Kikosi cha Klabu ya Simba kinatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya mchezo muhimu wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya RS Berkane utakaochezwa Mei 17, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika na msafara wa timu hiyo utaongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA.
"Tutaondoka kesho alfajiri, kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wetu huo, tukiwa na malengo ya kushinda mchezo huo, wenye kauli mbiu Tunabeba," amesema Ahmed Ally.
Ameeleza kuwa msafara huo utajumuisha wachezaji 24 pamoja na benchi la ufundi, huku idadi ya mashabiki watakaosafiri pamoja na timu hiyo ikitarajiwa kutangazwa kabla ya kuondoka.
Aidha, Ahmed Ally amesema kuwa wanatarajia mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa RS Berkane ambao tayari wamecheza fainali nne na kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo.
"Mchezo huu utakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu RS Berkane ni timu yenye uzoefu mkubwa katika michuano hii, lakini sisi tumejipanga kuhakikisha tunashinda," amesema.
Pamoja na mchezo huo wa Mei 17, Simba pia itakuwa na faida ya kucheza mchezo wa marudiano nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Mei 25, 2025. Ahmed amesema wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye michezo yote miwili.
Kwa upande wa mashabiki wanaotaka kusafiri pamoja na timu hiyo kwenda Morocco, Ahmed Ally amesema gharama ni Dola za Kimarekani 1,200 kwa kila mtu, kiasi ambacho kinajumuisha malazi, usafiri, na bima ya afya.
"Kila shabiki anayehitaji kusafiri anapaswa kulipa Dola 1,200 ambazo zitahusisha siku zote watakazokaa nchini humo, ikiwa ni pamoja na malazi, usafiri na bima ya afya," amefafanua.
Simba SC inasaka taji lake la kwanza la Kombe la Shirikisho baada ya kufika hatua ya fainali, na mashabiki wa timu hiyo wana matumaini makubwa kuwa mwaka huu utaandika historia mpya kwa klabu hiyo kongwe Tanzania.

0 Comments:
Post a Comment