliendelea kufanya mawasiliano na viongozi wake kwa njia ya simu ambapo aliwaambia waandishi waende na barua hiyo kwa hakimu mkazi mfawidhi ili aridhie waandishi kuingia mahakamani.
Waandishi walifika kwa hakimu mkazi mfawidhi ambaye ofisi yake iko kwenye jengo lingine ambapo baada ya mwandishi kumweleza sababu za kufika kwake na kumuonyesha marua hiyo aliwaambia wakaripoti ili mradi wafuate taratibu za mahakama ikiwemo kutokupiga picha wakati mahakama inaendelea.
0 Comments:
Post a Comment