MWAJIRI ARUSHA ADAIWA KUCHAPA WAFANYAKAZI NA UNAODAIWA MKIA WA FARU


WAFANYAKAZI wa kampuni ya Kilimanjaro MilleniumPrinters LTD

inayojishughulisha na utozaji wa ushuru wa maegesho ya magari kwenye
maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha wamelalamikia vitendo vya
unyanyasaji walivyodai kufanyiwa na uongozi wa kampuni hiyo ikiwemo
kuchapwa na mkia wa faru.

Aidha wafanyakazi hao wamedai kuwa walianza kazi kwenye kampuni hiyo
mwanzoni mwa mwezi huu lakini mpaka sasa uongozi wa kampuni hiyo
hautaki kuwaeleza watawalipa mshahara kiasi gani huku wakiwa
wanafanyishwa kazi kuanzia saa 12 asubuhi na muda wa kutoka kazini
ukiwa haujulikani kwani wakati mwingine hukaa mpaka saa tano usiku.

Wakiongea hivi karibuni mbele za ofisi za kampuni hiyo zilizopo eneo
la Kona Nairobi ,Ngarenaro jijini hapa wafanyakazi hao walidai kuwa
waliamua kugoma kufanya kazi ili kushinikiza uongozi kufanyia kazi
madai yao ili waweze kuamua endapo waendelee na kazi au waache.

Akiongea kwa niaba ya wenzake, Ally Abas alisema kuwa wao wamekuwa
wakifanya na kampuni mbalimbali zinazopata tenda ya kukusanya ushuru
kuanzia miaka ya nyuma ambapo kwenye makampuni hayo yote hawakuwahi
kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji kama wanavyofanyiwa na kampuni hiiya
sasa.

Alisema kuwa inashangaza kuona wakati hata hawajui mshahara utakuwa
kiasi gani lakini wameambiwa kuwa atakaeingia kazini baada ya saa 12
asubuhi  kamili atakatwa shilingi 2,000 kwenye mshahara.

“ Hapa tuko zaidi ya wafanyakazi 300 tukishafunga kazi saa 12 jioni
tunarudi hapa ofisini kwa ajili ya kufanya mahesabu, kutokana na wingi
wetu wakati mwingine unakaa mpaka saa tano usiku na hatupewi hata
nauli. Kuna mgambo hapa (Thomas) anatupanga kwenye foleni kwa
kutuchapa na mkia wa faru kwa kweli huu ni unyanyasaji wa hali ya juu”
alilalamika Ally Bakari.
Aidha wafanyakazi hao wamelalamikia kupewa malengo makubwa ya
makusanyo huku wengine wakipangiwa kukusanya maeneo ambayo magari
hayaruhusiwi kuegeshwa wakitolea kuwa wanatakiwa kukusanya mbele ya
benki kuu (BOT) wakati eneo hilo haliruhusiwi kuegesha magari.

Walidai kuwa wengine wamepangiwa kukusanya ushuru kwenye kituo cha
kati cha polisi, eneo la mbele ya chumba cha kuhifadhia maiti cha
hospitali ya mkoa ya Mount Meru, mbele ya  kituo cha mikutano cha
kimaifa cha Arusha, (AICC) ambapo hakuna eneo la kuegesha magari na
eneo mbele ya hoteli ya Impala ambapo hakuna eneo la maegesho ya
magari zaidi ya mzunguko wa magari ya kijenge.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni hiyo, Thomas Munisi alipofuatwa
ofisini na Tanzania Daima akitakiwa kutolea ufafanuzi madai hayo
aliomba apewe muda ili aweze kuwasiliana na watendaji wake kujua
undani wa madai hayo.

0 Comments:

Post a Comment