KAMPUNI YA SINGAPORE KUANDAA MASTER PLAN YA ARUSHA NA MWANZA

MKUU WA MKOA WA ARUSHA , MAGESA MULONGO AKIONGEA KWENYE HALFA HIYO

SERIKALI imeipa  kampuni  ya kimataifa ya Surbana International Pty Ltd  ya nchini  Singapore  kazi ya kuandaa  mpango kamambe (master Plan) kwa ajili ya majiji ya Arusha na Mwanza.

Kampuni hiyo inatakiwa kukamilisha shughuli hiyo ndani ya miezi 13 tokea kusainiwa kwa mkataba.

Mkataba huo ulisainiwa juzi jijini hapa na  Katibu mkuu wa wizara wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, Alphayo Kidata,  na Afisa Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Kong Wu Mun.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje na Mambo ya Ndani wa Singapore ,Masagos Zulkiflg walikuwepo kushuhudia tukio hilo la utiaji saini huo .

Pia viongozi waandamizi kutoka Wizarani na halmashauri za majiji ya Arusha na Mwanza waklikuwepo kushuhudia tukio hilo.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Kidata alisema kuwa, tukio hilo ni mwendelezo wa mchakato uliokuwa umeanza  kufuatia mkataba wa makubaliano ambao wizara ya ardhi ilisainiana na Singapore  mwezi  desemba 2013 kwa niaba ya serikali  ya Tanzania.

Alisema kuwa,lengo la kuanzisha mradi huo kuwezesha  miji iliyopangiliwa vizuri na yenye maendeleo na kuondokana na msongamano wa magari pamoja na nyumba zisizokuwa na mpangilio jijini Arusha .

“Kuwepo kwa mpango huu kutawezesha kwa kiasi kikubwa sana kuishi katika mpangilio unaohitajika na kuchangia nchi kupata maendeleo kwa kuwa na miundombinu  ya kutosha katika maeneo yenye mpangilio,” alisema Kidata .

Alisema kuwa wanatarajia kusaini mkataba na kampuni ya China kwa ajili ya kuandaa mpango kamambe kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo inatazamiwa kukua kwa kasi kubwa kutokana na kugunduliwa kwa nishati ya gesi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje na Mambo ya Ndani wa Singapore ,  Zulkiflg  alisema kuwa nchi yake imejikita katika kusaidia mataifa yanayoendelea hasa kwa kuwasaidia kuandaa uwepo wa mipango miji jambo alilodai kuwa itaharakisha maendeleo kwa kuhamasisha uwekezaji toka mataifa mbalimbali.



Sent from my iPhone

0 Comments:

Post a Comment