BARAZA la Wafugaji Ngorongoro limepinga mpango wa kuwaondoa wafugaji ndani eneo la hifadhi ya Mamlaka ya bonde la Ngorongoro,(NCA) huku wakiitaka serikali kutoharakisha suala hilo linalogusa maisha ya wananchi walio wengi.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Edward Maura ameyasema hayo leo jijini Arusha akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wakiwemo madiwani 16.
Amesema kuwa baraza hilo kwa niaba ya wenyeji wa eneo hilo wanapenda kuijulisha serikali kuwa wapo tayari kukaa meza moja na kuzungumza namna bora ya kutatua changamoto zinazoikabili katika uendeshaji wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro na si kuwahamisha watu kutoka katika maeneo yao.
Alisema kuwa kuna mijadala inayoendelea juu ya ugawaji wa eneo hilo aliyodai inaegemea upande mmoja jambo linalopelekea upotoshwaji wa uhalisia wa jambo hilo ambapo aliyataja magazeti mawili yanayodaiwa kunukuu taarifa hizo mwishoni mwa mwezi septemba.
Maura alisema kuwa chakula kinachotolewa na NCAA kwa wananchi wanaioshi ndani ya hifadhi hiyo ni kilogramu 15 za mahindi kwa kaya ambazo hazitolewi bure bali huuziwa kwa bei nafuu kila baada ya miezi mitatu.
Alisema kuwa ugawaji wa kanda pendekezwa alivyonukuliwa kamishina mkuu wa uhifadhi wa NCA, Edward Manongi hayatokani na maoni ya wenyeji wanaoishi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambaye alieleza kuwa serikali italigawa eneo hilo katika kanda nne jambo alilodai kuwa si sahihi.
WATOA SABABU ZA KUPINGA MAPENDEKEZO YA TUME YA KIGWANGALA
Baraza hilo la wafugaji linapinga mapendekezo ya tume ya ardhi mseto inayopendekeza vijiji nane vya kata za Endulni, Ngorongoro, Misigiyo na Alaitole zenye wakazi wapatao 24,199 na mifugo 194,039 inayojumuisha ng'ombe, kondoo na mbuzi waamishiwe zoni A kwa kile alichobainisha kuwa eneo hilo ni dogo wakichanganya na wakaazi ambao wako huko tayari.
"Itapelekea zoni pendekezwa iwe na jumla ya wakazi zaiai ya elfu 14 ambao ni sawa na asilimia 45 ya wenyeji wote wa NCA, ng'ombe 140,926 sawa na asilimia 59 ya ng'ombe wote wa NCA
Maura amesema kuwa maeneo yaliyopendekezwa hayatoshelezi kwa makazi na mifugo hivyo itaongeza migogoro isiyo ya lazima ndani ya hifadhi hiyo kwa kile alichodai kuwa kutakuwa na ushindani wa rasilimali maji, malisho, madini, lishe pamoja na kupelekea mlipuko wa magonjwa ya mara kwa mara kwa mifugo na binadamu.
Alipinga hoja ongezeko la watu na mifugo inayotumiwa kuwaondoa kwenye bonde hiyo akionyesha haina msingi wowote kwani ongezeko hilo liko maeneo yote ya nchi na akashauri njia ya kulitatua.
Ametaja njia hizo kuwa ni pamoja na kuweka miundombinu ya huduma za mifugo ikiwemo masoko ya kuuzia mifugo, kuandaa ranchi kwa ajili ya kunenepesha mifugo ambapi oia itatumika kama shamba darasa kwa wafugaji na kuanzisha kiwanda cha kusindika na kuchakata mazao yatikanayo na mifugo.
Amesema kuwa katika serikali iliunda tume tatu katika kutatua changamotoza uendeshaji wa eneo la hifadhi hiyo ikiwemo Tume ya Mpango wa jumla ya usimamizi wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro, Tume ya Marekebisho ya sheria ya hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya mapitio ardhi mseto.
"Kuundwa kwa tume hizi kwa wakati mmoja iliwachanganya wenyeji wa eneo la Ngorongoro kwa kuwa kila moja iliwasilisha mapendekezo tofauti juu ya namna ya uendeshaji wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kupelekea wananchi kushindwa kujua ni mapendekezo ya tume ipi yatuatwe," amesema Maura.
Hata hivyo mwenyekiti huyo wa baraza la wafugaji alidai kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kigwangala alizisimamisha kwa muda tume mbili ila ya Mpango wa jumla wa usimamizi wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya marekebisho ya sheria ya hifadhi hiyo na kuunda Tume ya mapitio ya ardhi mseto kwa ajili ya kuleta mapendekezo juu ya uendeshaji wa eneo ardhi mseto.
Septemba 22, 2019 Waziri wa Maliasili na Utalii, Kigwangala aliitisha kikao cha pamoja kikiwashirikisha watendaji wa wizara, NCAA, wawakilishi wa wananchi, halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro na baraza la wafugaji na kujadili mapendekezo ya mapitio ya mfumo wa matumizi jumuishi ya Ardhi.
Maura alisema kuwa wawakilishi wa wananchi walimweleza Waziri kuwa mapendekezo yaliyo kwenye rasimu hayakuhakisi maoni yaliyotolewa na wenyeji wa eneo hilo hivyo waziri akatoa siku 21 kwa tume hiyo kukusanya upya taarifa kutoka kwa wenyeji.
WAPINGA MUDA ULIOTOLEWA KWA TUME YA PILI
Hata hivyo alipinga muda uliotolewa kukusanya taarifa hizo kwa kile alichodai kuwa muda ni mfupi hivyo wanahofia inaweza kupelekea kukosekana kwa majibu sahihi ya kuondoa changamoto ya uendeshaji wa eneo la ardhi mseto.
"Tarafa ya Ngorongoro ina jumla ya tarafa 11, vijiji 25 ambapo kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na tume ya mapitio ya ardhi mseto itaenda kukusanya maoni ya wenyeji kwa muda wa siku sita tu ambao ni muda mfupi sana katika kukusanya maoni kwa wenyeji wa eneo," amesema Maura na kuongeza.
"Tunapenda ifahamike kuwa wenyeji wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro walipoamishwa kutoka Moru (Serengeti) majadiliano yalichukua zaidi ya miaka 18 kipindi hicho watu walikuwa wachache kuliko sasa.".
"Majadiliano hayo yalichukua muda mrefu kutoka na ukweli kuwa inagusa maisha ya watu na hivyo tunashauri majadiliano ya kina juu ya jambo hili la kuwahamisha wenyeji,".
KUONDOA BINADAMU KUTAATHIRI UTALII
"Kwa kuwaondoa wenyeji itaondoa sifa ya kipekee ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuitwa eneo la ardhi mseto ambayo imepelekea eneo hili kupata sifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa," amesema Maura .
Amesema uwepo wa wanadamu na wanyama kwenye bonde hilo kulisababisha kwa kwa nyakati tofauti lilitambuliwe kimataifa alitolea mfano kuwa mwaka 1979 Shirika UNESCO ililitangaza eneo hilo kuwa urithi wa dunia, mwaka 2013 likatangazwa kuwa eneo la maajabu saba ya dunia na lilipigiwa kura kuwa moja ya maajabu saba ya asili barani Afrika.
Mwenyekiti huyo amrsema mwaka 2015 bonde hilo la Ngorongoro lilitambuliwa kama eneo la lenye urithi mchanganyiko wa dunia na mwaka 2018 likatambuliwa kama eneo la dunia lenye mtandao wa miamba ya asili.
"Siyo kweli kuwa kuwaondoa watu ndani ya eneo la hifadhi itatatua mgogoro wa ardhi ya mseto isipokuwa itasababisha eneo kuondolewa kwenye sifa yake ya kipekee iliyopewa mwaka 1981 ya kuwa eneo la binadamu na uhifadhi wa baianuai," amesema Maura na kuongeza.
Kupendekeza kuondoa wenyeji ndani ya eneo inaweza kupelekea serikali kupoteza mapato mengi kwa kuwa wenyeji wamekuwa sehemu ya kivutio cha utalii ikiwa ni pamoja na kuvunja sheria ya uanzishwaji wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro iliyotamka wazi uwepo wa jamii ya kimaasai,",
WAPINGA UWINDAJI WA KITALII
Alipinga kuanzishwa kwa kushughuli za uwindaji wa kitalii kwenye bonde hilo kwa kile alichoeleza kuwa mbali ya kuwa ni kinyume cha sheria lakini itaweza kufungua mianya kwa watu wasioitakia mema nchi kutaka kumaliza wanyamapori ambao wameshiriki kuwahifadhi tokea kuanzishwa kwa hifadhi hiyo.
"Kupendekeza kuchukua eneo la kilometa 1,500 za pori tengefu la Loliondo ni kuendelea kuongeza mgogoro baina ya wawekezaji na wananchi wa tarafa za Ngorongoro na Loliondo na hata kuna uwezekano wa kuikosesha mapato yanayotokana na uwekezaji halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro," alisema Maura na kuongeza,
"Kanda zinazopendekezwa, mfano kanda ya maendeleo hazifai kabisa kwa kilimo na ufugaji kwa kuwa maeneo yote ya nyanda za chini yamevamiwa na mimea vamizi, maeneo kame na yana ugonjwa nyumbu 'malignant catarrhal fever' ambapo mpaka sasa hakuna kinga wala tiba ya ugonjwa huo . Hii itapelekea wananchi kupoteza mifugo yao na kuendelea kubaki maskini,".
Juhudi za kumpata Kamishina Mkuu wa NCAA, Manongi kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda kwani alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani iliita muda wote bila kupokelewa.
.jpeg)
0 Comments:
Post a Comment