Spika wa bunge la EALA, Martin Ngoga (katikati) akisoma sala ya kuliombea bunge
MJADALA mkali umeibuka kwenye bunge la Afrika Mashariki, (EALA) kufuatia hatua ya baraza la mawaziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki, (EAC) kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ya mwaka 2016/17 kwa kuchelewa na haijasainiwa.
Aidha wamesema hiyo itakuwa ni taarifa ya mwisho kupokelewa na kujadiliwa ikiwa haijasainiwa na wameagiza taarifa nyingine zipelekwe mapema bungeni hapo ili ziweze kujadiliwa.
Hayo yalijitokeza mwishoni mwa wiki wakati bunge likijadili taarifa hiyo na mapendekezo ya kamati ya bunge ya masuala mtambuka iliyowasilishwa na mbunge wa EALA, kutoka , Pamela Maassay, (Tanzania) kwenye kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao kikiongozwa na Spika wabunge hilo, Martin Ngoga.
Wabunge wa EALA wakishiriki kikao cha bunge kwa njia ya mtandao
Bunge hilo liliafiki na kuunga mkono mapendekezo ya kamati yaliyolitaka baraza la mawaziri la Jumuiya kuhakikisha wanawasilisha ripoti za utekelezaji za mwaka kwa wakati kama inavyoelekezwa na mkataba wa kuanzishwa jumuiya hiyo.
Waliazimia kuwa kuazia sasa bunge hilo halitapokea tena taarifa ya mwaka inayowasilishwa na mwenyekiti wa Baraza la mawaziri endapo haitakuwa imesainiwa.
Pia wametaka taarifa za utekelezaji ziwe zinaainisha utekelezaji viashiria vya utendaji vinavyohitajika, matokeo na athari za moja kwa moja kwa shughuli zinavyogusa maisha ya wananchi wa EAC.
Bunge hilo lililitaka baraza la Mawaziri la EAC kuharakisha mchakato wa marekebisho kamili ya muswada wa sheria ya usimamizi wa forodha na kuhakikisha inafikishwa bungeni kabla ya mkutano wa mwezi Julai, mwaka huu.
Pia walimtaka mwenyekiti wa baraza la mawaziri kuwasilisha bungeni ripoti za misheni za waangalizi wa chaguzi zinazofanyika kwenye nchi wanachama wa EAC ili kuliwezesha bunge hilo kuzipitia na kutoa mapendekezo yao.
Awali wakijadili taatifa hiyo, mbunge, Habibu Mnyaa, (Tanzania) alionyesha kushangazwa na ucheleweshwaji wa taarifa hiyo kufikishwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa jambo alilohoji zinazofuata tatu lini zitskuwa tayari.
Mbunge, Kennedy Musyoka, (Kenya) alikosoa ripoti hiyo akidai imepitwa na wakati jambo alilohoji endapo kuna manufaa yoyote kuendelea kuijadili.
Mbunge, Adam Kimbisa, (Tanzania) alihoji kama ripoti hiyo haijakamilika kutokana na kutosainiwa na walioiandaa kuendelea kuijadili itakuwa sawa kulingana na kanuni zinazolisimamia bunge hilo.
Hata hivyo ilibidi spika Ngoga kutolea muongozo suala la kwa nini wabunge waendelee kujadili taarifa hiyo licha ya kuwa haijasainiwa ili kuonyedha anayeimiliki kwa kile alichoeleza kuwa kwenye mapendekezo ya kamati limeshawekewa msimamo kuwa hiyo ni taarifa ya mwisho kujadiliwa ikiwa haijasainiwa.
Hivyo alisema kuwa suala hilo limeingia kwenye kumbukumbu za bunge hivyo ripoti hiyo itaambatanidhwa na kumbukumbu hiyo ya bunge ndipo wabunge waliridhia na kuendelea kuijadili.


0 Comments:
Post a Comment