SERIKALI imeshauriwa kuvisimamia kwa karibu zaidi Vyama Vya Ushirika wa Akiba na Mikopo,(SACCOS) kwani zina fedha nyingi ambazo zina mchango mkubwa sana kwenye maendeleo ya uchumi wa jamii hivyo ni vema zikasaidiwa ziendelee kuwa imara.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa TANESCO SACCOS, Thomas Samo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Ushirika duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Arusha.
Alisema kuwa SACCOS ni taasisi kubwa sana za kifedha japo kuna baadhi zinajifanyia mambo kiholela jambo aliloshauri serikali ihakikishe inazisimamia kwa karibu ili zisianguke.
"Serikali ivisimamie vyama vya ushirika ili vijiendeshe kwa kuzingati mifumo na kwa utaratibu na kufuata sheria na kanuni zilizopo. Hizi ni taasisi kubwa sana za fedha japo kwa sasa nyingi zinajifanyia mambo wanavyotaka wenyewe," alisema Samo.
Alisema Tanesco SACCOS ni kubwa ambapo inamiliki benki yao ambayo wanaendesha shughuli zao kwa kushirikiana na benki ya Posta, (TPB).
"Sisi ni SACCOS pekee tunaotumia kadi za benki kuendesha shughuli zetu. Ukihitaji fedha unaenda kwenye mashine unatoa," alisema Samo.
NGOME SACCOS HUWANDALIA MAZINGIRA MAZURI WASTAAFU
Kwa upande wao Ngome SACCOS LIMITED ambayo wanachama wake ni wanajeshi, watumishi wa umma na wastaafu waliokuwa wakifanya kazi Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wamejiimarisha kiuchumi ambapo kwa mwezi mmoja huweza kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.8.
Makamu Mwenyekiti, Brigedia Jenerali, Omary Matteka alisema kuwa mikopo hiyo hutokelewa kwa wanachama wao kwa ajili ya shughuli za maendeleo na dharura.
Alisema mwanachama anaweza kupatiwa mpaka shilingi milioni mbili kama mkopo wa dharura ambazo atatakiwa kurejesha kidogokidogo kila siku.
Brigedia Jenerali, Matteka alisema kuwa mkopo wa maendeleo hutolewa kulingana na kiasi cha akiba za mwanachama aliyojiwekea kwenye ushirika ambapo hukopeshwa hata mara tatu ya kiasi cha akiba hiyo.
"Tuna programu ya kuwaandaa wastaafu ambayo huanza miezi sita kabla ya mwanachama hajastaafu . Mwanachama hupatiwa mkopo wa kufanya maandalizi ili atakapostaafu asijekuta mambo ndivyo sivyo," alisema Brigedia Jenerali, Matteka.
Ngome SACCOS ina wanachama zaidi ya elfu 13 walio kwenye kambi zote za jeshi nchini na ilisajiliwa mwaka 2007 wakati huo wakiendeshea shughuli zao kutoka Upanga ambapo kwa sasa wanaendesha shughuli zao kwenye ofisi zao zilizopo Mwenge Mlalakua.
0 Comments:
Post a Comment