MKUU wa mkoa wa Arusha,Idd Kimanta ametaka juhudi za pamoja za wadau kuhakikisha huduma ya maji safi na salama zinawafikia wananchi wote maeneo ya vijijini ikiwa ni kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025.
Kimanta ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Wakala wa usambazaji maji vijijini (Ruwasa)mkoa wa Arusha wenye lengo la kutambulisha wakala huyo na shughuli zinazofanywa kwa watendaji wa serikali na wadau wanaojihusisha za sekta ya maji.
Amesema jumla ya vijiji 86 katika mkoa huo havina huduma rasmi ya maji kabisa ambayo ni sawa na asilimia 22.1 ya vijiji vyote hali ambayo inawanyima wananchi wengine kupata haki za msingi za huduma ya maji safi na salama.
“Upatikanaji wa maji safi na salama uwe kipaumbele kwa wananchi vijijini ili kuboresha maisha na afya zao kwa ujumla,ikizingatiwa Rais John Magufuli alisisitiza wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 upatikanaji wa maji vijijini ufikie asilimia 100,”amesema Kimanta
Amesema mkoa huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya maji hasa maeneo ya wilaya za wafugaji ambazo ni Monduli,Ngorongoro na Longido huku wilaya za Arumeru,Arusha na Karatu kuwa maeneo hayo yana maji ila hakuna mgawo mzuri wa huduma ya maji.
Kimanta amesema kipindi cha kwanza cha awamu ya tano ya Rais John Magufuli lengo lilikua upatikanaji wa maji vijijini unafikia asilimia 85 lakini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mkoa wa Arusha ulipiga hatua kwa asilimia 2.1 na kufanya upatikanaji wa maji kuwa asilimia 69.12 pekee.
“Kuna miradi ya maji ambayo imechukua muda mrefu kukamilika tumeelekeza fedha za kutosha kuhakikisha inakamilika kwa wakati ambayo ni vijiji vya Piyaya, Pinyinyi ,Oldonyosambu na Masusu wilayani Ngorongoro,”amesema Kimanta.
Meneja wa Ruwasa mkoani Arusha,Emmanuel Makaidi amesema lengo la mkutano huo wa wadau ni kufahamiana na mashirika binafsi yanayojihusisha na utoaji wa huduma za maji ili kujenga mipango ya pamoja katika kuwahudumia wananchi.
Imeandikwa na Happy Lazaro, Arusha.

0 Comments:
Post a Comment