Zikiwa
zimebaki siku chache kabla ya Kamati ninayoongoza ya PAC kuwasilisha
Bungeni Taarifa Maalumu kuhusu ukaguzi maalumu wa akaunti ya Tegeta
Escrow, kumekuwa na kampeni za chini chini zinazoendeshwa kwenye korido
za Bunge na kwenye mitandao dhidi yangu binafsi na baadhi ya wabunge
waliosimama kidete dhidi ya wizi wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania
akaunti ya Escrow.
Baadhi ya tuhuma nimezipeleka kwenye vyombo vya dola ili zichunguzwe
kwani zina vielelezo vya mahala pa kuanzia (kama leseni ya udereva ya
mwanamke anajulikana kama Vivian Emmanuel Sirikwa na muhuri wa kampuni
ya uwakili inayomilikiwa na Bwana Joseph Mkandege). Baadhi ya tuhuma
nitazijibu moja baada ya moja.
Waziri mmoja ambaye ni mtuhumiwa wa wizi wa fedha za Tegeta Escrow
anazunguka kwa wabunge akisema tuhuma hizi kupikwa kama njia yake ya
kuhamisha mjadala kutoka uporaji wa Tshs 200 bilioni kwenda kwenye
masuala binafsi.
Tuhuma hizi zenye kichwa cha habari "Zitto na Filikunjombe wanatumiwa na
Kenya na Uingereza kuvuruga na kudhoofisha Uwekezaji nchini mwetu"
zinajibiwa hapa chini. Utaona ndugu Filikunjombe ametajwa kwa kichwa cha
habari ili kumtaja tu bila sababu yeyote ile.
Tuhuma #1 :
Zitto anaye rafiki yake Mkenya aitwae Rapahel Ongangi ambao kwa pamoja
wameanzisha Gombe Advisors Co. Ltd (registered on 24 November 2011,
Certificate No 87387) kwa ajili ya kufanya biashara na Makampuni ya Gesi
na Mafuta yanayofanya kazi nchini hapa.
Majibu:
Gombe Advisors ni kampuni binafsi isiyofanya faida yaani ‘Company
Limited by Guarantee’. Haina kazi na kampuni yoyote ya Gesi na Mafuta na
wala yenyewe haijuhusishi na biashara hiyo. Gombe advisors haijafanya
kazi yoyote ile na kampuni nyingine zaidi ya kusaidia wasanii wa kundi
la Kigoma All stars. Upotoshaji hapa unalenga kupindisha mjadala.
Tuhuma #2 :
Zitto amemsaidia Ongangi kupata uraia wa Tanzania na kwa sasa ni raia wa
pasipoti. Zitto na Ongangi walimtafutia CEO wa Shell aitwae Axel
Knospe nyumba na gari ya kukodi.
Majibu:
Raphael ni mtu binafsi ambaye anafanya shughuli zake hapa nchini,
amesoma hapa nchini na ameoa na ana mtoto. Tuhuma hizi hazina msingi
wowote ule maana ni uwongo. Wanaotoa tuhuma hizi waonyeshe hiyo pasipoti
ya Bwana Ongangi kuthibitisha madai yao.
Tuhuma #3 :
Mikataba ya STATOIL iliyokuwa inarushwa kwenye mitandao ya jamii na
kuchapishwa kwenye magazeti ya Kenya ya hapa nchini (The Citizen na
Mwananchi) mwandishi mkuu alikuwa huyo CEO wa Shell.
Majibu:
Mkataba uliovujishwa wa StatOil ulivujishwa na waandishi wa habari wa
Norway. Uchambuzi wa mkataba huo nimeufanya mwenyewe kwa kutumia
utaalamu wangu niliosomea wa kuchambua mifumo ya kodi kwenye sekta ya
mafuta na gesi. Kwa namna yoyote ile, huyo anayetajwa kuwa CEO wa
kampuni ya Shell hahusiki. Tuhuma hii wanaoitoa watoe ushahidi usio na
chembe ya mashaka.
Ikumbukwe kuwa mkataba wa StatOil utaipotezea Tanzania mapato ya dola za
Marekani bilioni 12 (takribani Tshs 20,400,000,000,000/=) katika
kipindi cha miaka 15 baada ya gesi kuanza kuchimbwa. Uamuzi wa Kamati ya
PAC kutaka mikataba yote ya Gesi kuwa wazi una lengo la kuchambua
kuona kama mikataba yote nchini haipotezi mapato kwa nchi. Uamuzi huo
umewakasirisha sana baadhi ya waliohusika kuingia mikataba Serikalini
maana wanajua kuna madudu kwenye mikataba na wanataka umma wa watanzania
usijue!
Tuhuma #4 :
Kampuni ya SHELL imechukizwa sana kucheleweshwa kwa kupata kibali cha
kutafuta gesi na mafuta kule Pemba. Vilevile SHELL haina uwekezaji
mkubwa Tanzania Bara kwani ilishindwa kwenye tenda zenye vitalu vyenye
gesi nyingi upande wa Bara.
Majibu:
Ukweli ni kuwa Kampuni ya Shell ina vitalu 4 huko Zanzibar na tayari ina
makubaliano na Serikali ya Zanzibar kuhusu utafutaji mafuta huko
katika vitalu namba 9,10,11 na 12. Shell inafanya kazi na kampuni ya
Petrobras ya Brazil kwenye kitalu namba 6 na namba 8. Taarifa hizi zipo
wazi kwenye tovuti ya TPDC. Tuhuma nyepesi namna hii dhidi ya kampuni
kubwa kama Shell zinaonyesha dharau na kiburi kinachotokana na uelewa
mdogo wa mambo wa watu wanaotuhumu.
Tuhuma 5:
Ongangi anapokea maelekezo kutoka Serikali ya Kenya kuhujumu uwekezaji nchini mwetu.
Majibu:
Nazifahamu mbinu nyingi zinazotumika kufanya propaganda, lakini mbinu
hii imeshindwa ikiwa mapema sana. Ni vema wanaotoa tuhuma hizi
wazithibitishe vinginevyo ni mwendelezo wa propaganda zisozingatia
diplomasia ndani yake dhidi ya jirani zetu wa Kenya. Hizi ni propaganda
hatari ambazo hata hao wanaotuhumiwa wakisikia watatudharau sana.
Tuhuma #6 (juu ya Uingereza):
Uingereza imekuwa inamfadhili Zitto kwa miaka mingi kwa mambo yake ya
kisiasa kwa hiyo sasa hivi Ubalozi wa Uingereza unamlipa Zitto na
Kafulila kuhakikisha kwamba Standard Chartered ya Uingereza inalipwa
deni lake lisilotambulika kisheria nchini mwetu.
Majibu:
Nimetangulia kusema hapo awali kuwa kuna propaganda ambazo haziangalii
hata diplomasia; nyingine ni hii. Pamoja na kukanusha uzushi huu, ni
vizuri wanaotoa tuhuma za namna hii kuthibitisha. Mimi binafsi sijawahi
kufadhiliwa kisiasa na Taifa lolote lile. Inaelekea kuna wanasiasa
wanaofadhiliwa na mataifa mengine ambao kwakuwa kwao ndiyo maisha
wanaamini na wengine tupo kama walivyo. Kwangu itikadi yangu ni
‘Uzalendo kwa nchi yangu’, ni jambo ambalo halina mbadala wake. Siku
zote nasema “Right or wrong, my country first". Kurudia kurusha tuhuma
kwa Ubalozi wa Uingereza nchini ni kudhihirisha kwa mara nyingine kiburi
cha kuwa na mamlaka (arrogance of power) walicho nacho wanaotuma
tuhuma hizi.
Aidha, wanatuhumu kuwa “Kafulila na Zitto wamehaidiwa 15% ya USD 150 million kama deni likilipwa”
Mtanzania anayeweza propaganda dhaifu kama hizi basi anatakiwa
ajitafakari. Hata hivyo ni vema wanaotoa tuhuma hizi wathibitishe bila
chembe ya mashaka.
Tuhuma #7 :
Mbunge Mkono nae ameshikwa hasira kupoteza kazi ya uwakili pale TANESCO.
Kafulila na Zitto wanalipwa na Mkono kuvuruga Serikali kwa hasira za
kukosa fedha za kitapeli za TANESCO.
Majibu:
Hizi ni tuhuma ambazo sasa tumezizoea kutolewa. Mambo mepesi hayawezi
kujibu mambo ya msingi kama tuhuma za wizi wa fedha zaidi ya Tshs
bilioni 200 kutoka Benki kuu ya Tanzania. Kukusanya kila propaganda ili
kuuhamisha umma ni kupungukiwa hekima na busara.
Aidha, wanaotuhumu wanadokeza kuwa “Naomba tuwe macho na Wabunge wetu
achananeni na madai ya Zitto ya wizi. Huyu mtu anafanya biashara na
Kampuni ya SHELL na inasemekana analipwa na Ubalozi wa Uingereza.
Serikali ya Kenya na tapeli mkubwa Mbunge Mkono nae anawalipa Zitto na
Kafulila”.
Watanzania, haya ni maneno ya hasira ya watu wanaokaribia kukamatwa kwa
kushiriki wizi wa fedha katika Benki kuu ya Tanzania. Kamwe tuhuma kama
hizi haziwezi kutukatisha tamaa katika kupambana ili ukweli ujulikane.
Sisi tutapigana kwa ajili ya Taifa, kwa ajili ya mtanzania na
tunachotaka ni umma uujue ukweli wa mambo.
Hasira hizi zinatokana na mambo mawili:
Moja ni uamuzi wa kamati ya PAC kuwasweka ndani baadhi ya watendaji wa
TPDC kwa kushindwa kutekeleza maamuzi ya Kamati yanayohusu uwazi wa
mikataba ya Gesi na Mafuta.
Pili, ni uamuzi wa PAC kuagiza ukaguzi maalumu wa mchakato mzima wa
kuanzishwa na kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow ambapo zaidi ya
shilingi bilioni 200 ziliporwa na zaidi ya shilingi bilioni 12 zinalipwa
na TANESCO kila mwezi kwenda kampuni ya PAP inayomilikiwa na Harbinder
Singh Seth (50%) na watu wasiojulikana kupitia kampuni ya Simba Trust
iliyosajiliwa na kufichwa nchini Australia (50%).
Ieleweke kuwa PAP inalipwa shilingi milioni 400 kila siku kutoka TANESCO
izalishe au isizalishe Umeme! Watanzania, PAP itaendelea kulipwa namna
hiyo kwa miaka 20 ijayo. Kwa namna ambayo Seth analindwa na baadhi ya
watendaji Serikalini na hasa ndani ya Wizara ya Nishati na Madini.
Aidha, kuna fununu kuwa kuna maofisa serikalini wanaomiliki hizo 50% za
kampuni ya PAP. Seth pia anamiliki kitalu cha gesi Mnazi bay Kaskazini
kupitia kampuni ya HydroTanz.
Hasira hizi walizo nazo wanaonituhumu na Kamati yangu zimewapelekea
kugushi nyaraka mbalimbali zinazonituhumu mimi na wenzangu ili
kutuogopesha na kutukatisha tamaa katika kutafuta ukweli juu ya suala la
uporaji wa fedha kutoka Benki kuu. Lengo lao ni kututoa kwenye mstari.
Mimi na wenzangu hatutatoka kwenye mstari, tutashirikiana na wabunge
wenzetu kuhakikisha ukweli unajulikana na wezi kuchukuliwa hatua kali.
Harbinder Singh Seth aliiangusha Serikali ya KANU nchini Kenya, sasa
anachotaka kukifanya kinaweza kuiangusha Serikali ya CCM wakiendelea
kumkumbatia. Watanzania sio mabwege!
Zitto Kabwe
Mwenyekiti PAC
Dodoma, 9 Novemba 2014
RAIS SAMIA AUMIZWA MAUAJI YA KIBIKI
-
-Simanzi yatanda mazishi yake
-Nchimbi: matukio ya kutia hofu na shaka, hayakubaliki
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano...
2 hours ago