CHAMA Cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa bandari nchini, (Bandari SACCOS limited) kimetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 12 kwa wanaushirika wake kwa mwaka huu wa fedha.
Mwenyekiti wa SACCOS hiyo, Stella Mutayabarwa aliyasema hayo juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya ushirika duniani yaliyofanyika jijini hapa ambapo mgeni rasmi alikuwa naibu katibu mkuu wizara ya kilimo chakula na ushirika, Profesa, Siza Tumbo.
Mutayabarwa alisema kuwa mikopo hiyo imetolewa kwa kipindi cha kati ya Januari na Septemba mwaka huu kwa wanachama wao walio kwenye mikoa nane tofauti hapa nchini.
Bandari SACCOS ilianzishwa miaka 52 iliyopita ina jumla ya wanachama elfu 13 ambapo makao makuu yake yako Dar es Salaam na ina matawi kwenye mikoa ya Tanga, Mtwara, Mafia, Mwanza, Kagera, Kigoma na Kyela.
Mutayabarwa alisema kuwa SACCOS hiyo imekuwa ni msaada mkubwa kwa wafanyakazi wa TPA kwa kuwapa wafanyakazi wao mikopo yenye masharti nafuu iliyowawezesha kujenga nyumba, kusomesha watoto wao na wao wenyewe kujiendeleza kielimu.
"Wengine wamenunua magari na kufanya mambo yao mengine waliyojipangia. Pia SACCOS imewapatia wanachama viwanja vilivyopimwa ukizingatia wengi walikuwa wanaishi kwenye maeneo yasiyo rasmi," anasema mwenyekiti Mutayabarwa na kuongeza.
"Bandari SACCOS iliamua kununua viwanja na kuwashirikisha wizara ya ardhi wakavipima na kuvirasimisha kisha wakavitengenezea mitaa na kuwapa namba za hati ya umiliki wa ardhi hiyo,".
Mutayabarwa alisema kuwa kuna wanachama wengine walipatiwa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ambapo SACCOS hiyo husimamia ujenzi wa nyumba mpaka hatua ya kuezeka paa ndipo mkopaji huachiwa kuendelea kusimamia hatua ya umaliziaji.
Alisema kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya ushirika kwa wafanyazi wa bandari ili wengi waweze kujiunga huku ikiendelea kuwanoa wanachama wao kuendelea kuufahamu vema ushirika huo kwa kuelewa haki na wajibu wao kwa maendeleo na ustawi wa ushirika huo.
"Wakati mwingine kwa kutoelewa unakuta wanachama kwa wanachama wanakosana au wanachama na watendaji wanakosana, au wanachama na viongozi wanakosana tulipoliona hilo tukaanza kutoa mafunzo kwa wanachama wote," alisema Mutayabarwa.
Alisema wanajivunia mafanikio waliyoyapata kwani wananchama wamejua matumizi sahihi ya mkopo na warejeshe kwa wakati.
Mutayabarwa alisema kuwa wamejipanga kuongeza wigo wa wanachama ambapo kwa sasa sifa za wanachama wao ni kuwa mfanyakazi wa bandari au mstaafu wa bandari lakini wanaangalia uwezekano kuruhusu wenza na watoto wa wanachama wao kujiunga na ushirika huo.



0 Comments:
Post a Comment