KUTOKA TOVUTI YA GAZETI LA HABARI LEO MUHIMU:
MEANDIKWA NA SIFA LUBAS CHANZO HAPA
UTAFITI wa awali uliofanywa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Jukwaa la Utu wa Mtoto wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, umebaini wilaya hiyo kuwa na tatizo kubwa la mimba za utotoni.
PICHA KUTOKA SANTOS CHUA BLOG YA MWAKA 2014 |
Hali hiyo imesababisha watoto wengi kusitisha masomo na kuingia katika ulezi.
Ofisa ufuatiliaji na tathimini wa Shirika hilo, Dorothea Ernest alisema utafiti huo ulifanywa katika kata nne za Kibakwe, Mpwapwa mjini, Berege na Pwaga.
“Utafiti umebaini watoto wengi walio chini ya miaka 16 wamejikuta wakiingia katika malezi na hivyo wengi wao kuathirika kisaikolojia hivyo kushindwa kuwa wazalishaji na kubaki kuwa tegemezi,” alisema.
Alisema utafiti huo umegundua kuwa kwenye kundi la watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 17; kati ya watoto 10, watoto watatu tayari walipata ujauzito na wako katika malezi ya watoto wenzao.
Alisisitiza kuwa hali hiyo inafifisha ndoto nyingi za wasichana hao na kujikuta katika lindi kubwa la umaskini.
Dorothea aliomba Serikali pamoja na jamii ya watu wa Mpwapwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali kupunguza tatizo hilo ambalo linatishia uendelevu wa utu wa mtoto na hivyo kumfanya mtoto wa kike kupoteza ndoto zake nyingi na kuingia katika malezi kabla ya muda.
Kwa upande upande wake Ofisa Mradi wa shirika hilo, Clara Wisiko alisema chanzo kikubwa cha mimba za utotoni katika kata hizo ni umbali wa huduma za jamii kama maji, upatikanaji wa kuni pamoja umbali kati ya shule na vilipo vitongoji na vijiji wanapoishi wazazi wa watoto hao.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni ukosefu wa elimu ya uzazi kwa watoto wa kike, umaskini katika familia ambao huchangia mtoto kudanganywa kirahisi na watu wazima na kufanya ngono ili aweze kupewa kitu kidogo kukidhi mahitaji yanayomkabili kwa wakati ule.
Hata hivyo alisema pamoja na kuwapo kwa miongozo, sera na sheria ya mtoto lakini bado kuna vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto kutokana na usimamizi hafifu wa miongozo hiyo.
Alisema pamoja na mimba za utotoni pia wilaya hiyo inakabiliwa na ndoa za utotoni na mila ya ukeketaji kwa watoto wa kike.
Alisema shirika hilo limelenga kushirikisha jamii na serikali katika kukabili changamoto hizo kwa kufanya utafiti shirikishi ambao hushirikisha jamii yenyewe kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.
Mmoja wa wazazi watoto, ambae amejikuta akiingia katika ulezi akiwa na miaka 13, Diana (sasa ana miaka 14) Masawe alisema alipata ujauzito akiwa na miaka 13 wakati akisoma darasa la tano.
Alisema alilazimika kuacha shule ili aweze kumlea mtoto wake.
0 Comments:
Post a Comment