ANAYEDAIWA KUUA WANAWAKE ARUSHA ANASWA NA POLISI, USHIRIKINA WATAJWA

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Salum Hamduni


 JESHI la polisi mkoani Arusha linamshikilia Mbise Lukumo, (30) kwa tuhuma za mauaji ya wanawake mbalimbali jijini hapa likiwemo la Anna Edward,(44) aliyeuawa januari 25, mwaka huu na kupelekea maandamano makubwa ya wanawake.


Kamanda wa polisi mkoani hapa, Salum Hamduni amewaeleza waandishi wa habari leo ofisini kwake kuwa, Lukumo ambaye ni mkazi wa Olasiti, jijini hapa alikamatwa januari 27, mwaka huu.

"Baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika na tukio hilo la mauaji pamoja na matukio mengine yaliyotokea siku za nyuma," alisema kamanda Hamduni.

Aliyataja matukio mengine ya mauaji ya wanawake mtuhumiwa huyo anayodaiwa kukiri kuyafanya ni pamoja na lile la Mei 21, 2019 lililotokea Lolovono jijini Arusha ambapo Lukumo alikiri kushirikiana na  wenzake kumuua Stella Daniel, (22).

Tukio lingine ni lile la januari 16, mwaka huu lililotokea maeneo ya Ngaramtoni ya chini ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa akishirikiana na wenzake walimuua mwanamke, Bahati Prosper, (35).

"Baada ya kumhoji zaidi aliwataja washirika wenzake ambao ni Lembeka Olomorojo, (65) mkazi wa Osunyai jijini Arusha ma Bashiri Msuya ,(64), mganga wa kienyeji mkazi wa Kirika B, kata ya Osunyai jijini Arusha," amesema kamanda Hamduni na kuongeza.

"Hata hivyo chanzo cha tukio hilo imebainika kwamba  ni imani za kishirikina. Mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya mashitaka kwa hatua zaidi za kisheria,".

Januari 30, mwaka huu wanawake waliandamana na kufunga barabara ikiwa ni njia ya kufikisha ujumbe kwa serikali juu ya matukio ya mauaji ya wanawake yaliyoonekana kukithiri.

Maandamano hayo yalifanyika siku ya mazishi ya Anna mkazi wa kona ya A to Z kata ya Matevezi jijini Arusha ambapo mandamano hayo yalivuta hisia za wengi jijini hapa.

 

0 Comments:

Post a Comment