WAKATI TUNAMUOMBA MUNGU TUSISAHAU KUCHUKUA TAHADHARI

 

Mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa CCM,  (UWT)wilaya ya Moshi Vijijini, Grace Mnzava 


JAMII imetakiwa kumgeukia Mungu na kuendelea kumuomba kama Taifa atuepushe mbali na ugonjwa hatari wa corona ambao umesababisha vifo vya watu wengi ulimwenguni kote sambamba na kuchangia shughuli za kiuchumi kusimama.


Katika kufanikisha jambo hili wanawake ambao ndio walezi wakubwa wa familia wametakiwa kuwa mstari wa mbele kwa kuhimiza maombi hayo sambamba na kuendelea kuchukua tahadhari muhimu zinazotolewa na wataalamu wa afya mara kwa mara kwenye familia zao.


 Mwenyekiti wa umoja wa wanawake nchini, (UWT), wilaya ya Moshi Vijijini, Grace Mnzava, alisema licha ya kuwa jamii bado inachukua tahadhari lakini msisitizo ni lazima uwekwe na watu waone umuhimu wake na baada ya hapo ndipo maombi yafanyike sasa.


Alisema kuwa watu wengi hujisahau kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya na badala yake hukimbilia kwenye maombi pekee jambo ambalo sio sahihi kwani Mungu alituumba kwa mfano wake na kutupa akili ya kuweza kujua jema na baya.


"Ninaamini tukimlilia Mungu kama Taifa na kila mtu kwa imani yake tunaendelea kubaki salama kama alivyotuepusha tangu mwaka jana ila maombi haya yaendane na kuchukua tahadhari jamani na kina mama ndio walezi huu ni wajibu wenu pia"alisema Mnzava.


Alisema kila jaribu limpatalo mwanadamu huwa na njia ya kutokea kama lilivyoweza kuwa na njia ya kuingilia ila jambo la msingi ni kuungana na kumuomba Mungu naye atatusikia kwani hawezi kutuumba kwa mfano wake alafu akubali tuteseke.


Alisema kuwa maono yakumgekia Mungu katika kipindi hiki yalitangazwa na rais, Dkt, John Magufuli wakati akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa katibu mkuu kiongozi marehemu, Mhandisi, John Kijazi na kuwa kama Taifa halina budi kufanya hivyo kwani matokeo yalionekana mwaka jana na kila mtu asimamie imani yake na maombi yataenda kujibiwa.


"Tunamshukuru Mungu kwa yote na tuzidi kumuomba wenzetu ulimwenguni wanateseka kwa kufungiwa ndani lakini kwetu sisi kwa hisani ya Mungu bado tupo tunaendelea kuchapa kazi na kuwa haya yote yataenda kufika mwisho tu,"alisema Mnzava.


Askofu mkuu wa kanisa la Furaha nchini Ainea Mola alisema suala la maombi katika kipindi hiki dunia inapita katika kipindi kigumu si la viongozi peke yake bali ni la kila mwanadamu kwani athari zimeonekana kwa mataifa mengine tayari.


"Kumuomba Mungu katika hiki kipindi sio jambo la mchungaji pekee bali ni la kila mmoja wetu kwa Imani yake na kuwa nguvu ya maombi ilionekana mwaka jana ambapo ugonjwa wa corona ulivyoingia nchini"alisema Askofu Mola.


Alisema viongozi wa kiserikali kwa sasa wanatakiwa kutiwa moyo na kufarijiwa kwa kipindi ambacho kama taifa tunapitia na ili tisiweze kukumbwa na madhara makubwa Kama ilivyotokea kwa wenzetu duniani ambapo shughuli zimesimama na vifo vikiongezeka.

Imeandikwa na Gift Mongi,Moshi

0 Comments:

Post a Comment