KAMPENI ya ‘Vua Gamba Vaa Gwanda’ inayoendeshwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) imezidi kushika kasi mkoani Arusha ambapo imefanikiwa kuvuna jumla ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) 68 wakiwemo mabalozi watano kwenye kata ya Magadirisho wilayani Arumeru.
Hayo yalitokea kwenye mkutano wa Chadema uliofanyika kwenye viwanja vya Gengeni ambapo umati mkubwa watu ulijitokeza kwenye mkutano huo uliolenga kuimarisha chama hicho ambao iliongozwa na kada wa chama hicho , James Millya.
Akiongea kwenye mkutano huo, Millya aliwataka wananchi wajiunge na Chadema ili waweze kupigania haki ikiwemo kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali zilizopo nchini kwa kuhakikisha zinatumika kuliendeleza Taifa kwa kile alichodai kuwa harakati hizo hawataweza kuzifanya wakiwa ndani ya CCM kwani imeshindwa kuleta maendeleo kwa miaka 50 iliyokuwa madarakani hivyo kwa sasa hakina jipya.
“Watoto wa maskini kupata nafasi ya uongozi ndani ya CCM ni ndoto, hivyo hata mking’ang’ania huko hakuna mnaloweza kubadilisha, njooni Chadema huku kila mtu mwenye nia na uwezo anapata fursa ya kuchangia, mimi nimejiunga Chadema hivi karibuni lakini nyie mnaona napewa jukwaa nitoe elimu ya uraia, na nyie njooni tuongeze nguvu ya mapambano” alisema Millya.
Kwa upande wake Katibu wa BAVICHA kata , Nuru Ndossi aliwataka wanawake wajitokeze kutoa maoni juu ya katiba mpya pindi tume ya kukusanya maoni itakapopita kwenye maeneo yao ili waweze kutoa maoni yatakayowasaidia kuwapunguzia kero ikiwemo kuondoa sheria kandamizi kwa wanawake hasa kwenye masuala ya umiliki wa rasilimali kama ardhi.
Aliwataka wanawake waamke wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pindi zinapojitokeza ili waweze kuingia kwenye vikao vya maamuzi huku akiwataka wasikubali kuendelea kutumika kama mitaji ya wanasiasa ambao huwathamini wakati wa kampeni lakini zikimalizika huwaacha na kero zao bila kuzitafutia ufumbuzi.
Naye kada wa chama hicho, Chris Mboja aliwahimiza vijana kujiunga kwenye harakati za kisiasa kwa kile alichoeleza kuwa bila hivyo watazidi kulalamikia ugumu wa maisha huku wakiwa hawana suluhisho hivyo akasema njia sahihi ni kujiunga kwenye siasa na kushiriki kwenye mijadala mbalimbali kama ile ya michakato ya katiba mpya, sense na chaguzi zinazokuja siku za usoni.
Akiongea kwa niaba ya wenzake waliojiunga na Chadema, Vicent Mambo alisema kuwa alifikia hatua hiyo baada ya kutafakari na kuona kwa kipindi kirefu CCM imekuwa madarakani lakini haijaweza kupatia wananchi maisha bora kama ilivyoahidi mwaka 2005 kwani maisha yanazidi kuwa magumu huku viongozi wa juu wa chama hicho wakizidi kujilimbikizia mali kupitia ufisadi wanaoufanya.
0 Comments:
Post a Comment