UNGA CHAPA NGUVU WAWAPA MAFANIKIO CPB

 



BODI ya Nafaka na Mazao mchanganyiko,(CPB) tawi la Arusha imetengeneza faida ya zaidi ya shilingi milioni 800 kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu wakabidhiwe rasmi
kinu cha kusaga mazao cha iliyokuwa Shirika la Taifa la usagishaji, (NMC) mkoani Arusha.

Kinu hicho cha kukoboa na kusaga nafaka kilikuwa chini ya mwekezaji mzawa kampuni ya Monaban tokea mwaka 2008 ambapo kilirejeshwa serikalini Juni, mwaka uliopita.


Kaimu meneja wa CPB, tawi la Arusha, Idd Mkolamasa anasema kuwa wanafarijika kwa mafanio waliyoweza kuyapata kwa kipindi hicho ingawa anaona wanahitaji kuongeza juhudi na maarifa ili wafanye mambo makubwa zaidi.

Anasema wakulima wamenufaika kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja kwani wamenunua mahindi yaokiasi cha zaidi ya tani 6,000 .

Wameandaa mazingira kuhakikisha wakulima hao wananufaika na uwepo wa kinu hicho mkoni hapa kwa kuandaa utaratibu kuingia nao mkataba wa kununua mazao yao jambo litakalowapa uhakika wa soko wakulima hao.


Mkolamasa anasema, sehemu kubwa ya faida hiyo imetokana na biashara ya unga wa mahindi chapa Nguvu ambao umetokea kupendwa na wananchi kutokana kuwa na ladha nzuri na virutubisho vingi.

"Kwenye biashara ya unga wa chapa Nguvu ambao dona bora na sembe bora  tumepata faida ya zaidi ya shilingi milioni 500 na kwenye maghala yetu tunayokodishia taasisi nyingine kuhifadhi nafaka zao tumepata faida ya zaidi ya milioni 300," anasema Mkolamasa.

Anafafanua kuwa sababu ya unga wao kupendwa ni namna wanavyouandaa kwa usafi na utaalam wa hali ya juu kwa kuhakikisha viini lishe vya protini na mafuta ambavyo ni muhimu katika kuujenga na kuupa joto mwili vinabaki.

"Unga wetu tunauzalisha kwa usafi wa hali ya juu ili kumlinda mlaji. Mara baada ya kuingiza mahindi kiwandani tunahakikisha tunayapitisha kwenye mitambo yetu kwa ajili ya kuyapembua ili kuondoa takataka zote ikiwemo mawe na misumari," anasema Kaimu Meneja huyo wa CPB  tawi la Arusha na kuongeza.

" Tukishahakikisha mahindi yako safi tunapitisha kwenye mashine maalum kwa ajili kurahisisha umenyaji wa ganda la juu wakati wa kusaga kisha tunayasafisha ili kuhakikisha yanakuwa safi kabisa,".


Mkolamasa anasema kuwa unga chapa nguvu unapatika kwenye ujazo tofauti wa kilo moja, tano, 10 na 15 ambapo umekuwa ukiuzwa mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani ya Kilimanjaro, Manyara na Tanga ambapo hivi karibuni wanatazamia kufungua kituo cha mauzo Same mkoani Kilimanjaro.

"Kwenye vifungashio hatujajifunga sana, endapo mteja atasema anahitaji unga kwenye kifungashio chake cha mbili, 25 au 50 tutamfungia. Sisi tuko kibiashara hivyo mteja akiona soko lake lina uhitaji huo sisi tutamhudumia," anasema Mkolamas.

WAJIVUNIA SOKO LA BIDHAA ZAO

Anasema wanaendelea kujitanua kimasoko na wamejipanga kufungua vituo maalum vya mauzo kwenye maeneo ya Horohoro mkoani Tanga, Tarakea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na Babati mkoani Manyara.

Kaimu meneja huyo wa CPB tawi la Arusha anasema kuwa wamekuwa wakiuza unga huo kwenye shule mbalimbali pamoja na taasisi za serikali kama jeshi la Magereza, Chuo cha Mafunzo ya kijeshi Monduli ambapo wanaendelea na mazungumzo na chuo cha polisi moshi, (CCP) ili wakifikia makubaliano wawe wanawauzia unga wao.

Anasema, Kenya ni moja ya wateja wao wakubwa kwani wamekuwa wakiuza unga wa mahindi pamoja na pumba jijini Nairobi ambapo wakati mwingine hutumia mawakala wao waliopo kwenye maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

"Tuna mpango wakufungua kituo cha mauzo pale Horohoro, (mkoani Tanga) basi kama ndugu zetu wa Kenya wanataka kufanya biashara na sisi hawatakuwa na ulazima wa kuja huku Arusha atashughulikiwa palepale na sisi tutamsaidia kutafuta vibali," anasema Mkolamasa.


Kiwanda hicho kimeajiri  wafanyakazi 16 huku kikiajiri kwa mkataba wafanyakazi 25 ambapo kiwanda hicho kimekuwa kikifanya kazi siku tano za wiki usiku na mchana ingawa wanapokuwa na oda kubwa ya unga huendelea na kazi mpaka siku za jumamosi na jumapili.

CHANGAMOTO 

Anasema kuwa ubora duni wa mahindi kutoka kwa wakulima umekuwa ni changamoto ambapo wamejipanga kuona uwezekano wa kuingia mkataba na wakulima ili waweze kuzalisha mahindi bora wanayoyahitaji ambapo watawapatia mbegu na elimu ya kulima mahindi hayo.

"Wakati mwingine wakulima wanakuja na mahindi yao ukiyapima unakuta hayajakidhi ubora. Unapoyakataa anaona unamuonea na hii tunadhani wakulima wanahitaji elimu zaidi kwani matatizo hayo mara nyingi husababishwa na mahindi kuvunwa mapema au kabla hayajakomaa hivyo yanakuwa madogo ambapo sisi tukisaga yatatupa unga mdogo," anafafanua Mkolamasa.



Anasema kuwa tayari wamepata mkandarasi kwa ajili ya kufanyia ukarabati wa mitambo ya kiwanda hicho pamoja na majengo ya kiwanda hicho ili yawe bora zaidi.

NAMNA WANAVYOONGEZEA THAMANI MAZAO

Majukumu ya CPB ni pamoja na yale ya kibiashara ambapo wananunua mazao kuyaongeza thamani kwa kuyasindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali kisha kuyauza. 

Aidha wanashirikiana na wadau wengine katika kuendeleza biashara ya nafaka na mazao mengine .

"Shughuli kubwa tunayofanya hapa Arusha ni uzalishaji wa unga wetu wa mahindi wa chapa NGUVU ambapo tunanunua mazao toka kwa wakulima, tunayasafisha na kuyatunza kwenye ghala huku tukiendelea na uzalishaji kulingana na mahitaji ya soko," anasema Mkolamasa.

Anasema tangu waanze kazi kwenye kinu hicho mwaka mmoja uliopita uzalishaji haujawahi kusimama ambapo wanazalisha tani 45 kwa siku.

Kiwanda hicho kinafanya kazi siku sita za wiki ingawa hali hubadilika pale wanapokuwa na kazi nyingi basi huwalazimu kufanya kazi siku saba kwa wiki usiku na mchana ambapo wafanyakazi walio kiwandani huingia kwa kupokezana.

Anasema wanajivunia uwepo wa vijenge vyenye uwezo wa kuhifadhi tani elfu 28 viko 23. Wana maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani elfu 10 hivyo kwa pamoja  vihenge na maghala yana uwezo wa kuhifadhi tani elfu 38 kwa wakayi mmoja.

WAJIPANGA KUZALISHA UNGA WA NGANO NA MTAMA

"Hapa ndani sio tu tuna kinu cha unga wa  mahindi bali kipo pia cha ngano, tuna mashine za kuchakata ngano. Tuna mpango wa kuzalisha ngano na mchakato wa kibiashara umeshafanyika kuona namna gani tutatumia malighafi za ngano za hapa nchini kuzalisha unga," anasema Mkolamasa na kuongeza.

... Mipango na majadiliano yanaendelea kufanyika kuona ni namna gani tunaingia mikataba na wakulima ili tuweze kutumia ngano sisi hapa ya kwetu wenyewe kwenye kuichakata ili kupata unga wa ngano,".

Kaimu meneja huyo anasema ngano hiyo itakuwa kwa matumizi ya nyumbani na viwandani ambapo wanatarajia mpaka kufikia oktoba mwaka huu watakuwa wameshaanza mchakato na wakulima ili waanze kulima ili mpaka kufikia mwezi juni mwakani kinu cha ngano kianze uzalishaji.

Anasema  vilevile wana kinu cha mtama ambacho wanaangalia namna gani kitaanza kutumika kwa ajili ya uzalishaji.

SIRI ILI NYUMA YA UBORA WA UNGA WAO

Mkolamasa anasema tokea wachukue kiwanda hicho juni, mwaka jana uzalishaji haujawahi kusimama na tayari wameshapata mkandarasi kwa ajili ya kufanyia ukaguzi na maboresho mitambo hiyo.

"Unga tunaozalisha sisi kwa aina ya mashine zetu wanaita 'roller mill'. Hii mashine inazalisha unga bila kuondoa kiini cha mahindi. Na kama mnavyoelewa kile kiini kina  kirutubisho muhimu sana kinachoitwa hamirojo ambapo kitaalam kinatengeneza asilimia10," anasema Kaimu Meneja huyo wa tawi la Arusha.


MARADI WA MAHARAGE MABICHI

Mkolamasa anasema kuna mazungumzo yanaendelea juu ya uzalishaji wa maharage mabichi ambapo wameshafanya utafiti na kuna soko wanalifuatilia nchini belgiji.

Anasema wameshafanya upembuzi yakinifu wa biashara yenyewe kuona namna gani watachukua maharage hayo kutoka kwa wakulima, kuyaaanda, kuyaweka kwenye vifungashio, kuyahifadhi na kuyasafirisha mpaka nchini Ubelgiji.

"Tutaingia mkataba na wakulima vikundi viko 11 sehemu mbalimbali. Kuna vilivyoko Machame wilayani Hai, Sanya Juu, West Kilimanjaro. Wakulima hawa wanalima kwa mkataba kwa sababu maharage haya yanaharibika haraka 

Maharage haya yakishavunwa ndani ya siku moja yapili imezidi iwe imeshavungwa na kupelekwa nje ya nchi. 

Anasema mkataba huo umelenga kusimamia aina ya mbegu ya maharage watakayotumia wakulima hao kwani si kila aina inakibalika sokoni. 

"Tutawapatia mbegu wakulima na kama kuna mafunzo tutawapatia ili kuhakikisha wanazalisha maharage hayo kuweza kufikia viwango vya kimataifa,'

WAKULIMA WA MPUNGA NAO WANUFAIKA

Mkolamasa anasema kwa sasa wanafungasha mchele wanaoununua toka kwa wakulima ili kuanza kuzoeleka sokoni wakati wakisubiri kukamilika kwa ujenzi wa kinu cha CBP mkoani Mwanza.

Anasema taratibu kwa ajili ya ufungwaji wa kinu hicho zinzendelea ambapo kwa sasa tayari ameshapatikana mshauri elekezi.

Hivyo mwaka mmoja wa CBP kwenye uendeshaji wa NMC jijini Arusha umeleta neema kiuchumi kwa wakazi wa jiji hili na mikoa ya jirani hasa wanaojishughulisha kilimo na biashara bila kusahau wanufaika wakuu ni walaji ambao wamepatiwa unga chapa nguvu wenye virutubisho vya hali ya juu.



MWISHO

0 Comments:

Post a Comment