KATIBU mkuu wa wizara ya maji,Injinia Anthony Sanga ameitaka mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (AUWSA) kwa kushirikiana na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) kuongeza kasi ya usambaji wa maji kutoka wilaya ya Longido kwenda mji wa Namanga hadi kufikia julai badala ya agosti .
Ameyasema hayo wakati alipotembelea mradi huo na kujionea shughuli ya kulaza mabomba kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa usambazaji wa maji kuelekea mji wa Namanga ambapo zoezi hilo lilishaanza tayari.
Injinia Sanga alisema kuwa, mabomba hayo yanalazwa kutoka wilaya ya Longido Hadi mji wa Namanga ambapo ni kilometa 43 na mradi huo utagharimu kiasi Cha shs 4.58 bilioni ambapo fedha hizo zimetolewa na serikali ya awamu ya tano kupitia Rais John Pombe Magufuli.
Amesema kuwa ,mradi huo ambao umeanzia mto Simba mkoani Kilimanjaro hadi wilayani Longido umegharimu kiasi Cha shs 15.8 milioni na una kilometa 63.
Naye Mkurugenzi mkuu wa RUWASA,Clement Kivegalo alisema kuwa,uwepo wa mradi huo utatatua kwa kiasi kikubwa Sana matatizo ya wananchi yaliyokuwa yakiwakabili ya ukosefu wa maji.
Alisema kuwa, kupitia mradi huo wananchi kutoka vijiji 30 wataunganishiwa maji kupitia mradi huo wa maji kutoka wilaya ya Longido hadi mji wa Namanga ambapo aliomba kuharakishwa kwa mradi huo hadi mwezi wa sita ili wananchi wengi waweze kunufaika na mradi huo kwa haraka.
![]() |
Baadhi ya mabomba yakishushwa katika eneo la mradi wa maji Longido kwenda mji wa Namanga kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo unaoanzia Longido kwenda mji wa Namanga (Happy Lazaro)```
Naye Mkurugenzi wa AUWSA mkoani Arusha ,Injinia Justine Rujomba alisema kuwa mradi huo ulishaanza tangu mwezi huu ambapo zoezi la kulaza mabomba limeshafikia zaidi ya kilometa 10 na wanaendelea na zoezi la uchimbaji wa mtaro .
Alisema kuwa,watahakikisha wanaongeza kasi ya usambazaji wa mabomba na uchimbaji wa mitaro na kuhakikisha wananchi wanapata maji hadi kufikia mwezi wa sita .
Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mradi huo kwani wananchi wanaenda kupata maji safi na salama toka mto Simba wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Injinia alisema kuwa,changamoto iliyopo hivi Sasa ni tembo kuharibu miundombinu ya maji ambapo wanaangalia namna ya kuwatengenezea sehemu maalumu kwa ajili ya wanyama kunywa maji.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Longido,Juma Mhina amesema kuwa,mradi huo utavinufaisha vijiji vitatu ambavyo ni Namanga,Kimokoa, na Olendeki ,hivyo alitaka kuharakishwa kwa mradi huo ili wananchi waweze kunufaika kwa haraka zaidi.
Mhina alisema kuwa, watahakikisha wanaweka timu kubwa katika kutekeleza majukumu hayo ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati katika muda uliopangwa na hivyo wananchi kuweza kuondokana na adha ya maji ambapo zaidi ya wananchi 13,000 wanatarajia kunufaika na mradi huo.
Imeandaliwa na Happy Lazaro, Arusha


0 Comments:
Post a Comment