HII HAPA SABABU YA DK KIMEI KUMWAGA MACHOZI

MKURUGENZI Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amemwaga machozi wakati akiwashukuru watendaji wa benki hiyo kwa ushirikiano wanaompa unaomfanya apate sifa za kuiendesha benki hiyo kwa mafanikio.

Aidha wanahisa wa benki hiyo wameitaka bodi ya wakurugenzi ya benki hiyo kumuongezea mkataba wa kazi Dk Kimei ili kutoa muda zaidi wa kumpata mtu sahihi wa kushika nafasi hiyo huku wakiwaambia kama wataamua kujiuzulu kupinga uamuzi huo wanahisa wako tayari kuchagua bodi mpya.

Hayo yalitokea Mei 19,mwaka huu wakati wa mkutano Mkuu wa 23 wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika jijini hapa wakati Dk Kimei akimalizia kutoa taarifa yake ya utendaji wa benki kwa mwaka 2017 huku akiwaeleza kuwa ataendelea kuwepo kwani anastaafu Mei, mwakani kisha wanahisa kuanza kuijadili.

Dk Kimei alisema kuwa kuna wakurugenzi 13 wa benki hiyo ambao amefanya nao kazi ka ukaribu kwa muda mrefu pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo ndiyo siri ya benki hiyo kufanya vizuri ambapo alionekana sauti yake kuanza kubadilika kisha kufuta machozi.

Wakichangia taarifa yake ya utendaji wanahisa hao walisema kuwa kutokana na kazi nzuri aliyofanya mkurugenzi mtendaji huyo hakuna ulazima wa kumuondoa kwa haraka hasa kipindi hiki ambapo kuna ushindani mkubwa wa mabenki hapa nchini.

Wanahisa hao walisema kuwa Dk Kimei aongezewe muda wa kufanya kazi ili aandae mtu sahihi wa kushika nafasi hiyo kwa kile walichodai kuwa mkurugenzi mtendaji huyo ndiyo nguzo ya benki hiyo.

"Kimei ndiyo nguzo kubwa ya CRDB kama Rais (john Magufuli) amemsifu wakiwa kule Chato wakati wakifungua tawi la CRDB na kuahidi kumpa kazi endapo tutamuacha. Kama Mkuu nchi amemsifu nyie mnasemaje ondoka? Mtu akitaka kuvunja nyumba anaondoa nguzo kubwa," alisema mwanahisa Olle Sirikwa.

Alionya kuwa kuna vita kubwa ya mabenki hapa nchini kwa sasa hivyo akawata wanahisa wawe makini kwa kile alichodai kuwa kuondoka kwa Dk Kimei kunaweza kusababisha athari kubwa kwa benki.

Wanahisa hao walienda mbali wakidai kuwa mkutano mkuu ndiyo wenye maamuzi ya mwisho juu ya masuala yote yanayoihusu benki hiyo hivyo kama bodi ya wakurugenzi haikubaliani na hoja hiyo na kuamua kujiuzulu wafanye hivyo na mkutano mkuu utachagua wajumb wapya wa kuunda bodi hiyo.

"Tukae chonjo akiondoka huyu mtu baada ya miaka miwili tunaweza kuona vumbi sisi wanahisa tunasema 'Kimei shall remain until further notice' wakurugenzi msikasirike kwa sababu mkikasirika hatutawachagua," alisema mwanahisa Ole Sirikwa na kuongeza.

"Na kama mkikataa jiuzuluni tutachagua wengine, mwacheni Kimei akae mpaka amalize vizuri akabidhi na mtu wa kushika nafasi yake,".

Aidha mwanahisa mwingine alidai kuwa Dk Kimei tu ndiye mwenye uwezo wa kwenda ikulu kufuatilia mikopo iliyotolewa kwa udhamini wa  Serikali ambayo ni mikubwa na mpaka sasa haijarejeshwa.

Aidha walidai kuwa endapo italazimu Dk Kimei kustaafu kama alivyokwisha tangaza basi mrithi wake atoke hapahapa nchini badala ya kuleta watu nje ya nchi ambao watalazimika kukaa na kuanza kujifunza utamaduni wetu.

"Lazima mrithi apatikane ndani ya benki yetu, haiwezekani hawa vijana wetu waliofundishwa kazi washindwe kuchukua nafasi hiyo lakini kwa sasa Dk Kimei aongezewe miaka miwili au mitatu ili amalizie hiki kipindi kigumu cha uchumi ndipo aondoke," alisisitiza mwanahisa mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.

Akijibu hoja hizo Dk Kimei alisema kuwa, "Mimi siliagi ukiona nimelia ujue nilikuwa 'too emotional' ukipata furaha sana unalia na ukipata uchungu sana unalia, naomba suala hili ( la kustaafu) lisisumbue watu umefika umri fulani unastaafu lakini naamini mambo yanasikilizwa,".

BODI YASHIKILIA MSIMAMO

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi a benki hiyo, Ally Laay aliwaeleza wanahisa hao kuwa waliwachagua ili waendeshe benki hiyo kwa mujibu wa sheria ambapo walikuwa wakimpa Dk Kimei mkataba wa miaka minne ambapo miaka ya nyuma alitaka kustaafu akamuongezea miaka miwili.

"Desemba 28, mwaka jana Dk Kimei alitokea kwenye media na kutangaza anajiuzulu mei 2019 na sisi bodi tulitoa tangaza desemba 29, 2017 tukatangaza mchakati wa kumpata mkurugenzi mtendaji," alisema Mwenyekiti huyo wa bodi.

Alisema kuwa walifuata taratibu zote zinazotakiwa ikiwemo kutoa taarifa kwa soko la hisa Dar es Salaam na tumeajiri wataalam wa kusimamia zoezi la kupata mridhi wa Dk Kimei.

Laay alisema kuwa japo Dk Kimei atastaafu lakini wataendelea kumtumia kwa namna ambayo wataona inafaa huku akiwahakikishia wajumbe wa hisa kuwa wanaamini watala waliowaajiri watawezesha kupatikana mkurugenzi mwenye sifa kama za Dk Kimei au kumzidi.

0 Comments:

Post a Comment