WAKULIMA wa ngano wilayani Karatu wamesema kwa sasa wamepata matumaini mapya ya kuinuka kiuchumj baada ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, (CPB) kuwapatia mbegu bora.
Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa kilimo, Gilala AMCOS, Joseph Panga aliyasema hayo juzi wakati wakikabidhiwa tani 18.48 ya mbegu bora ngano na Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa CPB, Hiza Kiluwasha.
Alisema kuwa kwa sasa wanamatumaini makubwa ya kufanikiwa kiuchumi kupitia mkataba walioingia na CPB wa kununua mazao yao yote huku wakipatiwa mkopo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini,(TADB) ambapo wamelikatia zao hilo bima.
" Sisi tunafurahi kwa sababu zamani ulikuwa unapanda ngano mpaka unavuna haujui bei. Ilikuwa ukivuna unapambana na mteja anayejitokeza na bei yake. Kwa sasa tuna uhakika na bei,alisema Panga na kuongeza.
"Kwenye mkataba tulioingia na CPB pamoja na benki ulitufungua macho kwa sababu ulitutaka tukate bima. Kwa sasa tumeshakata hivyo hata yakitokea madhara ya ukame au majanga mengine basi bima itafanya kazi,".
Jumla ya wanaushirika 62 wamehamasika kulima ngano hiyo ya chakula ambapo wana jumla ya ekari 308 na wamepatiwa tani 18.48 ya mbegu bora ya ngano huku wakitarajia kuvuna zaidi ya tani 1.2 kwa kila ekari moja waliyoilima.
Akiongelea historia ya kilimo cha ngano kwenye kijiji hicho cha Kilima Tembo kilichoponkata ya Rotya, Panga alisema kuwa waliacha kulima ngano ya chakula baada ya vyama vya ushirika kufa miaka ya 70 kwani hawakuwa na uwezo wa kupata mbegu bora hivyo wakahamia kwenye kilimo cha mazao mengine ikiwemo shayiri, mahindi na maharage.
"Tulikuwa tukitaka kulima ngano ya chakula tulikuwa tunatafuta kwa wakulima walioleta mbegu kutoka maeneo mengine. Tukiona mbegu zimetoka mbali tulikuwa tunaona walau inaweza kuwa nzuri kuliko zetu ambazo zimechoka," alisema Panga na kuongeza
...Hata hatukuwa na soko la uhakika, tulikuwa tunabahatisha tunakutana na walanguzi huko vijijini mnavutana wanawapa bei ndogo kwasababu ngano haina ubora wowote hata mbegu zake ni mbovumbovu unakuta wakati mwingine zimeshachanganyikana na shayiri,".
Mkulima wa ngano tokea kijiji hicho, Desderi Male alisema kuwa amefarijika kwa ushirikiano waliopatiwa na CPB, anaamini baada ya mavuno hali ya uchumi wa wakulima kijijini hapo itabadilika na kuwa nzuri.
Mkulima mwingine, Tulifurahi bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko imetuletea mbegu bora. Tunatumaini wanatuleteza mbegu hii itatupa mavuno mengi kama ilivyokuwa miaka ya 70 wakati serikali ilipokuwa ikitupa mbegu bora za ngano tukawa tunapata mavuno mengi.tunasema labda tutarudia pale.
CPB YASISITIZA WATANUNUA NGANO YOTE
Meneja wa CPB Kanda ya Kaskazini, Kiluwasha aliwahimiza wakulima hao wafuate kanuni bora za kilimo ili wapate mavuno mengi na bora huku akiwahakikidhia kuwa wataalam wao watakuwa wakipita kwenye maeneo hayo mara kwa mara kwa ajili ya kutoa ushauri .
"CPB itahakikisha wataalam wetu wanakuwa pamoja na wakulima kuanzia wanapopanda ngano shambani mpaka wakati wa kuvuna.Nina uhakika wakulima watanufaika kwani mbegu hizi tumezileta kwa wakati sahihi. Kwa sasa msimu kupanda ngano umeanza," alisema Kiluwasha
Alisema kuwa CPB itanunua ngano yote ya wakulima walioingia mkataba nao hivyo ngano hiyo ikishavunwa watainunua na kwenda kuichakata kwenye kinu chao kilichopo jijini Arusha.

0 Comments:
Post a Comment