CCM Yasitisha Mikutano kwa Muda, Yajipanga kwa Kura za Maoni


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesitisha kwa muda ziara, mikutano, makongamano na semina zote zinazohusisha wajumbe wa vikao vya kupiga kura za maoni kwa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi, ili kutoa fursa ya maandalizi ya mchakato wa ndani ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.



“Nimesimama hapa kuwaeleza tutasimama kwa muda kwa maandalizi ya kura za maoni ndani ya chama,” alisema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, Juni 24, 2025, katika mkutano wa hadhara mjini Dodoma.

Akiwa katika ziara yake ya siku tatu, Makalla alieleza kuwa uamuzi huo unalenga kutoa nafasi kwa viongozi wa ngazi zote ndani ya chama, kuanzia mabalozi wa mashina hadi kamati za siasa za mikoa, kujiandaa kikamilifu kwa mchakato wa kura za maoni.

“Mabalozi ni watu muhimu, ndio wako kule, ndio wana wanachama. Tuwape nafasi kuandaa mazingira kuelekea kura za maoni. Viongozi wa matawi, kata, wilaya na mkoa nao wapate nafasi ya kujiandaa kuratibu,” alisema Makalla.



Uamuzi huo wa kusitisha shughuli umetangazwa rasmi kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ambapo alifafanua kuwa hatua hiyo ni ya kiutaratibu na inalenga kudumisha nidhamu na utulivu katika mchakato wa uchaguzi wa ndani wa chama.

“CCM inaendelea kusisitiza kuwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake kuepuka kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri kuwa ni kinyume cha katiba, kanuni na miongozo ya chama chetu,” alisisitiza Balozi Dk. Nchimbi.

Kwa mujibu wa chama hicho, usitishaji huo unahusu shughuli zote zinazohusisha wajumbe wa vikao vinavyopaswa kupiga kura za maoni katika ngazi zote, na utaendelea hadi pale mchakato wa kura za maoni utakapokamilika.

Makalla alisisitiza kuwa muda uliopo ni mchache, na hivyo ni muhimu kutoa nafasi kwa maandalizi ya kina badala ya kuendelea na shughuli nyingine ambazo zinaweza kuwahusisha wajumbe wa vikao muhimu.

“Muda hauko upande wetu, tunasitisha ziara hizi ili kutoa nafasi ya maandalizi ya mchakato ndani ya chama chetu. Maana hawa tukiwa tunawaita mara kwa mara watakosa muda wa kufanya maandalizi,” alisema.

Uamuzi huu ni sehemu ya maandalizi makini ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku chama hicho kikisisitiza nidhamu, uwazi na utii kwa taratibu za ndani kama msingi wa ushindani wa haki na maendeleo ya kidemokrasia ndani ya chama.

0 Comments:

Post a Comment