Fungashada: Wito wa Kutangaza Janga la Kitaifa Unapamba Moto

 
Wataalamu wa kilimo na wadau mbalimbali wameitaka serikali kulitangaza rasmi ugonjwa wa Fungashada unaoshambulia migomba, kama janga la kitaifa, wakieleza kuwa hali hiyo itasaidia kuongeza jitihada za kudhibiti maambukizi na kulinda zao hilo muhimu kwa usalama wa chakula na kipato cha wakulima.


Hemadi Msofe, mchambuzi wa mbegu na mtaalamu kutoka Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), alisema kuwa uzalishaji wa mbegu bora za migomba bado uko chini kutokana na ukosefu wa wazalishaji wa kutosha pamoja na rasilimali.
“TOSCI ilianza kuandaa viwango tangu mwaka 2020 kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha mbegu bora zinapatikana,” alifafanua.
Kwa upande wake, Filbert Luhunga kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) aliwahimiza wakulima kutumia taarifa za kisayansi kufanya maamuzi sahihi, huku akitoa tahadhari dhidi ya matumizi ya miche isiyothibitishwa.
“Matumizi ya miche isiyokaguliwa ndiyo chimbuko la maambukizi mapya,” alisema.
Katika kuonyesha uzito wa tatizo hili, mmoja wa wataalamu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea Tanzania (TPHPA), ambaye hakutaka jina lake litajwe, alieleza kuwa bado kuna mapungufu ya kimkakati katika kukabiliana na janga hilo.
“Tunaendelea kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili kama USAID. Hatujaitangaza BBTV kama janga la kitaifa, na huo ni udhaifu mkubwa wa kimkakati,” alisema.
Aidha, Godfrey Amba, mkulima kutoka Kata ya Kauzeni, Manispaa ya Morogoro, alisema kuwa ugumu wa kupata miche bora umesababisha kuenea kwa kasi kwa magonjwa ya migomba.
“Tunahitaji msaada wa haraka kutoka serikalini ili kulinda zao hili muhimu,” alisema.
Kwa sasa, kila mgomba unaoambukizwa ni sahani ya chakula inayopotea, kipato kinachofifia, na familia inayosogea karibu zaidi na umaskini. Wadau wanaamini kuwa hatua ya kuitangaza rasmi Fungashada kama janga la kitaifa itafungua milango ya rasilimali, mafunzo, na teknolojia itakayosaidia kupambana na ugonjwa huo kwa mafanikio.

0 Comments:

Post a Comment