YALIYOJIRI SAMIA AKIPOKEA TAARIFA YA CAG NA TAKUKURU


Aliyosema Rais, Samia Suluhu Hassan

Nimefurahishwa sana na mbinu hii (real time audit) kwa sababu itasaidia kubainisha mapungufu mapema na pia kuokoa matumizi mabaya ya fedha za umma.

 Naomba nitoe agizo kwako na kwa TAKUKURU kwamba CAG uende ukapitie fedha zote zilizotoka kuanzia Januari hadi Machi kwenda kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, tunataka kuziona.

 Katika ripoti yako nimeona ubadhirifu uliofanywa katika Shirika la Bandari, naomba TAKUKURU, hii ni kazi maalumu mkaishughulikie, najua Waziri Mkuu aliunda kamati na wakafanya uchunguzi kidogo pale na hatua chache zikachukuliwa lakini imani yangu ni kwamba ndani ya shirika kuna ubadhirifu wa kama bilioni 3.6 lakini Waziri Mkuu amefanya ukaguzi na waliosimamishwa ni watumishi wa chini. Naomba mara moja nitoe agizo la kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa Bandari halafu uchunguzi uendelee.

Kuna upotevu mkubwa wa fedha TAMISEMI na TAMISEMI wanafanya kama sheria zinazotungwa Serikali Kuu kuwa wao haziwahusu na hili Marehemu Mheshimiwa Rais ameshakwambia mara mbili mara tatu, naomba (Jafo) ukasimamie mapato na matumizi ya TAMISEMI.

 CAG naomba sana ulimi wako usiwe na utata, kama kuna Shirika halifanyi vizuri, tuambie kwamba hili halifanyi vizuri, kama Bodi haisimamii vizuri,  tuambie Bodi hii haisimamii vizuri, kwa sababu tutakaposema mapungufu ndio tutakapoweza kurekebisha na tukaweza kufanya vizuri zaidi. Tukinyamaziana kwa kutazamana sura hatutarekebisha na tutawaumiza wananchi. Naomba sana ripoti yako iwe wazi zaidi.

 Ukiangalia idadi ya kesi mlizo nazo, na zile ambazo mmezifanyia kazi na ziko mahakamani karibu ni nusu kwa nusu. Kuliko kujirundikia kesi, angalieni zile ambazo hazina misingi ya kukupeni uhalali wa kupeleka mahakamani, basi mzifute ili muondoe mzigo kwenye faili zenu lakini zile ambazo zina uhalali, mzifanyie kazi kwa kasi na muweze kuzifikisha kunakotakiwa.

 Moja ya mambo makuu katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ni kupambana na rushwa na ufisadi, tutaendelea kudhibiti rushwa na kuimarisha mifumo ya utawala bora na kukuza uwajibikaji katika Taifa letu, kwa hiyo niwahimize kwamba mambo yaliyoainishwa kwenye Ilani yetu kama muongozo wa mapambano dhidi ya rushwa yatekelezwe.

 Wale waliopo kwenye taasisi mbalimbali za Serikali, mashirika ya umma hata mashirika binafsi, nawaomba sana tufuate maadili ya taasisi zetu na sheria zetu ili kurahisisha kazi ya CAG na TAKUKURU. Haipendezi watu walioelimika na waliopewa dhamana kufukuzwa au kusimamishwa kazi kwa sababu ya wizi, haipendezi.

Aliyosema Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo

 Mheshimiwa Rais, taarifa ya utendaji kazi inayowasilishwa kwako ipo katika maeneo makuu matatu: Uchunguzi na huduma za kisheria, Uzuiaji rushwa na Uelimishaji Umma.

 Kwa ujumla, kwa mwaka 2019/2020,  TAKUKURU imefanikiwa kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa asilimia 89.8 tofauti na malengo ya mwaka 2018/2019 ambapo utendaji wa Taasisi ulifikia asilimia 88.1, ongezeko hili limetokana na kukamilishwa kwa uchunguzi wa majalada 1,079 ikilinganishwa na majalada 911 yaliyokamilishwa kwa mwaka 2018/2019.

 Ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za Umma katika utekelezaji  wa miradi ya maendeleo ambapo miradi yenye thamani ya shilingi Trilioni 11.08 ilifuatiliwa ikilinganishwa na miradi ya Trilioni 1.67 iliyofuatiliwa kwa mwaka 2018/2019.

Elimu ya kina kuhusu madhara ya rushwa, juhudi za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi katika vita dhidi ya rushwa imetolewa kupitia njia mbalimbali ambapo semina 3,683 zilitolewa ikilinganishwa na semina 2,513 za mwaka 2018/2019.

Mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi 3,866 ilifanyika ikilinganishwa na 3,273 ya mwaka 2018/2019.

Aliyosema Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ndg. Charles Edward Kichere

 Nimefanikiwa kufanya ukaguzi wa kitaalamu kwenye miradi sita ya kimkakati. Kwenye kaguzi hizo, ofisi yangu imetumia mbinu mpya ya ukaguzi ambayo  inahakikisha kwamba ukaguzi unafanyika kadiri ya mradi unavyoendelea kutekelezwa.

Mbinu hii ya ukaguzi inawezesha mapungufu yanayoonekana kufanyiwa kazi kwa wakati badala ya kusubiri mradi ukishatekelezwa ndio tunaenda kutoa mapendekezo.

Tutaendelea kutumia mbinu hii ya ukaguzi kwenye miradi ili kutoa ushauri kwa Serikali mapema ili kama kuna hatua za kuchukuliwa zichukuliwe mapema ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

 Mheshimiwa Rais, miradi ambayo nimefanya ukaguzi ni Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar-es-Salaam hadi Makutupora; mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP); mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kwa DSM (UDART) Gerezani mpaka Mbagala; upanuzi wa barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kibaha; mradi wa usambazaji maji wa Same, Mwanga na Korogwe; na mradi wa uzalishaji sukari huko Morogoro.

 Mheshimiwa Rais, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 nimetoa jumla ya hati 900 za ukaguzi ikiwa hati 243 za Serikali Kuu, hati 185 za mamlaka ya Serikali za mitaa, hati 165 za mashirika ya umma, hati 290 za miradi ya maendeleo, na hati 17 za vyama vya siasa.

 Katika mamlaka ya Serikali ya mitaa, nimekagua hati 185, hati zinazoridhisha ni 124, hati zenye mashaka ni 53, hati mbaya ni 8. Sikushindwa kutoa maoni kwenye halmashauri yoyote.

 Katika mashirika 165, mashirika 162 yana hati zinazoridhisha, hati zenye mashaka ni 3, na hakuna hati mbaya wala niliyoshindwa kutoa maoni kwenye shirika lolote.

# Katika Serikali Kuu nimetoa hati 243, hati ya hati 235 ni hati zinazoridhisha, hati zenye mashaka ni 6, hati mbaya ni 2.

# Katika vyama vya siasa, nimetoa hati 17, hati zinazoridhisha ni 4, hati zenye mashaka ni 4, hakuna hati mbaya lakini nimeshindwa kutoa maoni kwenye hati 9, vyama vya siasa 9 nimeshindwa kutoa maoni kwa sababu hesabu zao hazikuzingatia utaratibu wa kutengeneza hesabu na wengine hawakuleta kabisa hizo hesabu ili niweze kuzikagua.

# Katika miradi ya maendeleo, nimekagua miradi 290, hati zinazoridhisha ni 275, hati zenye shaka ni 15, hakuna hati mbaya wala hati ambazo nimeshindwa kutoa maoni.

*Imeandaliwa na Idara ya Habari - MAELEZO*

0 Comments:

Post a Comment