MBOWE AWAPATIA MASHINE YAKUSAGA NAFAKA WANAWAKE WA SANYA STATION






MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Freeman Mbowe, juzi akipokewa na wanawake wa Jamii ya Kimasai wa kijiji cha Sanya Station, kata ya Kia ambapo aliwapa msaada wa mashine ya kusaga nafaka yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 3.6. (Picha na Grace Macha)





KIONGOZI wa kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, (CHADEMA), ametoa msaada wa mashine ya kusagia nafaka kwa wananchi wa kijiji cha Sanya Station kata ya Kia wilayani Hai yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 3.6.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa Taifa wa Chadema amesema kuwa akiwa  mbunge wa Hai hataridhia mpango wowote wa kumega ardhi ya wananchi hao bila kufuata sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia masuala ya ardhi.

Mbowe aliyasema hayo juzi wakati akiongea na wananchi wa eneo hilo ambao walimsomea risala yao wakimweleza kuwa miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni tishio la kuondolewa kwenye ardhi yao kampuni inayosimamia uendeshaji wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, (KADCO)  pamoja na ukosefu wa mashine ya kusaga nafaka.

Mbowe alitoa   fedha taslimu ili azikabidhi kwa uongozi wa kikundi cha kina mama cha Embwaan kwa ajili kununulia mashine hiyo inayoendeshwa kwa nishati ya umeme lakini kwa sababu za kiusalama wananchi hao walimuomba akainunue kisha awapelekee jambo ambalo alikubaliana nalo.

Aliwaambia wananchi hao kuwa mgogoro wa ardhi baina yao na KADCO wanauendekeza wenyewe kutokana na uamuzi wao wa kukichagua Chama Cha Mapinduzi, (CCM), kwenye chaguzi mbalimbali kutokana na ahadi hewa wanazowapa kuwa watamaliza tatizo hilo lakini uchaguzi ukiisha hawaonekani.

"Sanya Station mnashindwa kuwa majasiri kujitetea, mmekuja mpaka Dodoma nikawapokea tukafuatilia suala hili kuhakikisha hamuondolewi kwenye ardhi yenu ya asili kihuni. Lakini anakuja Kinana ( Abdulrahman, Katibu Mkuu wa CCM) anawadanganya amemaliza mgogoro mnaipigia kura CCM, haijaisha muda mnarudi tena kwa Mbowe tusaidie wanataka kututondoa...

"Mngenisikiliza mkaipiga chini CCM, wangewasikiliza na hili jambo tungekuwa tumeshalizaliza zamani sana, angalieni kata ambazo wameikataa CCM kama zile kule ukanda wa milimani, kuna huduma zote muhimu, kule hakuna shida ya maji, hakuna watu wanahamishwa bila kufuata utaratibu, kuna hospitali na barabara za lami," alisema Mbowe.

Aidha, aliwaahidi wananchi hao kuwapelekea "greda" lake  linalotumika kutengeneza barabara jimboni kwake bure, mara  msimu wa mvua ukimalizika ili likatengeneze barabara kwenye kata hiyo kwani kitaalam haishauriwi kuchonga barabara nyakati za mvua.

Makamu Mwenyekiti wa kikundi cha kinamama cha Ebwaani waliopewa msaada huo wa mashine alimshukuru Mbowe kwa msaada huo ambao watautumia kama mradi wa kuwaingizia mapato na kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira.

Alisema kuwa kwenye eneo hilo wanawake hawana kitu cha kuwaingizia mapato hali nayowalazimu kufanya biashara ya kukata miti kwenye msitu wa Mererani ambao huitumia kutengenezea mkaa ambayo huja kuiuza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema, wilayani Hai, James Mushi aliwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha siku za mwanzo kabisa pindi tarehe za uandikishwaji zitakapotangazwa kwa wilaya ya Hai.

Naye Katibu wa Bawaza la Wanawake Chadema, (BAWACHA), mkoani Kilimanjaro, Helga Mchovu alisema hakuna dhambi kubwa mwaka huu kama Mtanzania anayejitambua kuacha kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili aweze kutumia haki yake ya kuchagua viongozi baadaye  Oktoba 25, mwaka huu.

0 Comments:

Post a Comment