“Bajeti hii imezingatia utekelezaji wa vipaumbele vingine ikiwemo ujenzi na ukarabati wa viwanja mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pamoja na ukamilishaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati” alisema Dkt. Nchemba.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 yenye thamani ya shilingi trilioni 56.49. Kati ya wabunge wote, zaidi ya 373 sawa na asilimia 98.7 walipiga kura ya ndiyo kuidhinisha bajeti hiyo.
Akihitimisha hoja za bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alisisitiza kuwa bajeti ya mwaka 2025/26 imejielekeza katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati, maandalizi ya michuano ya AFCON 2027, na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao.
“Serikali itaendelea kuhakikisha kupitia Bajeti hiyo ya 2025/26, malengo ya ukuaji wa uchumi yatafikiwa kwa kuzingatia utekelezaji madhubuti wa miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo (FYDP III), ikiwemo miradi ya kielelezo na kimkakati” alisema Dkt. Nchemba.
Akiendelea kuwasilisha vipaumbele vya Serikali, Dkt. Nchemba alieleza kuwa kiasi cha shilingi trilioni 10.24 kimetengwa kwa ajili ya sekta za uzalishaji ili kuchochea uchumi na kutoa ajira kwa wananchi.
“Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo, kwa mwaka 2025/26, Serikali imetenga jumla ya shilingi trilioni 1.9 kwa ajili ya sekta hiyo, sawa na ongezeko la asilimia 203.6 kutoka bajeti ya mwaka 2021/22” alibainisha.
Katika hatua nyingine, Serikali imejipanga kudhibiti mfumuko wa bei nchini kwa kuimarisha sekta za uzalishaji, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuongeza matumizi ya nishati mbadala.
“Tutahakikisha tunapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani hasa kwenye bidhaa kama mafuta ya kula, sukari, mbolea na gesi asilia” alieleza Dkt. Nchemba.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wabunge wote waliochangia bajeti hiyo kwa njia ya maandishi na kwa maneno.
“Tunathamini michango yote iliyotolewa kutokana na tija yake katika kujenga uelewa wa pamoja na kutanguliza vipaumbele vya wananchi tunaowawakilisha kwa maslahi mapana ya Taifa letu” alisema Dkt. Nchemba.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa bajeti na mipango mbalimbali ya maendeleo ni ushahidi kuwa Serikali imetekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya CCM ya mwaka 2020.
“Kitu kimoja ambacho ni dhahiri kama walivyochangia waheshimiwa wabunge ni kuwa hatuna deni na MAMA hasa baada ya kukamilisha yale yote yaliyoainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020” aliongeza Dkt. Nchemba.
Bajeti ya mwaka 2025/26 inatarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani ya shilingi trilioni 40.47, misaada ya shilingi trilioni 1.07, na mikopo ya shilingi trilioni 14.95. Mapato ya kodi yanakadiriwa kufikia shilingi trilioni 32.31, yasiyo ya kodi trilioni 6.48, na ya Serikali za Mitaa trilioni 1.68.
Katika matumizi, Serikali imepanga kutumia shilingi trilioni 7.71 kwa stahiki za watumishi na pensheni, trilioni 7.81 kwa ununuzi wa bidhaa na huduma, na trilioni 6.49 kulipa riba za mikopo. Ruzuku kwa taasisi za Serikali na mashirika ya umma zimetengewa shilingi trilioni 23.04, huku shilingi trilioni 7.72 zikitengwa kwa malipo ya mtaji kwa deni la ndani na nje.
“Waheshimiwa Wabunge mtakumbukwa sana kwa kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kusukuma gurudumu la maendeleo kwa nchi yetu, hususan kupitia utekelezaji wa miradi yenye matokeo chanya katika sekta mbalimbali za kiuchumi” alihitimisha Dkt. Nchemba.


0 Comments:
Post a Comment