Korea Kaskazini ilichukua hatua isiyo ya kawaida ya kutangaza matokeo ya jaribio lake la nyuklia la jana Jumapili kwa kuonyesha picha za kile ilichodai kuwa lilikuwa bomu la haidrojeni.
Hilo lilikuwa jaribio la sita la nyuklia kufanywa na nchi hiyo kwenye eneo la Punggye-ri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Baada ya jaribio hilo Korea Kaskazini ilitangaza kupitia shirika la habari linalomilikiwa na serikali yake kuwa ilifanikiwa kufanya jaribio la bomu la haidrojeni ambalo linaweza kuwa kichwa cha kombora lenye uwezo wa kuvuka mabara.
Masaa matatu kabla ya jaribio hilo, kituo cha televisheni cha Korean Central au KRT kiliripoti kuwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Kim Jong Un alilikagua bomu hilo lililokuwa kwenye taasisi ya utafiti wa silaha za nyuklia. Televisheni hiyo ya KRT pia ilionyesha picha za kifaa cha chuma kilichokuwa na muundo unaofanana na chungu.
Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya nchi hiyo nalo pia lilionyesha ripoti pamoja na picha muda mfupi kabla Kim na wajumbe wote wa nne wa Kamati Kuu ya chama kutoa amri ya kufanyika kwa jaribio hilo.
Ikumbukwe kuwa sio kawaida kwa Korea Kaskazini kutoa picha za kile inachodai kuwa ni jaribio la nyuklia pamoja na zile za Kim na wajumbe wa kamati kuu ya chama walipokuwa wanafanya maamuzi kabla ya kufanyika kwa jaribio hilo la nyuklia.
Wachambuzi wanasema Korea Kaskazini inajaribu kuuonyesha ulimwengu maendeleo inayofikia kwenye mchakato wa kuendeleza silaha ndogo lakini zenye nguvu za nyuklia wakati huo huo wakiendelea kumalizia utengenezaji wa kombora lenye uwezo wa kuvuka mabara lenye uwezo wa kupiga Marekani bara.
Wanasema utawala wa Korea Kaskazini pia unajaribu kuimarisha mamlaka ya Kim Jong-un wakati nchi hiyo ikielekea siku ya kumbukumbu ya kuanzishwa kwa taifa hilo tarehe 9 Septemba.

0 Comments:
Post a Comment