Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Kenan Laban Kihongosi, ameanza rasmi majukumu yake kwa msisitizo mkubwa juu ya kuharakisha maendeleo na kujenga imani ya wananchi kwa Serikali.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi na mtangulizi wake, Paul Makonda, iliyofanyika leo Juni 30, 2025 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Kihongosi amesema kuwa hatakubali vikwazo vyovyote visimamie maendeleo ya wananchi wa Arusha.
"Rais ametuteua au ametutuma kuja kuwatumikia wananchi. Sisi sio mabosi, tumekuja kufanya kazi ya watu na watu wenyewe ndio ninyi mlioko hapa. Mimi niombe ushirikiano wenu ili tuweze kusukuma agenda ya maendeleo mbele," amesema Kihongosi mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali, chama, dini na wananchi waliokusanyika kumshuhudia akipokea ofisi.
Kihongosi ameeleza kuwa uteuzi wake na Rais Samia Suluhu Hassan ni dhamana kubwa, na ameweka wazi kuwa hatarudia maneno ya Rais aliyoyasema hadharani wakati wa uteuzi wake, lakini atayatekeleza kwa vitendo.
"Sina sababu ya kurudia maneno yake, ila ninamaanisha sitaruhusu kikwazo chochote kitakachozuia maendeleo ya wananchi," amesisitiza.
Aidha, amewataka watumishi wa Serikali kushirikiana kwa uaminifu na kufanya kazi kwa bidii, akisisitiza kuwa kila nafasi waliyonayo ni dhamana kutoka kwa wananchi.
"Ajenda yetu ni wananchi kuwa na imani na Serikali. Fedha zinaletwa, miradi inajengwa na wajibu wetu ni kusimamia kikamilifu hadi kukamilika," amesema.
Katika hotuba yake, Kihongosi pia ametoa wito wa kuishi kwa upendo na kuepuka migogoro isiyo na tija.
"Mungu kila mmoja amemuandikia nafasi yake. Huna sababu ya kugombana au kuumiza watu. Tumuachie Mungu atimize alichopanga," amehimiza.
Akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye hafla hiyo, Kihongosi amewakumbusha mchango alioutoa kipindi alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, ikiwemo kushirikiana nao katika miradi ya elimu, na kuwaomba waendeleze ushirikiano huo.
"Asitokee mtu akawaambia msishirikiane na Serikali yenu. Serikali ndiyo jicho na msaada wa mwisho kwa wananchi," amesema.
Kwa upande wake, Paul Makonda ambaye sasa anaaga rasmi nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, amempongeza Kihongosi na kuahidi kuendelea kumpa ushirikiano.
"Nitampatia ushirikiano katika kila jambo atakalohitaji kutoka kwangu bila kujali umri au kwamba nimemtangulia kuingia kwenye uongozi Serikalini," amesema Makonda.
Aidha, amewataka wananchi wa Arusha waendelee kutoa ushirikiano kwa Mkuu wao mpya ili kufanikisha majukumu aliyopangiwa na Rais.
Katika hatua nyingine ya siku hiyo, Mkuu wa Mkoa Kihongosi aliwaapisha rasmi wakuu wapya wa wilaya walioteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Miongoni mwao ni Mwinyi Ahmed Mwinyi aliyeapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na
Hafla hiyo ya kihistoria ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, chama, dini, mila, watumishi wa umma pamoja na mamia ya wananchi waliokuwa na shauku ya kumpokea Kihongosi kwa nderemo na vifijo, wakionesha matumaini mapya kwa maendeleo ya Mkoa wa Arusha.















0 Comments:
Post a Comment