TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI.
Mkoa
wa Arusha hususani Manispaa ya Jiji la Arusha ilijulikana kama “Geneva of
Africa”. Hii ilitokana na ukweli kwamba ndani ya Manispaa ya Arusha watu mbali
mbali wenyeji kwa wageni walikuwa na uhakika wa usalama wa maisha yao.
Hali
hii imebadilika miaka ya karibuni na kuwa tofauti na ilivyokuwa ikijulikana kwa
watu wengi ndani na nje ya nchi yetu ya Tanzania. Hali hii ya kulifanya jiji la
Arusha kuendelea kupoteza hadhi yake ya kuwa “Geneva of Africa”, inatokana na
wimbi la vikundi vya watu wanaosadikika kuwa vikundi vya kigaidi kuendelea
kutishia amani na utulivu wa jiji hili la Arusha kwa urushaji wa mabomu ya mara
kwa mara.
Siku
chache zilizopita, tulishuhudia kupitia vyombo vya habari juu ya taarifa za shehe
wa msikiti wa Suni kurushiwa bomu akila daku nyumbani kwake maeneo ya Majengo,
mjini hapa. Wakati hilo halijatoka masikioni na akilini mwa wakazi wa Arusha na
Tanzania kwa ujumla, usiku wa kuamkia leo (8/7/2014), tumesikia taarifa kupitia
vyombo vya habari zilizotolewa na msemaji wa jeshi la Polisi nchini, akielezea
kutupwa kwa bomu jingine na kuwajeruhi watanzania wanane wenye asili ya Kiasia
pamoja na watoto wawili katika maeneo ya Gymkana karibu na Mahaka kuu ya
Tanzania kanda ya Kaskazini, mkoa Arusha.
SLPC,
tukiwa ni asasi ya kiraia inayotetea Haki za Binadamu tulizipokea taarifa za
tukio hilo kwa masikitiko makubwa kwani kitendo hicho kinahatarisha Haki za
Binadamu. Kutokana na hali hiyo, SLPC tunazitaka mamlaka husika za ulinzi
kuhakikisha kuwa zinawasaka na kuwakamata wale wote waliohusika katika kitendo
hicho na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kama walivyofanya kwa wale
waliohusika katika tukio jingine la bomu lililorusha katika baa ya Night Park
miezi michache iliyopita mjini hapa. Endapo vyombo vya ulinzi na usalama kwa
kushirikiana na raia, havitafanya jitihada za ziada kukomesha vikundi hivi vya
ugaidi, ni dhahili kuwa raia wasiokuwa
na hatia wataendelea ama kupata ulemavu au kupoteza maisha yao na kukosa Haki
ya Kuishi ambayo ni haki ya msingi ya Haki za Binadamu. SLPC, tunaamini kuwa
vikundi vya ugaidi kama vile Alshababu, Bokoharamu na Al Qaida, vilianza kama
vikundi vidogovidogo na leo ni makundi tishio katika nchi za Kenya, Nigeria na
Iraq. Hivyo basi, SLPC tunaamini kuwa ikiwa kundi hili la watu ambao wanaendela
kutumika katika vitendo hivi vya ugaidi hawatadhibitiwa na hatimaye kutokomezwa
kabisa mapema, ni hakika kuwa wataleta madhara makubwa baadaye si kwa Jiji la
Arusha tu bali kwa Tanzania nzima.
SLPC
tunaamini kuwa vyombo vinavyosimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao, vitahakikisha kuwa kundi hili la watu wachache
wanaohatarisha usalama na Haki za Binadamu, litadhibitiwa mapema kabla
halijaleta madhara makubwa.
SLPC
tunahitimisha kwa kusema kuwa vyombo vya usalama na ulinzi, mwananchi mmoja
mmoja, Asasi za kiraia na Taifa kwa ujumla tuungane kwa pamoja kuhakikisha kuwa
tunawafichua wale wote wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine katika vitendo
hivi vya kigaidi. “Ni ukweli usiopingika kuwa bila usalama, hakuna Haki za
Binadumu”. Aidha, SLPC, tunapenda kuwakumbusha wananchi wa Arusha na Tanzania
kwa ujumla kuwa kulinda, kuhifadhi na kudumisha umoja wa taifa ni wajibu wa
kila raia kama ilivyo katiba yetu ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977, ibara ya 28(1).
Taarifa
hii imetolewa na; MR. MASESA MASHAURI, Mwenyekiti -SLPC,
Simu
Na. 0768 610580.
0 Comments:
Post a Comment