Kikwete na Wassira, Kinana na vijana wake, mwacheni Mama apumzike
Ni kama vile kunalazimishwa mjadala wa kisiasa, tena ziwe siasa active kweli kweli, kuhusu msiba wa Mama Shida Salum, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na mpiganaji wa haki za makundi maalum katika jamii, ambaye Mwenyezi Mungu amempenda zaidi na akaaga dunia siku ya jana.
Siasa hizi pia zilianza tangu Mama Shida alipokuwa kwenye ‘mapambano’ akipigania afya yake dhidi ya kansa ya shingo ya uzazi. Badala ya kuwa pamoja na familia, kwa mbali na karibu, kumjulia hali na kumtakia kheri mgonjwa, kwao ilikuwa ni wakati wa kufanya sensa.
Mwanzoni siasa hizi zilikuwa zinalazimishwa kupitia kwa wapambe. Wapambe wakaanza kuzungusha maneno mitandaoni (social media) na mazingira fulani fulani hivi yakawa yanalazimishwa, lakini yakifichwa katikati ya mistari na maneno kwenye mainstream media.
Leo zimedhihirika kuwa nyuma yake walikuwepo wakubwa...ukiwa ni mpango wa kitaasisi.
Ni bahati mbaya kwamba siasa za nchi hii zina viongozi wa ajabu kweli kweli. Kitu kibaya kabisa kabisa ni kwamba wanaoziharibu zaidi ni hawa hawa ambao wanakalia ofisi za umma kuongoza nchi kwa niaba ya Watanzania wote.
Kuna wakati unaweza kukubaliana na ile falsafa inayosema kuwa yule mama ntilie, baba ntilie, msukuma mkokoteni au muuza machungwa barabarani au fundi baiskeli ambaye wakati mwingine unampita bila hata kumsalimia au unataka huduma kwake bila hata kumsabahi, angefaa kuwa mbunge au hata waziri kuliko watu wa ajabu ajabu wanaozikalia leo.
Leo asubuhi kupitia vyombo vya habari fulani fulani, waziri anayetegemewa kuwakilisha Serikali ya Rais Kikwete kwenye masuala ya mahusiano katika jamii, Steven Wassira amesikika akitoa kauli za ajabu kabisa ambazo kwa kiwango cha umri wa umbo lake, havikupaswa hata kuwa sehemu ya fikra zake.
Alichokisema akijaribu kuhusisha fikra zake hasi dhidi ya upepo wa mabadiliko unaotishia kumrudisha benchi alikokimbilia wakati Mwalimu Nyerere akingali hai (kwa makosa anayoyajua yeye na waliomrudisha kwenye timu), zimethibitisha maneno fulani niliwahi kuandika siku za nyuma kwamba katika enzi tulizonazo uwezo wa mtu kifikra haupimwi kwa kuangalia mvi na umri pekee.
Wassira anasema ‘Mama Shida Salum amefariki wakati chama chake kikiwa kinapukutika…kiko kwenye makundi mawili’.
Ama unaamini au hupendi, hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya Serikali ya Rais Kikwete kama salaam za pole kwa waombolezaji kutokana na msiba wa Mama Shida Salum!
Kwa wale ambao wamekuwa wakifuatilia siasa za walioko madarakani, kusikia porojo hizi za mtu anayetakiwa kuonesha weledi wa serikali katika kuwasiliana na kujenga mahusiano kwa jamii, wanaweza kusema bila shaka si ajabu maana ‘jasiri haachi asili’.
Ni serikali hii ambayo ilishindwa hata kuinua mdomo wake kutoa pole wala salaam za rambirambi, achilia mbali kuchukua hatua, kwa mauaji ya makusudi na kutisha ya Daudi Mwangosi au Ally Singano Zona.
Ni hawa hawa wamefunika blanketi zito ili kuficha ukweli, haki isipatikane kwa kifo cha Msafiri Mbwambo aliyeuwawa kikatili kwa kuchinjwa kwa msumeno wa umeme na mtu anayedaiwa kuwa kiongozi wa CCM.
Ni hawa hawa kwenye serikali hii hii, kupitia kwa Ndugu Lukuvi, badala ya kutoa pole na salaam za rambirambi kwa Watanzania kutokana na kulipuliwa bomu wakiwa kwenye mkutano wa hadhara eneo la Soweto, Arusha mwaka jana, wakaishia kufanya propaganda za kukimbia hatia iliyokuwa ikiwawinda kimya kimya kutokana na hila walizokuwa wanazijua ndani ya mioyo yao kwa tukio lile.
Kwao, watu hawa ‘wafadhilaka wapundaka’ tukio lile kukatisha maisha ya watoto waliokuwa wametokea madrasa, mama asiyekuwa na hatia, kukata watoto miguu na mikono, kujeruhi vibaya akina mama, vijana, wazee, halikuwa suala la kutosha kuzungumza mambo ya msingi wakati watu wako kwenye majonzi mazito. For them, like then like now (and tomorrow), it was time for utter nonsense for cheap political gains. Say anything, then you do the thinking after.
Kwao kutoa pole na kutuma salaam kwa viongozi wenzao, akiwemo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Arusha Mjini na viongozi wengine wa CHADEMA waliokuwa walengwa pale, ulikuwa ni msamiati ambao mtu anayejishtukia hawezi kuthubutu kuusema.
Labda kwa sababu ya ‘the guilty are always afraid’.
Labda hata jana Wassira akiwakilisha Serikali ya Kikwete, alikuwa ‘akiwindwa’ na sokomoko la moyoni kuhusu mipango ya hila zingine zinazopangwa, ndiyo maana kilichokuwa kikizunguka moyoni mwake ni ‘Chadema, Chadema, Chadema’. Maana mtu asiye makini humtoka mdomoni yaliyomjaa moyoni (heart driven thinking).
Au alikuwa akiwindwa na hofu! Hofu ya mabadiliko. Hofu ya kuondoka, ambayo kwa siku za hivi karibuni imekuwa ikijidhihirisha midomoni mwa walioko madarakani kwa uwazi kabisa.
Ukiogopa sana kitu au hata kinyume chake kwa maana ya kukihusudu, utaishia kukiota au kukiwaza sana. Unaweza kufanya hivyo usingizini au ukiwa unatembea mchana kweupe. Na wakati mwingine hata kama hupendi kuziweka wazi hizo hisia zako unaweza kujikuta umeropoka.
Kama hiyo haitoshi ‘vijana’ wanaofanya kazi kwa maelekezo ya Kinana, nao hawakubaki nyuma, wameeneza kila ambalo ni mtu aso haya pekee anaweza kuthubutu kuandika. Lengo lao, kuweka mbali ushiriki wa CHADEMA na viongozi wake katika hali ya kuugulia maumivu ya ugonjwa aliyokuwa nayo Mama Shida na sasa wakati wa msiba.
Unaweza usiamini, lakini kwa mtu ambaye amekuwa akitumia mikakati ya mtongozwaji aliyekataliwa na hana mbinu mpya kama Kinana, ofisi yake kutuma vijana wafanye kazi hiyo haliwezi kuwa jambo la kukushtua. Unahitaji kuwa na usuli tu mzuri wa mambo kadhaa. Ikiwemo kujua kuwa wapo vijana wa ‘mainstream’ na wengine wako kwenye ‘offshoots’ za CCM.
Kilele cha kazi ya vijana wa Kinana kimeonekana leo kwa kile alichokitoa mdomoni mwake Naibu Katibu Mkuu wa CCM, (anayo majina mengi sana, mengine yanajichanganya huwezi kuwa na uhakika utumie lipi).
Alipopewa fursa ya kuchangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji, neno pekee, kwa kadri ya uwezo wake wa kujua mambo, kutafakari na kusema, lilikuwa ni kuonesha kuwa viongozi wa CHADEMA hawakumjali Mama Shida Salum wakati akingali anaugulia hospitalini. Utter nonsense from the same old man…one of the shameful men CCM does posses as its leaders.
Vijana hawa wa Kinana walitaka kwamba siku ambayo Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alipokwenda kumjulia hali Mama Shida Salum, mjumbe wake wa Kamati Kuu ya chama, angepiga filimbi, miluzi, kuchukua kamera nyingi ili tu ajipatie (kama wafanyavyo wao) ujiko wa kisiasa kwa kutumia wagonjwa.
Vijana hao ambao viongozi wao wamewawakilisha leo hadharani, walitaka kwamba chama kupitia kwa Mwenyekiti Mbowe, kilipotoa mchango wa hali na mali kwa familia ya Mama Shida Salum, ikiwa ni sehemu ya kushirikiana na familia kwenye kumuuguza mama, kingefanya kama wafanyavyo wale ‘wajipigao kifuani au wasimamao njia panda’ ili kila mmoja awaone.
Vijana hawa wanaowakilisha fikra za viongozi wao, walitaka kwamba viongozi mbalimbali wa chama, wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu, watendaji wa chama makao makuu na wabunge waliokuwa wakimjulia na kufuatilia hali ya Mama Shida Salum wakati akiwa nyumbani na hospitalini, kwa mbali au kwa karibu, wangefanya hivyo kwa kupiga tarumbeta na madebe kama vile ni fursa…
Bila shaka walitaka kuona au kusikia mawasiliano yote ya ‘hali na mali’ yaliyokuwa yakifanywa na chama kwa familia, yangelikuwa yakibandikwa pembezoni mwa njia na barabara.
Vijana wa Kinana kwenye Gazeti la Uhuru
Katika hali hiyo hiyo ya ‘kupika’ siasa, CCM kupitia gazeti lao wameamua kufanya ‘uhandisi’ wa habari. Aina hii ya kuandika habari, imekuwa ikifanyika sana kwenye gazeti hilo, kama walivyoendelea leo kwa kuandika ‘Mbowe, Dk Slaa wamkwepa Zitto’.
-Wakacha kuhudhuria mazishi ya mama yake.
Katika Uhandisi (si uandishi) wa habari chombo cha habari hakina haja ya kuzingatia maadili na misingi ya uandishi wa habari, ikiwemo kupata facts za jambo wanalotaka kulitoa kwa umma na kuhakikisha pande zote zinazozungumzwa kwenye hiyo habari zinapata fursa.
Kisemea uongo hicho cha CCM, kilichoko chini ya Ofisi ya Kinana, kama kingekuwa kinafanya uandishi wa habari na kuthamini wajibu wa taaluma hii kwa jamii, kingeweza kujua kwa nini Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na Katibu Mkuu Dkt. Slaa hawakufanikiwa kwenda kumzika Mama Shida Salum, wakalazimika kumtuma Mjumbe wa Kamati Kuu, Waziri Kivuli na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Ezekia Wenje akiambatana na wabunge wengine, kuwakilisha chama kwenye mazishi hayo!
Imenichukua muda sana kuamua kuandika mambo haya, hadi baada ya kuona waliokuwa nyuma ya siasa hizo wakijitokeza wazi na hadharani, tena kupitia watu na vyombo vyao rasmi vinavyowakilisha taasisi yao (CCM). Mambo ya namna hii yanapofanywa na watu wazima wanaopaswa kuwa viongozi, inakuwa ni sawa na ajabu ya Firauni.
Hii nayo ni dalili ya wazi kuwa Serikali na CCM, wanazidi kuchoka. Serikali ikiwa katika hali ya kushindwa, CCM ikiwa kwenye kuporomoka (failing government and falling ruling political party).
Walioko nyuma ya tabia hii ya kufanya hizi siasa kwenye suala hili, wamuache Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, mpiganaji wa haki za makundi maalum katika jamii, Mama Shida Salum apumzike kwa amani mahali pema.
Tusaidie na kuwafariji familia na wafiwa wote, kupata ahueni kwa msiba huu mzito badala ya kuongeza mzigo kwa kuufanyia ‘maneno’ yasiyokuwa na hoja wala haja.
Makene
0 Comments:
Post a Comment