ZAIDI ya wananchi 400 wa Kitongoji cha Momela kata ya Ngarenanyuki wilayani Arumeru wamemuomba Rais John Magufuli aingilie kati kunusuru ardhi yao zaidi ya ekari 600 wanayodai kupokonywa na Hifadhi ya Taifa ya Arusha, (ANAPA) kwa msaada wa ofisi ya mkuu wa wilaya ya Arumeru.
Aidha wameitaka serikali kuwafafanulia wako kwenye eneo gani la nchi baada ya uongozi wa kijiji cha Olkung'wado kusema kitongoji hicho hakipo kwenye kijiji hicho wakati kitongoji hicho kilichokuwepo kabla ya uhuru.
Wanadai hata Rais wa Kwanza, Julius Nyerere mwaka 1975 aliwaongezea sehemu ya ardhi wakati wa operesheni vijiji vya ujamaa kati ya mwaka 1975 na 1977 ila wameshangaa kwa sasa kitingoji hicho kimeindolewa kwenye ilani ya serikali (GN).
Pia wamelalamikia hatua Katibu Tawala wa wilaya ya Arumeru, Timetheo Mzava, kwa kufika kwenye eneo hilo januari 29, mwaka huu kusimamia zoezi la uwekaji geti la ANAPA kwenye maeneo yao akiwa ameambatana na askari polisi wenye silaha na mabomu ya machozi huku akiwatolea maneno ya kuudhi.
Wananchi hao wakiongea kwa uchungu huku wengine wakitokwa na machozi kwenye mkutano maalum wa kitongoji ulioitwa na mwenyekiti wao, Senyaeli Nko Februari 3, mwaka huu kwa lengo la kupokea ujumbe kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya waliopelekewa na Katibu Mtendaji wa kata Ngarenanyuki, Ndikilo Mbise.
Mbise alitolea ufafanuzi juu taratibu zilizofuatwa mpaka ardhi ya kitongoji hicho kuchukuliwa na ANAPA bila wananchi au mwakilishi kutoka kitongoji hicho kushiriki kwenye kikao kilichofanya maaamuzi hayo kilichoitishwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Alexander Mnyeti.
Wananchi walidai kuwa eneo lao limefanana na maeneo ya vita kwani askari wa hifadhi ya ANAPA wamekuwa wakizunguka kwenye makazi yao huku wakiwa na silaha za moto.
Wanadai kwa sasa hawajui watapata wapi msaada baada ya viongozi kuanzia kijiji, kata na wilaya kuungana na ANAPA katika kuwadhulumu ardhi hiyo kwa kile walichodai kuwa hata kikao kilichokaa na kuamua ardhi hiyo ichukuliwe na ANAPA ambacho waliambiwa kilifanyika mwezi mei mwaka jana hakuna kiongozi wala mwananchi wa kitongoji hicho aliyeshiriki.
Kwa upande wake DAS wa Arumeru, Mzava, alipotafutwa kwa njia ya simu alisema yuko kwenye kikao akaahidi akimaliza atapiga simu ambapo alipopigiwa baadaye simu yake iliita tu bila kupokelewa.
Naye Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA), Paschal Shelutete, hakuwepo ofisini kwake ambapo alipopigiwa aliahidi kutoa ufafanuzi saa nane mchana ambapo alipotafutwa tena kupitia simu yake ya kiganjani alituma ujumbe kuwa yupo kikaoni.
0 Comments:
Post a Comment