RAIS SAMIA: UHURU WA HABARI, MAONI NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA NI ISHARA YA DEMOKRASIA INAYOKUA

 


“Uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao umeongezeka,” alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alipohutubia Bunge la 12 jijini Dodoma tarehe 27 Juni 2025. 



Akitolea mfano ongezeko la majukwaa ya habari nchini, Rais Samia alieleza kuwa hatua hizo zinaashiria ukuaji wa demokrasia na utawala bora nchini.



“Tunathamini na kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari,” alisisitiza, akionesha dhamira ya serikali kulinda na kuimarisha uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa.



Katika hatua nyingine, Rais Samia aligusia suala nyeti la mchakato wa katiba mpya ambao kwa muda mrefu umekuwa ukisubiriwa na wananchi. “Mchakato wa katiba mpya ni miongoni mwa ahadi ambazo zinaonekana katika ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2025/2030,” alisema, akieleza kuwa serikali inatambua umuhimu wa kuwa na katiba inayoendana na wakati na matakwa ya Watanzania.



Mageuzi ya Kidemokrasia: Tume Huru ya Uchaguzi

Katika hotuba hiyo, Rais Samia alieleza mafanikio ya kisiasa yaliyopatikana kupitia kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, jambo alilolitaja kuwa la kihistoria.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliundwa kwa sheria yake yenyewe ili kujibu rai ya muda mrefu ya wadau wa siasa nchini,” alisema.

Aliongeza kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu yamekamilika na wananchi wameonesha ushiriki mkubwa. “Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itatangaza hivi karibuni tarehe ya siku ya uchaguzi, zoezi la uandikishaji limeshakamilika nchi nzima. Sote tumeshuhudia mwitikio mzuri wa wananchi kujitokeza kwenye vituo vya wapiga kura,” alisema.

Uchumi: Ukuaji, Pato la Taifa na Mfumuko wa Bei

Katika sekta ya uchumi, Rais Samia alitangaza ongezeko la pato ghafi la taifa na utulivu wa mfumuko wa bei.

“Pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021 hadi kufikia trilioni 205.84 mwaka 2024,” alisema.

Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), “Kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania mwaka 2025 inatarajiwa kufikia asilimia 6,” alisema Rais Samia.

Alieleza kuwa Tanzania imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei chini ya asilimia 5 kwa miaka minne mfululizo. “Mfumuko wa bei tulionao ni miongoni mwa viwango bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na upo chini ya wastani wa mfumuko wa bei Barani Afrika,” alisema.

Hali hiyo imechangiwa na utekelezaji wa sera madhubuti na upatikanaji wa chakula kwa wingi sokoni.

Biashara ya Kimataifa na Akiba ya Dhahabu

Akigusia biashara ya nje, Rais Samia alieleza kuwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameongezeka kwa kiwango kikubwa.

“Mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 6.39 mwaka 2021 hadi kufikia dola bilioni 8.7 mwaka 2024,” alisema.

Aliongeza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza kununua na kuhifadhi dhahabu kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha uchumi wa taifa.

“BoT imeweza kununua na kuhifadhi akiba ya dhahabu yenye thamani ya trilioni 3.424. Hadi sasa tayari dhahabu yenye thamani ya shilingi bilioni 702.3 imenunuliwa na ununuzi unaendelea,” alisema.

Kodi na Mapato ya Ndani

Katika hotuba hiyo, Rais Samia alieleza msimamo wake juu ya ukusanyaji wa kodi, akisisitiza umuhimu wa kutoa elimu badala ya kutumia nguvu.

“Napendelea kuona wafanyabiashara na wawekezaji wanaelimishwa kuhusu umuhimu wa kodi badala ya kutumia nguvu katika ukusanyaji wake,” alisema.

Alieleza kuwa serikali imeimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki, na kuongeza uwezo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Jitihada hizo zimechangia kuongeza mapato ya ndani kwa mwezi kutoka shilingi trilioni 1.51 mwezi Novemba 2020 hadi kufikia trilioni 3.09 mwezi Machi 2025,” alisema.

Hotuba ya Rais Samia mbele ya Bunge la 12 imebeba ujumbe wa matumaini kwa Watanzania, ikionesha dira ya serikali katika kukuza demokrasia, haki za kiraia, na ustawi wa kiuchumi. Kwa kuzingatia ahadi ya mchakato wa katiba mpya, uhuru wa habari, na mafanikio ya kiuchumi, taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 likiwa na msingi wa matumaini na mwelekeo wa maendeleo ya pamoja.

0 Comments:

Post a Comment