Falsafa ya Chadema

Falsafa ya Chadema
  1. Falsafa ni fikra na mtazamo wa Chama ambayo ni kuamini katika “Nguvu na Mamlaka ya Umma” (The People’s Power) katika kumiliki, kuendesha, kubuni, na kuendeleza maamuzi, mawazo, rasilimali, uchumi na siasa ya nchi yao.
  2. Aidha falsafa ya “Nguvu na Mamlaka ya Umma” ndiyo msingi na chimbuko la kuundwa dola ya nchi, na kuwa, Umma ndiyo wenye madaraka ya mwanzo na ya mwisho katika kuamua hatima ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni.
  3. Ujenzi na udumishaji wa Demokrasia na Maendeleo nchini vitatokana na Nguvu na Mamlaka ya Umma wa Watanzania. Nguvu na Mamlaka ya Umma itabainishwa, kuainishwa na kulindwa katika Katiba ya nchi na Umma ndiyo utakuwa chimbuko la Katiba hiyo.
  4. Historia inaonyesha kuwa “UMMA” wa Watanzania haujawahi kuwa na sauti, mamlaka na madaraka juu ya maamuzi ya hatima ya maisha ya watu. Uhuru, nguvu, mamlaka na madaraka wakati wote, tokea enzi za ukoloni mpaka leo, vimekuwa vikihodhiwa na kumilikiwa na watu wachache ambao wana mamlaka ya kuongoza SERIKALI na kuwakandamiza wananchi.
  5. CHADEMA tunaamini kuwa mifumo na miundo ya utawala wa nchi yetu havijawapo kwa ajili ya kuutumikia umma, bali umma ndiyo huzitumikia serikali hizo ambazo ni mali ya watu wachache wanaopoka “Nguvu ya Umma”. Sambamba na hilo, umma wa Watanzania umekuwa hauna mamlaka ya mwisho ya kuhoji maamuzi ya serikali yanayowaathiri watu, na hivyo kujikuta hauna mamlaka juu ya rasilimali, sheria, utawala, na uendeshaji wa nchi. Aidha, Katiba ya Nchi imekuwa miliki ya Serikali kwa kutumia Bunge ambalo linatawaliwa na mawazo kongwe ya ukiritimba wa enzi za mfumo wa Chama kimoja cha siasa nchini.
  6. CHADEMA tunaamini na kutambua kuwa “kuchaguliwa” kuunda utawala wa kuongoza nchi hakumaanishi wachaguliwa kujitwalia mamalaka ya UMMA na kisha kuyatumia mamlaka hayo kuwakandamiza “waliowachagua” kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma.
  7. Hivyo basi, falsafa ya “Nguvu na Mamlaka ya Umma” ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na za haki.
  8. Falsafa ya “Nguvu na Mamlaka ya Umma” inalenga kuwaamsha, kuwahamasisha, kuwaelimisha, kuwashawishi na kuwaandaa Watanzania wachukue hatua ya kuimiliki, kuitawala, kuilinda na kuifaidi nchi yao tofauti na kipindi cha miaka mingi chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa na miaka kumi na nne ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi.