Margareth Hovekela
CHAMA cha Walimu nchini,(CWT) wakumbuka mchango wa mbunge wa Urambo, Magreth Sitta katika kuibua na kuwajengea ujasiri walimu wanawake kushiriki kwenye uongozi.
Hayo yalisemwa juzi na mwaliju mstaafu, Margareth Hovekela wakati akitoa mada ya mwanamke na uongozi kwenye semina ya siku moja kwa wawakilishi wa walimu wanawake toka shule zote za jiji la Arusha.
Alisema kuwa miongoni mwa watu waliomuibua na kumhamasisha kugombea nafasi za uongozi ni Sitta wakati huo akiwa Rais wa Chama Cha Waalimu ambaye wakati wa uongozi wake alianzisha kitengo cha walimu wanawake.
"Mwenyekiti wa CWT jiji la Arusha (Grace Msaki) amenipa sifa ya mimi kumuibua yeye, lakini na mimi niliibuliwa wakati nikiwa mwalimu wa kawaida. Wakati huo nilikuwa naona chama cha waalimu si kitu cha maana ila walinishawishi na nikajaribu nikawa mwakilishi wanawake mkoa wa Arusha," alisema Hovekela.
Alisema kuwa wakati huo nafasi zote za uongozi zilikuwa zinashikiliwa na wanaume hivyo ikaonekana ni vema kikaanzishwa kitengo hiki cha wanawake waalimu kwa ajili ya kuwaandaa kushika nafasi za uongozi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CWT jiji la Arusha, Grace Msaki alisema kitengo cha wanawake kinaimarisha na kuwandaa wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi huku akitolea mfano wake yeye mwenyewe aliweza kufikia kugombea na kushinda nafasi hiyo kutokana na kitengo hicho ambapo walimuibua na kumshawishi agombee.
Alisema kuwa kuanzia aibuliwe mwaka 2003 kilipoanzishwa kitengo hicho amekuwa akigombea nafasi mbalimbali za uwakilishi ikiwemo hiyo ya uenyekiti wa CWT jiji la Arusha hivyo kuwa mwanamke pekee anayeongoza wilaya kwenye mkoa huu.
"Viongozi wa wilaya zote za Arusha ni wanaume isipokuwa mimi mwenyewe hivyo ile dhana iliyotumika kuanzishwa kwa kitengo hiki mimi ni mfano. Kusema ukweli bila kushikwa mkono mwanamke huwezi kusimama manake changamoto ni nyingi sana," alisema Msaki na kuongeza
"Niwatie moyo msikate tamaa kwa kuona nafasi uliyo nayo ni ndogo, hiyo ni kubwa sana.... katika mkutano wauongozi wa mkoa mimi nilishinda kuwawakilisha wenyeviti wenzangu kwenye mkutano mkuu wa Taifa,".
Msaki alisema kuwa mkutano huo wa Taifa wajumbe ni 77 ila wanawake ni 12 tu ambapo wenyeviti wa wilaya ni 10 na wenyeviti wa mikoa ni wawili tu kutoka Lindi na Dar es Salaam.
Alisema kuwa wamewaita kwa ajili ya kuwajenga na kuwaimarisha ili kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Aliwahimiza wawakilishi hao kuwahamasisha kuchangia mfuko wa ustawi wa jiji la Arusha ambao kila mwalimu anachangia shilingi 1,000 ambapo ikitokea changamoto kama mwalimu amefariki au anaumwa mfuko huo hutumika kusaidia kumaliza changamoto ndogondogo.
Msaki alisema kuwa CWT hushirikiana na afisa elimu jiji na kata kwenye kuusimamia na endapo itatokea mwalimu amepata changamoto hukutana kujadiliana kuona frdha zinazochangwa zitumike kusaidia kitu gani kama mwalimu ni mgonjwa au alifariki husaidia familia ya marehemu huku akisisitiza fedha hizo hazitumiki kwenye msiba.
"Tujitahidi wewe kama mwakilishi wa wanawake kwenye shule ushirikiane na mwakilishi wa CWT na mwalimu mkuu kuhamasisha upatikanaji wa mchango shilingi 1,000 inapotokea mwenzetu amepata shida ili kuhakikisha zinapatikana," alisema Msaki.
Aliwasisitiza umuhimu walimu hao kuwa na upendo na umoja miongoni mwao ikiwa ni sanjari na kuwasikiliza, kuwashauri kwa busara na kuwasaidia kwa upendo waalimu wa kike w pindi wanapopitia changamoto mbalimbali za kimaisha.
Katibu wa CWT wilayani Arusha, Abraham Kamwela aliwafafanulia wawakilishi hao juu ya kanuni za CWT, sera za walimu wa wawanawake na sheria zinazowahusu huku akiwahimiza kujituma zaidi wanapokuwa kwenye sehemu zao za kazi ili wanapopata changamoto ya kushindwa kufika kwa wakati isichukuliwe kuwa ni kawaida yao.
Alisema kuna masuala ya kifamilia na kibailojia yanayomfanya mwanamke kwenye baadhi ya siku kushindwa kufika kazini kwa wakati au kufanya kazi ipasavyo jambo alilowataka kuhakikisha pindi wanapomaliza changamoto hizo kuendelea kuchapa kazi zaidi ili isoonekane ni kawaida yao kushindwa kutimiza wajibu.
WATAKIWA KUTUMIA BUSARA ZAIDI KUONGOZA
Katibu wa CWT mkoa, Felix Mnyanyi aliwataka walimu hao mbali ya kuzingatia sheria lakini watumie busara na hekima wanapowaongoza wenzao.
Alitolea mfano mara mwalimu anapotoka kwenye likizo ya uzazi ni vema wakakaa nao kujadili kuona ni muda gani anaoona unafaa kwa ajili ya kwenda kunyonyesha iwe katikati ya muda wa kazi au muda wa mwisho wa kazi.
Mnyanyi alisema kwenye uongozi usiri ni jambo la muhimu sana pale inapotokea ameelezwa changamoto inayomkabili mwalimu asiitangaze bali aifanye iwe siri.
Aliwahimiza waalimu ambao ni waathirika wa Virus vya UKIMWI wasijifiche kwani wana haki zao ikiwemo kupunguziwa idadi ya vipindi wanavyofundisha kwa siku.
"Anapewa fedha za nyongeza ili kuboresha lishe yake ambayo si chini ya laki moja kila mwezi nje ya mshahara hii ni haki ya mtumishi za zinakuwa chini ya idara ya ustawi wa jamii," alisema Mnyanyi.






0 Comments:
Post a Comment