Fwd: MONDULI MAITI YAKAA BARABARANI SAA 18 IKISUBIRI POLISI WA KUPIMA AJALI, YACHUNGUZWA NA DAKTARI HAPOHAPO KISHA YAENDA KUZIKWA




 

MAITI ya Idd Shamba, imekaa barabarani kwa zaidi ya saa 21 ikisubiri kukamilika kwa taratibu za polisi kupima ajali na daktari kuifanyia uchunguzi katika kijiji cha Engaruka wilayani Monduli.

 

Polisi walifika eneo la tukio saa 7 mchana ikiwa ni  saa 18 baada ya kutokea ajali hiyo ambapo baada ya kumaliza kazi yao ya kukagua eneo la tukio maiti hiyo ilihamishiwa chini ya mti wa kivuli kuikinga na jua isiharibike mapema wakati wakisubiri daktari wa kuja kuifanyia uchunguzi.

 

Tanzania Daima ilishuhudia wananchi na viongozi wa Kata ya Engaruka wakiulinda mwili huo wakati wakisubiriwa daktari kutoka Mto wa Mbu kuja kuufanyia uchunguzi mwili huo ambaye naye alifika majira ya saa 10 jioni.

 

Hayo yalitokea Juni 12, mwaka huu baada ya Shamba kudondoka kutoka juu ya mizigo kwenye gari aina ya Toyota DCM, yenye namba za usajili T 995 AMB iliyokuwa ikitokea mnadani Engaruka kuelekea kijiji cha Selela.

 

Diwani wa kata hiyo, Pashet Sengerwan, (CCM), alithibitisha mwili huo wa Shamba kufanyiwa uchunguzi kwenye eneo hilo la ajali kisha kuzikwa siku hiyohiyo juni 13, mwaka huu majira ya saa 11 jioni kwenye makaburi ya kijijini hapo bila kuwasubiri ndugu zake waliokuwa wakitokea Singida kutokana na kukosekana kwa chumba cha kuhifadhia maiti.

Alisema kuwa kabla ya kukutwa na Mauti, shamba alikuwa ni mjasiriamali anayejishughulisha na kuchoma mkaa kijiji hapo ambapo alidai kuwa aliingia kijijini hapo miaka mingi akiwa mtoto mdogo jambo alilodai kuwa hawakuwahi kuwaona ndugu zake.

 

"Jana jioni Iddi aliniaga kuwa tutaonana kesho wakati ametoka dukani kununua "viroba" akaviweka ndani ya koti  kisha akapanda juu ya gari eneo la mizigo wakaondoka ilikuwa kama saa 12 jioni  ndipo baada ya muda tukapata taarifa amedondoka amekufa tukaenda eneo la tukio ikabidi nilipe vijana wa kulinda maiti yake.

 

"Tuliwapigia simu polisi kuwapa taarifa lakini hapa tunategemea polisi wa Mto wa Mbu, ndiyo wamekuja mchana huu na pikipiki, tena nimewasubiri nikaona hawatokei nikaamua kuingia kwenye kikao cha bodi ya elimu pale shule ya sekondari Engaruka wakati tunaanza ndipo wamekuja ikabidi niache nirudi kwenye eneo la ajali.

 

"Kama ulivyoona  Polisi wameshamaliza kazi yao kupima, tatizo limekuja muuguzi wa zahanati ya kijiji chetu amesafiri leo asubuhi ndiyo tumewaomba hawa maafisa kutoka halmashauri wakatuletee daktari kutoka Mto wa Mbu au makuyuni aje afanye kazi kuuchunguza," alisema diwani Sengerwan .

 

Baadaye akizungumza kwa njia ya simu, diwani huyo alisema kuwa walifanikiwa kumzika Shamba majira ya saa 11 jioni kwenye makaburi ya kijiji ambapo wamehifadhi vitu alivyokuwa navyo ikiwemo fedha taslim sh 15,000 ambavyo wanatarajia kuwakabidhi ndugu zake mara atakapofika.

 

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo tayari wameshamuhoji mmiliki wa gari hilo Sauli Kitomari huku wakiendelea na juhudi za kumtafuta dereva wa gari hilo aliyetambulika kwa jina moja la Laning'o ambaye alitoroka baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

 

Akizungumzia uchelewaji wa polisi kufika kwenye eneo la tukio alisema kuwa inawezekana imesababishwa na kukosekana kwa  kituo cha polisi kwenye eneo la Engaruka ambalo pia linatatizo la kukosekana kwa mawasiliano ya simu ambapo huwalazimu watu kwenda umbali wa zaidi ya kilometa 60 karibu na ziwa Engaruka kwa ajili ya kupiga simu.

 

"Nimeshafanya kikao na wananchi wa pale pamoja na diwani wao wamenipa ardhi kwa ajili ya kujenga kituo cha polisi na tayari tumeshafyatua matofali 2,000 muda si mrefu kutoka sasa utaanza tukishirikiana na wananchi," alisema Sabasi.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Monduli, Twalib Mbasha, alisema kuwa hana taarifa ya tukio hilo lakini kwa mujibu wa Sera ya Afya hata muuguzi wa zahanati ya kijiji angekuwepo asingeweza kuufanyia uchunguzi mwili huo kwani shughuli hiyo inapaswa kufanyika kwenye kituo cha afya au hospitali yenye chumba cha upasuaji.

 

Hata hivyo aliahidi kufuatilia tukio hilo ili kujua ni nini hasa kilichotokea na kupelekea uchunguzi huo kufanyikia barabarani.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moduli, Dowika Kasunga, alisema kuwa inawezekana hali hiyo ilisababishwa na tatizo la kukosekana kwa mawasiliano na mamlaka husika kwani kata ya Engaruka ili upige simu  huwabidi kwenda umbali mrefu maeneo karibu na kijiji Selela kutafuta mawasiliano ya simu.

 

Hata hivyo alisema kuwa kwa sasa wanaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mbalimbali ya simu kuona kama kuna uwezekano wa kufunga mnara wa mawasiliano ya simu  kwenye eneo hilo.

 

Naye mwanakijiji wa Engaruka, Labrui Laizer aliieleza Tanzania Daima kuwa kutokana na kukosekana kwa huduma za afya za uhakika kijijini hapo imekuwa ikiwalazimu kusafiri umbali mrefu mpaka Mto wa Mbu kupata matibabu ya uhakika.

Alisema kuwa inapotokea mtu kufariki dunia humzika siku hiyohiyo ili kumuepusha asiharibike kwani hawana chumba cha kuhifadhia maiti kwenye kata hiyo.

 



0 Comments:

Post a Comment